Utafiti wafichua makundi yanayoongoza Ukimwi Z’bar

Makamu wa Kwanza wa Rais Othman Masoud akizungumza wakati wa maadhimisho ya siku ya Ukimwi Duniani yaliyofanyika Nungwi Mkoa wa Kaskazini Unguja.

Muktasari:

  • Utafiti mpya wa 2023 unaohusu hali ya maambukizi ya Virusi Vya Ukimwi (VVU) Visiwani Zanzibar, unaonyesha kundi la wanaofanyabiashara ya ngono, ndilo linaloongozwa.

Unguja. Utafiti mpya kuhusu mwenendo ugonjwa wa Ukimwi visiwani Zanzibar, umebainisha makundi matatu yanayoongoza kwa maambukizi ya Virusi Vya Ukimwi (VVU), huku wanawake wanaouza miili yao, wakitajwa kuongoza.

Haya yamebainishwa leo Ijumaa Desemba Mosi, 2023 na Makamu wa Kwanza wa Rais, Othman Masoud wakati wa maadhimisho ya Siku ya Ukimwi Duniani yaliyofanyika kitaifa visiwani humo  kwenye eneo la Nungwi, Mkoa wa Kaskazini Unguja.

Utafiti huo wa 2023 uliofanywa na Tume ya Ukimwi Zanzibar (ZAC), umeonyesha wanawake wanaofanya biashara ya kuuza miili yao wanaoongoza kwa asilimia 21.1.

Aidha, utafiti huo pia umeonyesha wanaume anaoshiriki mahusiano yasiyofaa  wakiwa ni  asilimia 11.2; huku waraibu wa dawa za kulevya wakichukua asilimia 9.4.

Wakati kesi tatu za kwanza za Ukimwi zilipogundulika visiwani humo, mwaka 1986, maambukizi ya VVU yalikuwa chini ya asilimia 1.

Ni kwa sababu hiyo, Othman amezitaka taasisi zinazohusika na masuala ya Ukimwi, Wizara ya Afya na wadau wa maendeleo kwa pamoja kuingiza kwenye mipango yao namna ya kushughulikia tatizo hilo, ili kuendana na mkakati wa kutokomeza Ukimwi ifikapo 2030.

“Inaonekana tabia hatarishi na maambukizi kwa baadhi ya mikoa yanaendelea kuongezeka jambo ambalo linahitaji juhudi zaidi ya kila mmoja, ili kuondokana na hali hiyo,” amesema Othman.

Kwa mujibu wa utafiti huo, watu 10, 580 sawa na asilimia nne ya Wazanzibar (milioni 1.8), wanaishi na VVU, kiwango ambacho kinatajwa kuwa kikubwa cha mabukizi ikilinganishwa na idadi ya watu waliopo.

Othman amesema kwa mujibu wa utafiti huo, Unguja ina maambukizi makubwa ya asilimia 0.5 ikilinganishwa na Pemba yenye maambukizi ya asilimia 0.3, huku Mkoa wa Kusini Unguja ukiongoza kwa asilimia 0.8, ukifuatiwa na Mkoa wa Kaskazini Unguja wenye maambukizi ya asilimia 0.7.

Kwa upande wa Mwakilishi wa Jumuiya ya Watu Wanaoishi na Virusi Vya Ukimwi Zanzibar (Zapha+), Sara Abdi amesema kuna haja ya Serikali kuziwezesha kamati za Ukimwi katika ngazi za Shehia na Wilaya, ili ziweze kufanya kazi kwa ufanisi,  na kufikia malengo wanayowekwa.

Naye Mwenyekiti wa Bodi ya ZAC, Dk Ali Salim amesema kazi kubwa ya uhamasishaji inafanyika na mwaka huu wananchi 80,760 wamejitokeza kupima afya zao, kati yao 404 waligundulika kuwa na VVU.

“Katika jitihada hizo, wote walioorodheshwa kwenye vituo vya matibabu wanaendelea kutumia dawa za kufubaza virusi, hii itasaidia kudhiti tatizo hili hususani maambukizi mapya,” amesema Dk Salim.

Akitoa salamu za Umoja wa Mataifa (UN), Mwakilishi wake, George Weiy amesema maadhimisho hayo ni kwa ajili ya kuonyesha mshikamano na kuungana na wanaoishi na virusi, pia ni fursa ya kujitathmini na kufanya kazi kwa karibu zaidi na watu, ili maradhi hayo yasiwe kikwazo kwa maendeleo yao.