Jenista Mhagama – Waziri wa Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu

Waziri wa Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu, Jenista Mhagama.

Muktasari:

Jenista Joakim Mhagama ni Waziri wa Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu katika Serikali ya Awamu ya Tano, akiwa kwenye baraza la mwanzo la Rais John Magufuli. Jenista ni mbunge wa jimbo la Peramiho lililoko Ruvuma tangu mwaka 2005 hadi sasa.

Historia na elimu

Jenista Joakim Mhagama ni Waziri wa Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu katika Serikali ya Awamu ya Tano, akiwa kwenye baraza la mwanzo la Rais John Magufuli. Jenista ni mbunge wa jimbo la Peramiho lililoko Ruvuma tangu mwaka 2005 hadi sasa.

Hivi sasa, Jenista ana miaka 48 na ifikapo mwezi Juni mwaka huu atatimiza miaka 49 kwa kuwa alizaliwa Juni 23, 1967 mkoani Ruvuma. Baba mzazi wa Jenista ni Joakim Ngonyani (marehemu) ambaye wakati wa uhai wake alikuwa mwalimu na baadaye mkuu wa Chuo cha Maendeleo ya Jamii. Mama yake ni Epifania Shawa (marehemu) mwenyeji wa kijiji cha Maposeni. Alikuwa mama wa nyumbani na anatoka kwenye ukoo wa Chifu Gama wa kabila la Wangoni.

Jenista alianza elimu ya msingi mwaka 1976 katika Shule ya Msingi ya Mfaranyaki iliyoko Peramiho. Alihitimu darasa la saba mwaka 1982. Mwaka 1983 alianza elimu ya sekondari katika Shule ya Wasichana ya Peramiho. Alihitimu kidato cha nne mwaka 1986. Mwaka uliofuata aliendelea na kidato cha tano katika Chuo cha Mafunzo ya Ualimu Korogwe na kuhitimu kidato cha sita mwaka 1989.

Baadaye aliendelea na masomo ya stashahada ya ualimu chuoni hapo na kuhitimu mwaka 1990. Lakini, mwaka huohuo, yaani 1989, alisoma na kuhitimu kozi ya ngazi ya cheti katika masuala ya utengenezaji wa mitaala na upangaji wa programu.

Rekodi zinaonyesha pia kuwa Jenista alienda nchini Italia na kusoma kwa miezi kadhaa masuala ya ujasiriamali hadi alipohitimu kwa ngazi ya cheti, kutoka kituo cha Shirika la Kazi Duniani (ILO) kilichoko mjini Turin.

Baadaye akasoma na kuhitimu stashahada ya kimataifa ya uongozi na usimamizi wa kisasa nchini Uingereza. Hivi sasa anaendelea na masomo ya shahada ya umahiri kwenye katika chuo hicho hicho, lakini akisoma bila ya kuhudhuria darasani (Long Distance Studies). Jenista ni mjane na ana watoto watatu.

 

Uzoefu

Mara baada ya kuhitimu stashahada ya elimu, Jenista aliajiriwa na Wizara ya Elimu akiwa mwalimu. Amefundisha shule mbalimbali kwa miaka sita mfululizo--, kuanzia mwaka 1991 hadi 1997-- lakini pia kwa miaka mitano mfululizo--1995 – 2000-- amekuwa katibu wa mfuko maalum uliokuwa chini ya ofisa elimu wa Wilaya ya Ruvuma (Ruvuma DEO-Trust Fund).

Kati ya mwaka 1997 na 2000 alifanya kazi Mamlaka ya Mafunzo ya Elimu ya Ufundi Tanzania (VETA).

Wakati Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2000 unakaribia, akiwa na miaka 33, Jenista ambaye ni mwanachama wa CCM wa muda mrefu, alichukua fomu za kuomba ubunge wa viti maalum upande wa ubunge. Alipambana ndani ya chama chake na kupitishwa na vikao vya juu vya CCM kuwa mbunge kutoka Mkoa wa Ruvuma. Uzoefu wa miaka mitano ya ubunge ulimpa Jenista kila sababu ya kuingia kwenye ubunge wa jimbo kuchuana na wanaume.

