Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Zanzibar yaja na mkakati kuendeleza zao la chumvi

Kaimu Katibu Mtendaji wa Tume ya Mipango Zanzibar, Afua Mohamed (wapili kushoto) wakati akifungua semina ya kuwajengea uelewa waandishi wa habari kuhusu majukumu, kazi na nafasi ya Tume katika maendeleo ya Zanzibar. Picha na Zuleikha Fatawi

Muktasari:

  • Serikali inafanya hivyo kwa lengo la kuongeza viwanda vitakavyosaidia kutoa ajira na kukuza vipato vya wananchi.

Unguja. Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) imeandaa mkakati maalumu wa kuendeleza zao la chumvi kisiwani hapa ikiwa na lengo la kuongeza ajira kwa vijana.

Hayo yamebainishwa leo Alhamisi Juni 4, 2026 na Mkuu wa Divisheni, Uratibu wa Fedha za Tafiti, Idara ya Utafiti kutoka Tume ya Mipango Zanzibar, Hamisa Ali Mohamed katika semina ya kuwajengea uelewa waandishi wa habari kuhusu Tume hiyo.

Amesema idara hiyo imepitia ripoti mbalimbali za kutambua hali halisi ya zao hilo ikiwemo changamoto zinazoikumba sekta ili kuzitafutia ufumbuzi.

Hamisa amesema Serikali inafanya hivyo kwa lengo la kuongeza viwanda vitakavyosaidia kutoa ajira na kukuza vipato vya wananchi.

“Idara ya utafiti ipo katika mkakati wa kuendeleza zao la chumvi na ripoti mbalimbali za kuchambua hali halisi na changamoto ambayo sekta hiyo inakumbana nayo imepitiwa,” amesema.

Vilevile, Hamisa amesema idara hiyo kupitia programu maalumu imefanikiwa kukamilisha tafiti za kuliendeleza na kuliimarisha zao la karafuu.

Amesema kupitia idara ya utafiti kwa kushirikiana na taasisi zilizoguswa na zao hilo wameandaa programu ya maendeleo ya zao la karafuu itakayosimamiwa na Shirika la Biashara la Taifa Zanzibar (ZSTC).

Amesema sababu ya kufanya hivyo imetokana na kutambua kuwa karafuu ni miongoni mwa uchumi wa Zanzibar na utamaduni kisiwani humo, hivyo ni wajibu wao kulifanya zao hilo kurudi kama awali.

Pia, amesema idara hiyo imefanikiwa kukamilisha tathmini ya utekelezaji wa ajenda ya utafiti mwaka 2021/26 ambapo kwa sasa wapo katika mchakato wa kuandaa ajenda hiyo kwa miaka mitano ijayo.

Naye, mkuu wa kitengo cha uchambuzi wa kiuchumi, Idara ya Ukuzaji Uchumi kutoka Tume ya Mipango Zanzibar, Shemsha Abdallah Mbarouk amesema kazi kubwa ya kitengo hicho ni kusimamia na kufuatilia mwenendo wa uchumi wa Zanzibar, kuimarisha utulivu wa uchumi jumuishi na chanzo kikuu cha uchambuzi na ushauri wa sera za kiuchumi za Serikali.

Mbali na hayo, amesema wanafanya ufuatiliaji wa mabadiliko ya kiuchumi na hatari zake kwa kutoa ushauri na taarifa na ufuatiliaji wa bei za mafuta na vita vya dunia vinavyoendelea.

“Kupitia vita hivyo tunapata nafasi ya kutoa ushauri kuhusiana na namna ya kuandaa sera za uchumi zinaoweza kuilinda nchi ili isiathirike,” amesema.

Kwa upande wake, Kaimu Katibu Mtendaji wa Tume hiyo, Afua Mohamed amesema tume hiyo ilianzishwa kwa lengo la kuhakikisha kuwa Zanzibar inakuwa na mfumo madhubuti wa kupanga, kusimamia na kutekeleza na ufuatiliaji wa maendeleo kwa kuzingatia vipaumbele vya kitaifa vilivyozingatia mahitaji ya wananchi.