Zanzibar inavyoanza kujitegemea uzalishaji wa nyama, mboga na viungo
Sehemu ya kuku wa mayai wanaofugwa katika shamba la Farm Poultry Mbuzini Mkoa wa Kaskazini Unguja. Pcha na Jesse Mikofu
Muktasari:
- Ni safari ya kuanza kujitegemea kuzalisha nyama, hususan kuku, mbogamboga na viungo baada ya kuweka mazingira na mkazo katika sekta hiyo ili kuacha kuagiza bidhaa hizo kutoka nje ya nchi.
Unguja. Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imeanza kutekeleza mkakati wa kuongeza tija katika sekta ya kilimo na mifugo, hatua inayolenga kupunguza utegemezi wa kuagiza mazao na bidhaa za mifugo kutoka nje ya nchi na kukidhi mahitaji ya soko la ndani, hususan sekta ya utalii.
Hatua hiyo inakuja wakati visiwa hivyo vikikabiliwa na uhitaji mkubwa wa nyama ya kuku, mayai, mboga, matunda na viungo vinavyotumiwa na hoteli za kitalii zaidi ya 600, ambapo takribani asilimia 70 ya mahitaji hayo yamekuwa yakiagizwa kutoka nje.
Akizungumza leo Jumatano, Julai 22, 2026, baada ya ziara ya mawaziri wa kisekta kukagua miradi ya kilimo na mifugo, Waziri wa Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo, Suleiman Masoud Makame, amesema Serikali imeanza kutekeleza mpango maalumu wa kutatua changamoto zinazowakabili wakulima na wafugaji ili kuongeza uzalishaji wa ndani.
Amesema ziara hiyo imelenga kutathmini hali halisi ya uzalishaji na kuweka mikakati ya kuifanya Zanzibar ijitosheleze kwa bidhaa muhimu za kilimo na mifugo.
"Baada ya ziara yetu hii na mikakati ambayo tunategemea kuwa nayo, tunakwenda kupunguza kwa kiasi kikubwa sana, au kumaliza kabisa, suala la uagizaji, hasa mayai, kuku na mboga. Ripoti ya ziara hii tutaiwasilisha katika Baraza la Mapinduzi," amesema Makame.
Katika ziara hiyo, mawaziri kutoka wizara mbalimbali, zikiwemo Fedha, Ardhi, Ofisi ya Rais Ikulu na Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, walitembelea shamba la kisasa la uzalishaji wa kuku na mayai la kampuni ya Zanbreed linalojengwa Kitope, Mkoa wa Kaskazini Unguja.
Meneja Mkuu wa Zanbreed, Emin Saat, amesema uzalishaji unatarajiwa kuanza Agosti mwaka huu, na kampuni hiyo itakuwa na uwezo wa kuzalisha kuku milioni moja kwa mwezi katika hatua ya awali.
Sehemu ya shamba la nyanya zinazolimwa katika eneo la Bambi Mkoa wa Kusini Unguja. Eneo hilo lenye ukubwa wa ekari 18 linalimwa mboga na viungo kutoka kwa wananchi wa mkoa huo. Picha na Jesse Mikofu
Amesema nusu ya uzalishaji huo utauzwa ukiwa mbichi (fresh), huku asilimia 50 nyingine ikiwa ni kuku waliogandishwa (frozen), akibainisha kuwa kampuni hiyo inalenga kuwahamasisha wananchi kutumia zaidi kuku wabichi wanaozalishwa nchini.
Mbali na uzalishaji wa kuku, amesema mradi huo utakuwa na uwezo wa kuzalisha tani 12,000 za chakula cha mifugo kwa mwaka na kupitia nyumba nane za kufugia, kila moja ikiwa na uwezo wa kuzalisha vifaranga 80,000 kwa mzunguko, sawa na zaidi ya vifaranga 640,000 kwa wakati mmoja.
Hata hivyo, Saat amesema changamoto kubwa inayoweza kuathiri uzalishaji ni upatikanaji wa umeme wa uhakika, akiiomba Serikali kuweka suluhisho la kudumu.
Akizungumzia hilo, Waziri Makame amesema Serikali itafanyia kazi changamoto zote zinazowakabili wawekezaji ili kuweka mazingira bora ya uzalishaji na kuongeza ajira kwa vijana.
"Wawekezaji hawa wanakwenda kupunguza kwa kiasi kikubwa uagizaji wa kuku kutoka nje. Pia watazalisha kuku wabichi kwa wingi, jambo litakalowanufaisha wananchi na sekta ya utalii," amesema.
Kwa upande wake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Sera, Uratibu na Baraza la Wawakilishi, Hamza Hassan Juma, amesema Zanzibar imeanza kushuhudia mabadiliko makubwa katika sekta ya mifugo baada ya wafugaji kuhamasishwa kuwekeza katika ufugaji wa kisasa wenye tija.
"Kwa muda mrefu tulikuwa na wafugaji wadogo wenye uzalishaji mdogo. Sasa tunaona uwekezaji mkubwa unaoweza kuongeza uzalishaji na kupunguza utegemezi wa bidhaa kutoka nje," amesema.
Amesema hatua hiyo ni muhimu kwa kuwa uchumi wa Zanzibar unategemea kwa kiasi kikubwa sekta ya utalii, ambayo imekuwa ikihitaji kiwango kikubwa cha bidhaa za chakula kutoka nje ya nchi.
Naye Ofisa Mkuu wa Ugani, Salim Rehani, amesema jitihada za Serikali za kuwahamasisha wakulima zimepunguza uingizaji wa mboga na matunda kutoka nje kwa takribani asilimia 80.
Amesema kwa sasa mazao yanayoendelea kuagizwa kwa kiwango kikubwa ni vitunguu maji na viazi mbatata, huku Serikali ikiendelea na mikakati ya kuongeza uzalishaji wake ili kupunguza kabisa uagizaji.
"Tunatarajia kuona ongezeko kubwa la uzalishaji wa mboga na matunda, ikiwemo pilipili, tikiti, maboga na mazao mengine, jambo litakalopunguza kwa kiasi kikubwa uagizaji kutoka nje," amesema.
Kwa mujibu wa hotuba ya bajeti ya Wizara ya Kilimo ya mwaka 2026/27, uzalishaji wa mayai Zanzibar umeongezeka kutoka mayai 22,089,658 mwaka 2024 hadi mayai 29,861,934 mwaka 2025.
Katika kipindi hicho, idadi ya kuku waliochinjwa imeongezeka kutoka 1,085,856 mwaka 2024 hadi 1,472,903 mwaka 2025, hatua inayoonesha ukuaji wa sekta ya mifugo visiwani humo.