Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Miradi ya maendeleo yaahirisha Tamasha la Kizimkazi

Mwenyekiti wa Tamasha la Kizimkazi, Mahfoudh Said Omar akizungumza na waandishi wa habari kuhusu kuahirishwa kwa Tamasha hilo kwa mwaka huu lililokuwa limepangwa kufanyika Julai 19 hadi 26 katika eneo la Sports Samia Academy Kizimkazi Mkao wa Kusini Unguja. Picha na Jesse Mikofu

Muktasari:

  • Tamasha hilo lilipangwa kufanyika kwa siku nane kuanzia Julai 19 hadi 26 mwaka huu katika uwanja wa Sports Suluhu Academy Kizimkazi, lakini kutokana na kukosekana miradi ya kufunguliwa.

Unguja. Tamasha la Kizimkazi limeahirishwa sababu kubwa ikitajwa ni kukosekana kwa miradi ambayo itafunguliwa wakati wa tamasha hilo.

Kwa mujibu wa taarifa iliyokuwa imetolewa awali Juni 15 mwaka huu,  tamasha hilo la 10 lilitarajiwa kuanza Julai 19 hadi 26 mwaka huu.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Julai 3, 2025 Kizimkazi Mkoa wa Kusini Unguja, Mwenyekiti wa Tamasha hilo, Mahfoudh Said Omar amesema tamasha hilo lina malengo mengi, lakini kubwa zaidi ni kuhamasisha miradi ya maendeleo.

"Kwa hiyo mwaka huu hatuna miradi, kwa sababu ya kukosa miradi ya maendeleo ya kufungua imebidi tuahirishe mpaka itakapopangwa tena mwakani," amesema Mwenyekiti huyo

Katika tamasha hilo ambalo lilianza tangu mwaka 2015 katika ngazi ya shehia hadi kufikia kitaifa, huwa inazinduliwa miradi mbalimbali ya maendeleo zikiwemo shule, vituo vya afya, na kuwajengea uwezo wajasiriamali.

Katika tamasha la mwaka huu sekta saba zilikuwa zimepangwa kufikiwa kwa kuwajengea uwezo wananchi na kukuza biashara zao kupitia sekta hizo za uvuvi, kilimo, ufugaji, utalii na elimu.

Pia, malengo mengine ya tamasha hilo huwa ni kuwaunganisha wana-kizimkazi, kulinda na kuendeleza mila na desturi za mkoa huo na kutangaza fursa za uwekezaji zilimo katika mkoa huo.

Kutokana na kuahirishwa kwa tamasha hilo, mwenyekiti Mahfoudh amesema ni hasara sio tu kwa wadhamini ambao walikuwa tayari wameshajitokeza kulidhamini, lakini pia ni hasara kwa kamati ya tamasha hilo na wananchi kwani walikuwa wameshajiandaa na fursa zinazopatikana sambamba na kupoteza burudani mbalimbali za asilia.

Hata hivyo, mwenyekiti huyo hakutaja ni hasara kiasi gani itapatikana.  

"Ule utamu tuliouzoea tunakwenda kuukosa mwaka huu, ni hasara, lakini ndio hivyo hakuna namna tutajipanga kwa wakati mwingine.

Miongoni mwa miradi ambayo imetajwa ilitarajiwa kuzinduliwa, lakini haijakamilika ni pamoja na uwanja wa mpira wa kisasa wa Suluhu Academy.

Mingine ni mradi wa kiwanja cha kufurahishia watoto, mradi wa maji na uzinduzi wa Ofisi za matawi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM). Hata hivyo hakutaja gharama za miradi hiyo.

Baadhi ya wananchi wa Kizimkazi wamesema kuahirishwa kwa tamasha hilo ni pigo kubwa kwao kwani walikuwa tayari wamejiandaa na kuandaa biashara zao kwa ajili ya kuuza.

Mwachumu Ali Shaka Sheha wa Shehia ya Kizimkazi Mkunguni, amesema ni kilio kwa wananchi maana walikuwa tayari wamejiandaa kwa mambo mbalimbali zikiwemo fursa za biashara.

"Lakini, hakuna namna maana yote yanapangwa na Mungu inshallah tutangoja lijalo," amesema.

Naye mkazi wa Kizimkazi, Tatu Mussa Haji amesema wamepata mshtuko kuahirishwa kwa tamasha hilo kwani wamezoea kila mwaka kusherehekea na kupata wageni mbalimbali kupitia tamasha hilo.

Tamasha hilo lilianzishwa na Rais Samia Suluhu Hassan wakati alipokuwa Makamu wa Rais katika ngazi ya Shehia, lakini likaendelea kukua na kupata hadhi hadi ngazi ya kitaifa.

Wakati akilifunga tamasha hilo mwaka jana, Rais Samia alisema limekuwa kubwa kwa hiyo linakwenda kuwa la kimataifa na wataliondoa kwa wananchi badala yake litaanza kuratibiwa kitaifa.