Ule uchaguzi wa “kimbunga cha CCM” ulipowadia mwaka 2005, Jenista aliyapanda majukwaa ya jimbo la Peramiho akiiwakilisha CCM. Mwisho wa siku aliwashinda wagombea kutoka Chadema, CUF na TLP kwa zaidi ya asilimia tisini ya kura zilizopigwa. Alipata kura 46,480 sawa na asilimia 93.2% na kuwaacha wagombea wa vyama hivyo vitatu wakigawana asilimia 6.8 ya kura zote.

CCM ilimpa Jenista heshima ya kuwa mmoja wa wenyeviti wa Bunge, nafasi ambayo ni nadra kwa wanawake kutokana na mfumo wa mitandao na nguvu kubwa za wanaume kisiasa katika maeneo mbalimbali ya nchi.

Katika uchaguzi wa mwaka 2010, Jenista alishinda kwa mara ya pili kura za maoni ndani ya CCM na kupitishwa kuwa mgombea. Alishindana na mgombea pekee kutoka CUF, Emmanuel Chilokota na safari hii ushindi wake ulipungua baada ya kupata kura 28,782, sawa na asilimia 89.43 akimuacha mgombea wa CUF ambaye alikuwa na kura 2,642, sawa na asilimia 8.21.

Baada ya ushindi wa ubunge wa mwaka 2010, CCM ikampa heshima tena Jenista, akapewa uenyekiti wa Bunge na kuwa mmoja kati ya wafanya maamuzi wakubwa na waendesha vikao maalum vya chombo hicho cha kutunga sheria. Januari 20, 2014, Rais wa awamu iliyopita, Jakaya Kikwete alimteua kuwa Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi akichukua nafasi ya Philipo Mulugo. Januari 2015 alihamishwa wizara na kuteuliwa kuwa waziri kamili kwenye Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera na Utaratibu wa Bunge). Jenista amedumu kwenye wizara hiyo hadi kumalizika kwa uongozi wa JK.

Katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015, Jenista alichukua fomu ndani ya chama chake na dalili zilianza kujionyesha mwanzo kwamba hakuwa na washindani thabiti. Siku ya upigaji kura za maoni, washindani wake ambao ni Lazaro Bunungu, mfanyakazi wa Tanroads mkoani Tanga na Clement Makaburi Mwinuka, mwananchi wa kawaida aishiye Peramiho, hawakutokea. Ilidaiwa kwamba wa kwanza alianguka siku moja kabla ya uchaguzi huo na wa pili fomu yake ilisainiwa na mtu mwingine. Jenista akapita bila kupingwa.

Kwenye Uchaguzi Mkuu, Jenista alishinda kwa kura 32,057 dhidi ya mgombea Chadema, Erasmo Mwingira, jambo lililompa nafasi ya kuwa mbunge kwa kipindi cha nne. Baada ya uchaguzi wa Oktoba 25 mwaka jana, Rais JPM alimteua kuwa Waziri wa Sera, Bunge, Vijana, Kazi, Ajira na Walemavu.

Ndani ya CCM, Jenista ameshikilia nyadhifa kadhaa kwa kipindi kirefu. Kwanza alikuwa katibu wa tawi tangu mwaka 1987 hadi 1990, pili amekuwa mjumbe wa Baraza la Wilaya la CCM tangu mwaka 1995 na amewahi kuwa katibu wa Umoja wa Wanawake (UWT) ngazi ya kata kati ya mwaka 1995 hadi 2000.

