Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Wizara ya Habari yabainisha vipaumbele tisa, ikiomba Sh243.3 bilioni

Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Dk Riziki Pembe Juma akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya wizara hiyo Barazani Chukwani Unguja, Zanzibar

Muktasari:

  • Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Dk Riziki Pembe Juma ameliomba Baraza la Wawakilishi kuidhinisha Sh243.3 bilioni kwa ajili ya kutekeleza vipaumbele hivyo.

Unguja. Wizara ya Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo imeainisha vipaumbele tisa kwa mwaka wa fedha 2026/27 ikiwa ni pamoja na kuimarisha upatikanaji na usambazaji wa habari.

Akisoma makadirio ya mapato na matumizi ya wizara hiyo leo Juni 4, 2026, Waziri mwenye dhamana na wizara hiyo, Dk Riziki Pembe Juma ameliomba Baraza la Wawakilishi kuidhinisha Sh243.3 bilioni kwa ajili ya kutekeleza vipaumbele hivyo.

Dk Riziki amesema wizara inapanga kuimarisha upatikanaji na usambazaji wa habari, kuimarisha usimamizi na udhibiti wa vyombo vya habari, uchapaji na utangazaji na kutoa elimu kwa jamii juu ya kulinda mila, silka na utamaduni wa Mzanzibari.

“Kusimamia shughuli za sanaa na burudani, kuendeleza, kukuza na kueneza matumizi ya Kiswahili fasaha na sanifu, kusimamia na kuimarisha miundombinu ya michezo, kuratibu maendeleo ya michezo nchini,” amesema.

Kipaumbele kingine ni kusimamia matayarisho na uratibu wa mashindano ya AFCON 2027 na kutayarisha sera, sheria, kanuni na miongozo mbalimbali itakayowezesha kusimamia pamoja na kutoa huduma bora kwa jamii katika sekta za habari, sanaa, utamaduni na michezo.

Akisoma maoni ya Kamati ya Ustawi wa Jamii, Ibrahim Hussein Makungu amesema kamati imebaini changamoto ya ufinyu wa ofisi pamoja na kukosekana usafiri kwa Baraza la Kiswahili la Zanzibar (Bakiza).

“Ufinyu wa ofisi inayotumiwa na Bakiza inatoa taswira mbaya kwa watendaji na wageni wanaofika katika ofisi hiyo kupata taaluma, hii ni taasisi muhimu tunaona wageni wengi wanaotoka ndani na nje hufika kujifunza,” amesema Makungu.

Kamati imeishauri Serikali kupitia Wizara ya Fedha kuwatafutia usafiri wa uhakika kutokana na changamoto hiyo.

Akichangia bajeti hiyo, Mwakilishi wa Wawi, Bakar Hamad Bakar (CCM), amesema sekta ya habari ndio inasukuma juhudi na mipango ya serikali katika kufikia maendeleo lakini bado kuna changamoto mbalimbali zinazoikabili hivyo zifanyike jitihada kuhakikisha zinaondoka.

Amesema sekta hiyo ndio inatumika kuhamasisha umoja, kuleta mshikamano na hatimaye kuleta maendeleo nchini.

“Kwa hiyo ipo haja kuendelea kuijengea uwezo na kujadili masilahi ya wanahabari katika vyombo vya habari vya Serikali na binafsi lakini hazitekelezeki, ikilinganisha na kazi kubwa wanayoifanya katika Taifa hili,” amesema.

Mwakilishi wa Paje, Jaku Hashim Ayub (CCM), amesema kumekuwapo na maudhui mabaya ya vyombo vya habari vingine vikijenga na kuharibu utamaduni wa Zanzibar.

Pia, amesema ipo haja kuzingatia matumizi fasaha ya lugha ya Kiswahili kwani kumekuwapo na makosa mengi ya kisarufi hivyo inaharibu Kiswahili.

Katika mchango wake, Jaku amehoji Sheria ya Habari imefikiwa wapi kwani umepita muda mrefu.

Naye, Mwakilishi wa Tumbatu, Mahmoud Omar Hamad amesema ipo haja kuhakikisha Bakita inafanana na hadhi ya Kiswahili tofauti na ilivyo sasa.

“Tulitegemea kutokana na umuhimu wa lugha ya Kiswahili kuwe na tafiti nyingi zilizofanywa kuhusu lugha hiyo,” amesema.

Amesema mahitaji ya Kiswahili ni makubwa zaidi duniani kuliko ndani ya nchi kwa hiyo ipo haja kufanya utafiti na kuwa na machapisho ili kukipanua, kukikuza na kukiendeleza kwa ajili ya maendeleo ya badaye.