Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Wazazi wanavyopambania elimu ya mtoto wao asiyeona kama wao

Khamis Hassan Makame mwenye ulemavu wa kuona  akizungumza kuhusu changamoto za upatikanaji wa elimu kwa watu wenye mahitaji maalumu katika wilaya ya Kaskazini B Mkoa wa Kaskazini Unguja. Picha na Jesse Mikofu

Muktasari:

  • Masafa marefu na changamoto za usafiri vinaingilia ndoto za watu wenye ulemavu kutoka Mkoa wa Kaskazini Unguja kufuata elimu jumuishi kwenye shule ya Kisiwandui iliyopo Mkoa wa Mjini Magharibi

Unguja. Kila alfajiri, saa mbili asubuhi, Khamis Hassan Makame husimama kando ya barabara eneo la Kitope, Wilaya ya Kaskazini B, akisubiri daladala kwenda Shule ya Mjumuisho ya Kisiwandui, iliyopo Mkoa wa Mjini Magharibi. Mkono mmoja hushika fimbo yake ya kumwongoza kwa kuwa ana ulemavu wa kuona, huku mkono mwingine ukimshika mkono mtoto wake anayesoma darasa la maandalizi, ambaye naye ana ulemavu wa kuona.

Safari hiyo si ya hiari, bali ni matokeo ya ukosefu wa shule ya elimu jumuisho katika Mkoa wa Kaskazini Unguja, hali inayowalazimu wazazi wa watoto wenye mahitaji maalumu kusafiri umbali mrefu kila siku ili watoto wao wapate haki ya elimu.

Khamis na mkewe wote ni wenye ulemavu wa kuona. Licha ya changamoto walizopitia maishani, wameamua kupigania ndoto ya mtoto wao wa kwanza asikose elimu kutokana na ulemavu wake.

"Nina kipato kidogo, lakini kila siku natumia zaidi ya Sh4,000 kwa nauli kumpeleka na kumrudisha mtoto wangu. Ana uwezo wa kujifunza, lakini wakati mwingine najiuliza nitaweza kubeba gharama hizi hadi lini?" anasema Khamis.

Anasema changamoto si gharama za usafiri pekee, bali pia namna wanavyotendewa wanapokuwa safarini.

"Wakati mwingine makondakta wanapotuona wenye fimbo za kuongozea hutwambia hakuna nafasi, ilhali daladala halijajaa. Hali hiyo hutufanya tujisikie tumetengwa kwa sababu ya ulemavu wetu," anasema.

Khamis anakumbuka pia changamoto alizokutana nazo alipokuwa mwanafunzi wa Shule ya Msingi Kitope, ambako hakukuwa na walimu wenye taaluma ya elimu maalumu wala vifaa vinavyokidhi mahitaji ya wanafunzi wasioona.

"Tulichanganywa na wanafunzi wengine bila kuzingatia mahitaji yetu katika ufundishaji. Ningependa watoto wa sasa wapate mazingira bora kuliko tuliyokuwa nayo sisi," anasema, huku akiiomba Serikali kujenga shule au madarasa ya elimu mjumuisho karibu na maeneo wanayoishi.

Hata hivyo, akizungumzia changamoto hiyo, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Lela Mohamed Mussa, anakiri kuwa changamoto hiyo ipo katika baadhi ya maeneo ya visiwa hivyo.

Anasema Serikali tayari imeanzisha shule maalumu Kusini Unguja na Kusini Pemba, huku ikipanga kupanua huduma hizo katika mikoa mingine, ikiwamo Kaskazini Unguja.

"Tunafahamu wazazi wengi wanaichagua Shule ya Kisiwandui kutokana na uzoefu wake katika elimu jumuisho. Mpango wetu ni kuhakikisha huduma kama hizi zinapatikana angalau katika kila mkoa," anasema.

Katibu wa Jumuiya ya Watu Wasioona Wilaya ya Kaskazini B, Awena Hassan Seif, ambaye pia ni mwalimu katika Shule ya Mjumuisho ya Kisiwandui, anasema wapo watoto wengi wanaoshindwa kuhudhuria masomo kwa sababu ya umbali na gharama za usafiri.