 

Nguvu

Kwanza, Jenista kwa zama za sasa ndiye mwanamama mzoefu kisiasa kuliko wote kwenye Baraza la Mawaziri la JPM. Kwenye baraza hilo hakuna mwanamama ambaye amekuwa mbunge kwa zaidi ya miaka 15 kama yeye na pia hakuna mwanamama ambaye amekuwa na uzoefu wa uongozi wa juu ndani ya Bunge kwa miaka tisa kama alivyo yeye, hivyo hiyo ni dalili kwamba bado anaweza kufika mbali kisiasa kwa kuwa siasa zina zama zake katika ukuaji.

Pili, Jenista anao uwezo mkubwa wa ujenzi wa hoja na kushawishi. Kwenye Bunge lililopita, nilikuwa namchukulia kama mmoja wa wabunge wenye uwezo mkubwa wa kujenga hoja na ushawishi kutoka upande wa CCM na hasa kwenye eneo la wanawake.

Hayo yamemfanya aendelee kuwa na nguvu kubwa kwa wananchi anaowaongoza jimboni hadi ndani ya Serikali. Huyu kwa sasa hajifunzi siasa, ana uwezo na fursa na kila sifa ya kufanya vizuri katika siasa na watu wayaone matokeo.

Tatu, Jenista ni mwanamama anayeyajua mazingira ya watu wa chini na hali hiyo itamsaidia sana ikiwa ataamua kuwa waziri bora anayeshughulikia masuala ya vijana. Amekuwa mwalimu kwa miaka kadhaa na amefanya kazi katika halmashauri kwa miaka kadhaa. Huyu ni mtu anayejua nini vijana wanataka. Anaweza kukosa ujuzi na uwezo au weledi wa masuala ya vijana, lakini akisaidiwa anaweza kabisa kujenga msingi mzuri.

 

Udhaifu

Udhaifu mkuu wa Jenista ni kushindwa kuacha alama thabiti kwenye wizara alizopitia kwa miaka miwili ambayo ametumikia Baraza la Mawaziri la JK. Kuanzia kule kwenye elimu aliporithi mikoba ya Philipo Mulugo hakufurukuta sana. Tungeweza kusema kwamba huenda mfumo wetu haumpi naibu waziri majukwaa ya kutosha kufanya uamuzi, lakini baadaye amekuwa Waziri wa Sera na Uratibu wa Bunge na hakufanya maajabu.

Wakosoaji wa Jenista wanasema huenda hatumii vizuri vipaji vyake, uwezo wake na ushawishi wake katika kufanya mambo yanayoweza kuonekana na hasa wana wasi wasi na uwezo wake wa kufanya na kusimamia uamuzi thabiti peke yake. Utetezi wa pekee anaoweza kuueleza ni kwa sababu hata kwenye uwaziri kamili hakukaa hata mwaka mmoja. Utetezi wa namna hiyo unaweza kupimwa ndani ya miaka miwili ijayo. Nini Jenista atafanya ili atofautishwe na yule aliyemsaidia Waziri Shukuru Kawambwa na baadaye akaongoza mikoba iliyoachwa na William Lukuvi.

 

Matarajio

Wakati Jenista anatarajia kutulia na kuondoa vikwazo vilivyomsababisha asing’are kipindi kifupi alichofanya kazi chini ya baraza la JK, atakuwa anajua kuwa sekta aliyokabidhiwa hivi sasa ina kelele za moja kwa moja kwa sababu imeunganishwa na masuala ya vijana, ajira, kazi na walemavu. Jenista anajua kuwa hatalala usingizi kwa miaka kadhaa kutoka sasa.

Watu wenye ulemavu, mathalani, wanatarajia waziri huyu aanzishe mpango na mkakati utakaoisaidia serikali iwatambue mahali walipo, wanafanya nini na ichukue hatua watakazoona kweli zinaweza kuwakwamua. Vijana walio wengi wanasubiri mipango ya kazi na ajira kutoka kwa Jenista. Hakuna cha kuongeza kwa sababu hizo ndiyo ndoto zao za kila siku.

