Ushirika dhidi ya ukeketaji


Ushirika dhidi ya ukeketaji

Mwaka 2018 Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, iliandaa mjadala wa kitaifa uliokuwa ukilenga kukabiliana na ukeketaji, ndoa na mimba za utotoni.

Mwaka 2018 Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, iliandaa mjadala wa kitaifa uliokuwa ukilenga kukabiliana na ukeketaji, ndoa na mimba za utotoni.

Mikoa mitano ambayo ilitembelewa na wanaharakati watano na wahamasishaji wa utokomezaji wa vitendo vya ukeketaji, yalikuwa miongoni mwa maeneo lengwa yaliyoorodheshwa katika mjadala huo.

Katika kutambua umuhimu wa ushirika na mshikamano katika kushughulikia kero hizi tatu, wizara iliwaalika wadau mbalimbali ikijumuisha mashirika yasiyokuwa ya kiserikali (NGOs) na asasi za kiraia kuwa sehemu ya mazungumzo hayo muhimu.

Kila mkoa uliweka vipaumbele vyake muhimu na muundo wake wa kiutekelezaji katika kukabiliana na aina tatu za ukatili wa kijinsia, kama ilivyo kwenye mpango kazi wa taifa wa utokomezaji ukatili dhidi ya wanawake na watoto wa mwaka 2018-2022 (NPA-VAWC).

Kwa kutumia mkakati huu wa kina, ulioridhiwa na makundi mbalimbali kimataifa wenye lengo la kupambana na aina zote za ukatili wa kijinsia nchini, wadau walifafanua uzoefu wa aina mbalimbali wa vitendo vya ukeketaji kulingana na mkoa husika au kabila. Hivyo, kila moja ya mkakati ulioridhiwa kutumika ulizingatia mambo haya.

Kwa mfano, katika mkoa wa Singida, Doris Mollel mwanaharakati wetu, alikutana na shirika linaloitwa Empower Society Transform Lives (ESTL) ambalo linapatikana katika mkoa huo. ESTL ina programu kadhaa zenye ubunifu, kama vile program iliyopewa jina la Kick female genital mutilation out of Singida region (Tokomeza ukeketaji katika wa Singida. Kulingana na kuwepo idadi kubwa ya watoto waliokeketwa wa chini ya mwaka mmoja, ESTL inalenga wanawake, wasichana, viongozi wa jadi na wakunga kuwa mabalozi wa utokomezaji wa mila hii yenye athari kubwa kwa jamii – kama vile suala la wadudu aina ya lawalawa linavyoaminika, na badala yake kutoa taarifa sahihi zisizopotosha. Vile vile shirika hilo linawahamasisha wavulana na wanaume kuwa sehemu ya umalizaji tatizo, na hutoa fursa mbadala za kujipatia kipato kwa mangariba.

Diana Lukumay, alitembelea Health Integrated Multi-Sectoral Services (HIMS) ambayo inaendesha program inayofadhiliwa na UNFPA, inayofanya kazi katika mikoa ya Arusha na Manyara. HIMS inalenga jamii za wafugaji katika kujenga uelewa juu ya athari za kiafya za ukeketaji kwa jamii. Katika kutambua umuhimu unaowekwa juu ya ustawi wa mtoto katika jamii za wafugaji, HIMS inasisitiza juu ya madhara ya ukeketaji kwa mama wakati wa kujifungua, na madhara kwa mtoto pia. Pia huelezea juu ya hatari za kuambukizwa au kusambaza magonjwa kama vile Ukimwi, fistula na maambukizi mengine kupitia ukeketaji.

Katika matoleo yaliyopita, baadhi ya manusura wa ukeketaji ambao Diana alizungumza nao walikaribishwa katika makazi yaliyokuwa chini ya HIMS. Wasichana waliendelea na masomo yao wakiwa kwenye makazi hayo.

Namaiyani, ngariba wa zamani, alikuwa mmoja wa mangariba 160, ambao walishawishiwa na HIMS na wakakubali kuachana na ukeketaji, mwaka 2018. Walipewa mafunzo ya ustadi tofauti, kama ufundi wa mikono na biashara ndogo. Kila mmoja alipewa kondoo dume mmoja na jike mmoja kama njia ya kusaidia kuendesha maisha yao. Baada ya muda, sasa ni mabalozi na wahamasishaji wa athari za ukeketaji katika jamii.

Mashirika kama OIKOS East Africa hufanya kazi na wadau wengine na jamii za wafugaji kuboresha maisha na kupunguza umaskini, kwa kukuza ujumuishaji wa kijamii na kiuchumi wa wanawake na wasichana kwa kuwekeza katika maarifa na ujuzi wao.

Diana pia alitembelea moja ya vituo vya OIKOS vinavyofadhiliwa na Jumuiya ya Ulaya (EU), jijini Arusha na kukutana na wanawake ambao walikuwa wakifanya mafunzo ya usindikaji wa ngozi, uelewa wa wanunuzi na soko na kuendesha benki ndogo za jamii. Pia walielimishwa juu ya haki zao za kijamii haswa juu ya haki za ardhi, haki za urithi na haki za kijinsia. Kama sehemu ya mpango huo, vikundi zaidi ya 30 vya wanawake wa jadi (TWG) viliwezeshwa na kuhimizwa kutambua jukumu la wanawake na haki yao katika jamii. Vikundi vya TWG vimesaidia sana katika kujenga uwezo na kusaidia wanawake wengine katika mazingira ya kitamaduni.

Baadhi ya wanawake waliokuwa katika kituo hicho walitoa ushuhuda wao wa jinsi uhuru wa kiuchumi ulivyowapa nguvu ya kuhakikisha watoto wao wanakwenda shule na binti zao hawakeketwi. Kupitia benki ndogo za jamii (VICOBA na SACCOS), wanawake walikutana na kujadili juu ya changamoto au masuala yanayowakabili. Walisaidiana wenyewe kwa wenyewe na waliweza pia kutoa mikopo midogo kwa wanachama kukabiliana na changamoto za kiuchumi, pamoja na kutoa elimu kwa watoto wao.

Mmoja wa wanufaika alimwambia Diana wakati wa ziara hiyo:

“Kabla ya kujiunga na kituo hiki, nilimtegemea mume wangu kwa kila kitu. Wakati mwingine hakuweza kutupatia mahitaji yetu yote. Lakini baada ya kujiunga, sasa naweza kupata pesa kutoka kwenye bidhaa za ngozi tunazouza, nilifanikiwa kupata mkopo kutoka kwenye VICOBA na kuanza bustani yangu ndogo ya mboga mboga na sasa sihitaji kumtegemea mume wangu kwa kila kitu.”

Katika toleo linalofuata, tutaona jinsi Association of Termination of Female Genital Mutilation (ATGM) na wadau wengine walivyoanzisha utaratibu mbadala wa kumuandaa binti kuelekea utu uzima katika mkoa wa Mara, kama njia ya kutokomeza ukeketaji.