"Tuna mwanafunzi kutoka Kaskazini B anayehudhuria masomo kwa kusuasua. Mara nyingi hukaa nyumbani kwa sababu ya ukosefu wa nauli. Ni mtoto mwenye uwezo mkubwa darasani, lakini mazingira yanamrudisha nyuma," anasema.

Awena anashauri Serikali kuhakikisha angalau kila wilaya au mkoa unakuwa na darasa au shule yenye huduma za elimu jumuishi, ikiwemo walimu waliobobea na vifaa kama vitabu vya nukta nundu kwa wanafunzi wenye ulemavu wa kuona.

Anasema kuwajumuisha wanafunzi wenye mahitaji maalumu katika madarasa ya kawaida bila maandalizi ya kutosha ni kuwanyima fursa sawa ya kujifunza.

Kwa upande wa viongozi wa dini, Imamu wa Shehia ya Kitope, Sheikh Wadi Ali Mjengo anasema jamii ina wajibu wa kushirikiana kuhakikisha watu wenye ulemavu wanapata elimu bila vikwazo.

Naye Mchungaji wa Kanisa la TAG Kitope, Emmanuel Balingila anasema elimu ni haki ya kila mtoto bila kujali hali yake.

"Hakuna anayetamani kupata ulemavu. Leo unaweza kuwa mzima, kesho ukapata ajali. Ndiyo maana haki ya elimu inapaswa kutolewa kwa usawa kwa kila mtu," anasema.

Wito huo unaungwa mkono na Mradi wa Uwezeshaji wa Jamii katika Haki na Utawala Bora (CEJG Phase V), unaotekelezwa na Idara ya Maendeleo ya Kanisa Katoliki Jimbo la Zanzibar.

Mwanasheria wa mradi huo, Peter Marwa, anasema elimu ni haki ya msingi inayomwezesha mtoto kutimiza ndoto zake na kujenga maisha bora.

"Serikali inapaswa kusogeza huduma hizi karibu na wananchi ili kuhakikisha hakuna mtoto anayekosa elimu kwa sababu ya ulemavu au umbali anaotoka," anasema.

Anasema kupitia mradi huo, kanisa limejikita katika kuongeza uelewa wa jamii kuhusu haki za watu wenye ulemavu na kushirikiana na viongozi wa dini, Serikali na jamii kuondoa vikwazo vinavyowakabili.

Hata hivyo, kupitia bajeti ya Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali ya mwaka 2026/27 yenye thamani ya Sh1.1 trilioni, hakuna kipengele kinachoonyesha ujenzi wa shule mpya za elimu mjumuisho. Badala yake, Serikali imeweka mkazo katika kuongeza idadi ya walimu waliopata mafunzo ya elimu mjumuisho na stadi za maisha kutoka 2,096 hadi 2,500.

Aidha, wizara imepanga kuongeza uandikishaji wa wanafunzi wenye mahitaji maalumu kutoka 10,341 mwaka 2025/26 hadi 10,500 mwaka 2026/27, pamoja na kuwapatia vifaa vya kujifunzia wanafunzi 50 wenye mahitaji maalumu.

Pamoja na hatua hizo, wazazi na wadau wa elimu wanaamini changamoto ya umbali na gharama za usafiri zitaendelea kuwa kikwazo kwa watoto wengi wenye ulemavu hadi pale huduma za elimu mjumuisho zitakaposogezwa karibu na makazi yao.

Kwa sasa, kwa baadhi ya familia za Kaskazini Unguja, haki ya mtoto kupata elimu bado inaanza na uwezo wa mzazi kumudu nauli ya kila siku.

Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Khamis Abdulla Said anasema Serikali inaendelea kuimarisha uwezo wa walimu ili shule nyingi zaidi ziweze kuhudumia wanafunzi wenye mahitaji maalumu.

"Tumeajiri walimu 90 wa elimu mjumuisho na lengo letu ni kuwapatia walimu wote wa Zanzibar mafunzo ya elimu mjumuisho, ili wanafunzi wenye mahitaji maalumu wapate huduma katika shule mbalimbali bila kutegemea vituo vichache vya wataalamu," anasema.