 

Changamoto

Changamoto ya jumla itakayomkabili Jenista ni namna ya kuratibu na kuunganisha masuala sita mtambuka yanayohusu wadau muhimu kwa wakati mmoja. Hii ni wizara ambayo inahusika na masuala ya Bunge, Serikali, Vijana, Walemavu na Sera. Inafanya kazi kama kiungo cha Bunge na Serikali, vijana na Serikali, walemavu na Serikali, mipango ya sera, ajira na kazi. Ikiwa Jenista hatajipanga kwenye eneo hili, mboga yote inaweza kutiwa mafuta ya taa.

Changamoto ya kwanza iko kwenye eneo la sera. Nchi yetu imekuwa inajikongoja kimaendeleo kwa sababu sera zetu hazieleweki, hazishikiki, hazitulii na hazidumu. Kila siku Tanzania inajiendesha kwa sera mpya karibu kwenye kila sekta, zile zinazokaa muda mrefu (thabiti) hazitekelezwi kwa usimamizi wa kutosha. Matokeo yake tumekuwa taifa linalokwenda mbele hatua kumi na kurudi nyuma hatua 30.

Sera ndiyo msingi mkuu wa kuzaa sheria nzuri na taratibu nzuri za kusimamia masuala muhimu ya nchi. Taifa letu limekuwa linajiendesha kwa bahati nasibu na mara nyingi kwa kuacha misingi ya sera zake na kufuata misingi ya muda mfupi ya wanasiasa walioko madarakani, mwisho wa siku tumekuwa tukilalamika kwamba taifa linaangamia na halina mipango ya kudumu. Jenista amekabidhiwa jukumu kubwa la kuionyesha Serikali kila mara inakosea wapi na jukumu la kuileta kwenye mstari, kuifanya ishirikiane na Bunge kusimamia sera zetu, sera hizi zifahamike kwa kila mmoja wetu na zitekelezwe kwa usimamizi thabiti.

Kwa upande wa Bunge, huu ni mhimili muhimu wa dola ambao una nguvu ya kuifuatilia serikali na kuihoji, na kuirekebisha na kuichukulia hatua pale ambapo haitendi kwa mujibu wa Katiba na taratibu za nchi au Serikali ikijaribu kutenda masuala kinyume na matakwa na maslahi mapana ya taifa. Kwa bahati mbaya serikali nyingi za Afrika zimekuwa zikiutumia vibaya mhimili wa Bunge na kwa maslahi si ya taifa, bali vyama vilivyoko madarakani kwa ajili ya kuendelea kuongoza. Bunge la Tanzania limekuwa likiyumba sana mara nyingi na myumbishaji mkuu amekuwa ni Serikali na kiungo kikuu cha uyumbishaji huo ni wizara hii.

Wengi wanategemea kuwa Jenista anayatambua madhambi na rafu hizo za Serikali dhidi ya mhimili huu na kwamba atachukua hatua za kuishauri Serikali mara kwa mara itumie ushauri wa Bunge na wabunge kwa kiasi cha kutosha na pia iheshimu maazimio na maamuzi ya bunge bila kulihujumu. Changamoto ya uhuru wa Bunge imekuwa suala la muda mrefu na mara hii hatutegemei tena kuona Jenista naye anatumika moja kwa moja kulidogoesha Bunge na kuifanya Serikali ijiendeshe kwa mwendo wa kuweka pamba masikioni.

