Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Wahitimu kidato cha sita waitwa maonesho ya elimu ya juu Zanzibar

Wanafunzi wakiwa katika banda ya Taasisi ya Global Education Link wakipata miongozo mbalimbali namna ya kujiunga na vyuo vya elimu ya juu nje ya nchi

Muktasari:

  • Hatua hiyo itawasaidia kupata taarifa za namna ya kujiunga na vyuo vya ndani na nje ya nchi kwa kukutana na wataalamu mbalimbali.

Unguja. Wanafunzi waliohitimu kidato cha sita wamehimizwa kutumia Maonyesho ya Wiki ya Elimu ya Juu Zanzibar 2026 kupata taarifa kuhusu fursa za kujiunga na vyuo vikuu, mikopo ya elimu na udhamini wa masomo unaotolewa ndani na nje ya nchi.

Akizungumza katika maonyesho hayo leo Jumapili, Julai 19, 2026, Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi, Mohamed Abdulla, amesema Serikali imewaleta pamoja wadau wa elimu ili kurahisisha upatikanaji wa taarifa kwa wanafunzi na wazazi.

"Waje wajionee fursa zilizopo. Kuna taasisi zaidi ya 84 za elimu zinazoshiriki maonyesho haya, hivyo wanafunzi watapata nafasi ya kujifunza na kufanya maamuzi sahihi kuhusu masomo yao ya baadaye," amesema.

Kwa upande wake, Taasisi ya Global Education Link imewahimiza wanafunzi wa Zanzibar kutembelea banda lake ili kupata huduma za udahili wa papo kwa papo, ushauri wa kitaaluma, pamoja na taarifa kuhusu mikopo na udhamini wa masomo.

Meneja wa Tawi la Zanzibar wa taasisi hiyo, Zulfiya Labhulal, amesema tangu maonyesho hayo yaanze Julai 14, zaidi ya wanafunzi 250 wametembelea banda hilo na kunufaika na huduma mbalimbali za ushauri wa elimu.

Amesema wanafunzi wanaotaka kujiunga na vyuo vikuu wanashauriwa kufika wakiwa na vyeti vyao, ili wapate udahili wa moja kwa moja na maelekezo kuhusu taratibu za kuomba mikopo ya elimu na udhamini.


"Mwanafunzi anayefika kwenye banda letu tunahakikisha anaondoka akiwa amepata udahili na maelekezo muhimu kuhusu hatua zinazofuata katika safari yake ya elimu," amesema.

Ameongeza kuwa taasisi hiyo inaendelea kushirikiana na vyuo vya ndani na nje ya nchi ili kuwaunganisha wanafunzi na programu za masomo zinazowaandaa kwa soko la ajira na kujiajiri.

Labhulal amesema maonyesho hayo pia yanawapa wanafunzi nafasi ya kukutana na wawakilishi wa vyuo vya kimataifa, kupata taarifa kuhusu kozi mbalimbali, utaratibu wa kujiunga na maandalizi ya kwenda kusoma nje ya nchi.

Kwa mujibu wake, baadhi ya wanafunzi wanaweza kupata udhamini wa masomo wa kati ya asilimia 50 na 100, kulingana na sifa na vigezo vya vyuo husika.

Mshauri wa wanafunzi wa Global Education Link Zanzibar, Said Suleiman, amesema maonyesho hayo ni fursa muhimu kwa wanafunzi na wazazi wanaojiandaa na mwaka wa masomo wa 2026/27.

Amesisitiza umuhimu wa wanafunzi kupata ushauri wa kitaaluma kabla ya kuchagua kozi ili uamuzi wao uendane na uwezo, mchanganyiko wa masomo waliyosoma na malengo yao ya baadaye.

Kwa upande wake, Meneja Mwandamizi wa Udahili wa Kimataifa wa Chandigarh University ya India, Harsimran Singh, amesema chuo hicho kinaendelea kuwapa wanafunzi wa kimataifa, wakiwemo wa Zanzibar, fursa za kujiunga na programu za shahada, uzamili na uzamivu, pamoja na udhamini wa masomo.

Amesema chuo hicho kina mazingira bora ya kujifunzia, maabara za kisasa na ushirikiano wa karibu na sekta za viwanda na biashara ili kuwajengea wanafunzi ujuzi unaohitajika katika soko la ajira duniani.

Naye Mkurugenzi wa Idara ya Elimu ya Sekondari katika Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Asya Issa, amewataka wanafunzi kutumia maonyesho hayo kupata ushauri wa kitaaluma, kujifunza namna ya kufungua akaunti za mikopo na kufahamu taratibu za kujiunga na vyuo vikuu.

"Akifika hapa mwanafunzi ana nafasi ya kuzungumza na wataalamu na kupata ushauri wa kuchagua kozi inayolingana na ndoto na malengo yake," amesema.

Maonyesho ya Wiki ya Elimu ya Juu Zanzibar 2026 yamewakutanisha taasisi mbalimbali za elimu ya juu kutoka ndani na nje ya nchi kwa lengo la kuwapatia wanafunzi, wazazi na wadau wa elimu taarifa kuhusu udahili, mikopo, udhamini na fursa nyingine za masomo.