Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Zanzibar yatenga Sh99 bilioni kujenga shule 13 za ghorofa

Waziri wa Elimu na Mafunzo, Lela Mohamed Mussa (kulia), akimkabidhi nyaraka za ujenzi wa sekondari Jang' ombe mkandarasi Fakih Abdalla Pandu kutoka kampuni ya Faster inayojenga shule hiyo Mkoa wa Mjini Magharibi Zanzibar. Picha na Jesse Mikofu

Muktasari:

  • Shule hizo zitajengwa na makandarasi watano tofauti kwa kipindi cha takribani mwaka mmoja kuanzia Februari mwaka huu hadi Februari 2027, zina ukubwa tofauti wa kati ya vyumba vya madarasa 16 hadi 41. Jumla zitakuwa na vyumba vya madarasa 397.

Unguja. Safari ya kumaliza mfumo wa mikondo miwili kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari Zanzibar imeanza rasmi baada ya Serikali kuwakabidhi makandarasi maeneo ya ujenzi wa shule 13 za ghorofa Unguja na Pemba.

Shule hizo zitajengwa na makandarasi watano kwa kipindi cha mwaka mmoja kuanzia Februari 2026 hadi Februari 2027. Zitakuwa na kati ya vyumba 16 hadi 41 kila moja, jumla ikiwa vyumba 397, na zitajengwa kwa gharama ya Sh99.187 bilioni. Shule saba zinajengwa kupitia mradi wa kuboresha elimu ya msingi Zanzibar (Zique) unaofadhiliwa na Benki ya Dunia, huku nyingine zikigharamiwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ).

Kwa sasa, asilimia 81 ya wanafunzi wa sekondari katika shule 227 za Serikali wanaingia mkondo mmoja, wakati shule za msingi zikiwa zimefikia asilimia 70 kati ya shule 341 za Serikali. Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali, Lela Mohamed Mussa, amesema ujenzi huo utamaliza asilimia 20 iliyosalia kwa sekondari na asilimia 30 kwa msingi ili wanafunzi wote wasome asubuhi pekee.

Amesema Serikali imeipa kipaumbele sekta ya elimu kwa kuimarisha miundombinu, akisisitiza makandarasi kukamilisha miradi hiyo kwa wakati na viwango vinavyotakiwa. Pia amewataka kutoa ajira za muda kwa vijana wa maeneo husika kwa kazi zisizohitaji utaalamu maalumu.

Mshauri elekezi kutoka kampuni ya wahandisi, Valence Jeremia, amesema watahakikisha miradi inatekelezwa kwa kasi na ubora unaohitajika. Makandarasi wameahidi kujenga kwa viwango ili kulinda imani waliyopewa na Serikali.

Mafundi wakiendelea na maandalizi ya ujenzi wa sekondari ya Jang'ombe baada ya kukabidhiwa eneo na serikali kujenga jengo la ghorofa tatu Mkoa wa Mjini Magharibi Zanzibar. Picha na Jesse Mikofu

Mkandarasi wa kampuni ya Faster inayojenga Shule ya Ufundi Mikunguni, Fakih Abdallah Pandu, amesema wanalenga kukamilisha jengo hilo mapema ili liwe miongoni mwa miradi itakayozinduliwa katika maadhimisho ya miaka 63 ya Mapinduzi ya Zanzibar mwaka 2027.

Mkuu wa Shule ya Sekondari Jang’ombe, Abdalla Idd Hassan, amesema shule hiyo yenye wanafunzi 1,200 na walimu 54 itanufaika na maabara za kemia, fizikia, biolojia na kompyuta pamoja na vyumba 38 vya madarasa, hatua itakayokomesha mikondo miwili.

Kazi ya kukabidhi maeneo ya ujenzi ilianza Februari 16, 2026 na inatarajiwa kukamilika Februari 28, 2026.