Eneo la kazi na ajira nalo ni pana, hili mara nyingi linaunganishwa na vijana kwani wao ndiyo wako kwenye umri wa kutafuta kazi na ajira kwa kiasi cha kutosha. Kama taifa lazima tukubali kuwa nchi yetu haina ajira za kutosha na haina mikakati ya muda mrefu ya kuanzisha ajira mpya kwa watu wetu na hasa vijana. Kwa mwaka mmoja Tanzania inazalisha makumi elfu ya vijana kwenye soko la ajira lakini haina uwezo wa kuajiri au kuwapa nyezo za kujiajiri hata asilimia 20 ya vijana hao. Asilimia kubwa ya vijana wa Tanzania hawajaajiriwa kwenye sekta rasmi wala kujiajiri kwenye sekta rasmi wala hawana mitaji ya kuwafanya wajiingize kwenye shughuli za ujasiriamali. Changamoto hii imezaa tatizo kubwa na kulifanya taifa lipoteze nguvu kazi yake kila mwaka. Jenista na wizara yake wanayo kazi ya kuzibana sana wizara zingine na kushirikiana nazo kimipango kwani zenyewe hasa ndizo zenye ajira. Tukiendelea kukosa mipango ya muda mrefu, utatuzi wa masuala ya kazi na ajira utaendelea kuwa wa kudumu.

Pana suala la mwisho linalowahusu watu wenye ulemavu. Hawa wamesahaulika na lazima tukubaliane hivyo, wamesahaulika na kila mmoja wetu na kwenye maeneo yote. Ndiyo maana unakuta hata majengo mapya ya serikali yanayojengwa yakiwa hayana sejemu maalum ambazo walemavu watatumia kupanda na kushuka, kila sehemu kuna ngazi na hakuna njia zao.

Mahitaji ya watu wenye ulemavu ni makubwa, wengi wao wametelekezwa na jamii na ndugu zao na serikali nayo imewakimbia wamebaki kuanzisha familia na makazi mitaani wakiomba omba. Nchi yetu inahitaji kuwa na mkakati wa kudumu wa kupunguza visababishi vya ulemavu lakini pia ikihakikisha wale ambao tayari wana ulemavu wanapangiwa taratibu maalum ikiwemo mafunzo ya kijitegemeza kisha wanapewa mitaji na kusimamiwa kwenye shughuli za ujasiriamali. Huwenda kama taifa tutakuwa kitu kimoja ikiwa tutakuwa na sera za kuwatoa watu wenye ulemavu mahali walipo kwenda mbele zaidi. Jenista Mhagama ana changamoto ya kufanya haya yawe dhahiri.

 

Hitimisho

Uzoefu wa Jenista na namna alivyo ni tunu tosha za kumfanya awike katika utatuzi wa changamoto za uhusiano kati ya bunge na serikali pamoja na uratibu wake, masuala ya vijana na ajira, walemavu na kusahauliwa kwao n.k. Rekodi ya Jenista huko nyuma ilikuwa ni uhodari mkubwa sana ndani ya bunge lakini alipopewa uwaziri hakusikika sana. Wafuatiliaji wengi wa mambo wanasubiri kuona namna gani mwanamama huyu atawatumia vyema vijana aliopewa kama manaibu wake, Daktari Possi (PhD) na Antony Mavunde (Mwanasheria) ili kwa pamoja wamtengenezee kombinesheni ambayo ikiingia kazini ikatenda, inaweza kufunika udhaifu na mapungufu ya waziri wao na hivyo yeye Jenista azidi kujiweka katika anga muhimu za utendaji ndani ya serikali ya sasa. Namtakia kila la heri.

 

*Uchambuzi huu unatokana na utafiti na maoni binafsi ya mwandishi).

 

Kuhusu mchambuzi

Julius Mtatiro ni Mchambuzi wa Masuala ya Kisiasa na Kijamii, ni mmoja kati ya vijana wenye uzoefu mkubwa na siasa za Tanzania. Ana Cheti cha Juu cha Sarufi (“Cert of Ling”), Shahada ya Sanaa “B.A” katika Elimu (Lugha, Siasa na Utawala), Shahada ya Umahiri ya Usimamizi wa Umma (MPA) na Shahada ya sheria (L LB) – Simu: +255787536759, Tovuti: www.juliusmtatiro.com, Email; [email protected]).