Sophia Mbimbi: Mwanamke anayeendesha mitambo mikubwa katika mgodi wa dhahabu Geita (GGML)


Sophia Mbimbi: Mwanamke anayeendesha mitambo mikubwa katika mgodi wa dhahabu Geita (GGML)

Sophia Mbimbi ambaye anafanya kazi kwenye machimbo ya Mgodi wa Dhahabu Geita (GGML) ni mmoja wa wanawake waliojitoa kimasomaso na kuingia katika shughuli za uchimbaji wa madini kwenye machimbo ya mgodi wa madini na kujenga historia katika nchi ya Tanzania.

Sophia Mbimbi ambaye anafanya kazi kwenye machimbo ya Mgodi wa Dhahabu Geita (GGML) ni mmoja wa wanawake waliojitoa kimasomaso na kuingia katika shughuli za uchimbaji wa madini kwenye machimbo ya mgodi wa madini na kujenga historia katika nchi ya Tanzania.

Sophia ni mwanamke wa shoka ambaye huwa hakati tamaa kirahisi. Ingawa amekabiliwa na changamoto nyingi na vikwazo maishani mwake, lakini amekuwa akisimama kila wakati na kusonga mbele akikabiliana na changamoto hizo.

Sophia ambaye hivi karibuni ameteuliwa na GGML kuwa msimamizi wa shughuli za uchimbaji wa chini kwa chini (underground) kwenye migodi hiyo, anajisikia faraja kupata nafasi hiyo kwa sababu ni nafasi ambayo alipambana sana kuipata.

Kazi yake ya sasa ni kusimamia shughuli za usafirishaji wa shehena na vifaa mbalimbali chini ya ardhi ya mgodi wa dhahabu wa GGML. Pia husaidia usimamizi wa utekelezaji wa mpango wa kila siku kwa ufanisi, huku akihakikisha kuwa utendaji kazi wa mitambo unakuwa bora.

Ukimwangalia kwa umbo lake, umri wake bado ni binti mdogo sana lakini ameweza kufanya mambo mazuri na makubwa ya kihistoria ambapo mabinti wadogo kama yeye wanaweza kufuata nyayo zake.

Akizungumza na gazeti hili hivi karibuni, Sophia anasema anajivunia kuwa kwenye sekta hiyo ya uchimbaji wa madini kwani ilikuwa ni ndoto yake ya siku nyingi, hivyo anajivunia kuwa mwanamke shupavu na mpambanaji.

Anasema kwa kupitia kazi hiyo ameweza kuendesha maisha yake vizuri na kuisaidia jamii yake inayomzunguka kutokana na na kipato anachokipata katika kazi zake za migodini. “Mwanzoni nilikuwa na ndoto ya kufanya kazi katika moja ya migodi mikubwa hapa Tanzania, ndio ilikuwa ndoto yangu kubwa, lakini wakati huo nilikuwa sifikirii kufanya kazi katika migodi mingine,” alisema Sophia.

“Nilianza kazi kwenye mgodi mmoja hapa nchini ambako niliajiriwa kama Ofisa rasilimali watu mwaka 2003. Kufikia wakati huo, nilihisi kuwa kuna mengi ambayo naweza kufanya hususani katika kubadili muelekeo kutoka Ofisa rasilimali watu hadi kusimamia shughuli za uchimbaji wa chini ya ardhi, “anafafanua Sophia.

Anasema, kwa miaka yake sita (6) ya kufanya kazi katika machimbo ya madini ya mgodi huo, alikuwa akifanya kazi na wanaume peke yake jambo ambalo anasema halikumtia hofu japo alipitia katika changamoto mbalimbali kwa sababu yeye alikuwa mwanamke pekee. Kutokana na kazi hiyo, anasema amekuwa mwanamke shupavu kwa kufanya kazi katika mgodi wa madini na kuingia chini ya ardhi na alikuwa akifanya kazi mchana na usiku tena kwa kujiamini.

“Najivunia kuwa mwanamke wa kwanza kuingia ardhini katika mgodi wa madini, mwanamke ambaye anaendesha mashine kubwa katika migodi ya madini ambapo baadaye nilihamia katika mgodi wa madini ya dhahabu wa Geita Gold Mine Limited (GGML) na bado naendesha mitambo mikubwa hadi wanaume wananiogopa, licha ya kwamba kazi hiyo ni ngumu,”Anasema, ilikuwa sio sana kufanya kazi hiyo, lakini kwa sababu alikuwa akijitambua nini anafanya akiwa kama mwanamke alijitoa kimasomaso kwani ndoto yake ilikuwa ni kufanya kazi hiyo licha kwamba ilikuwa ni ngumu.

“Hii kazi sikufanya kwa kujaribu, mimi kama mwa-namke niliyekuwa najitambua nilifanya kazi tena kwa kujiamini, nilikuwa sijali kwamba mimi ni mwanamke peke yangu eti niwe na hofu hapana, nilifanya kazi kweli kweli na sio kufanya kwa kujaribu,” anasema Sophia.

Sophia anasema kuwa, amekuwa akikatishwa tamaa na watu hususani wanaume ambao waliamini amepoteza maono yake baada ya kutoka Ofisa rasilimali watu kwenda kufanya kazi chini ya ardhi kwa sababu ni moja ya ajira hatari.

“Niliendelea kusimamia ninachokiamini nikisisitiza kwamba nataka kuanza kufanya shughuli za kuchimba madini chini ya ardhi. Mwanzoni ilikuwa ngumu sana lakini baadaye, meneja wangu alikubali kwamba naweza kufanya kazi hiyo, “anafafanua Sophia.

Alikaa miaka kadhaa akifanya kazi kama muendeshaji wa chumba cha winch katika kampuni hiyo ambapo pia alifanya kazi za kibenki na shughuli nyingine zilizo-anzishwa. Baada ya mkataba wake kumalizika, alikwenda Mamlaka ya Mafunzo ya Ufundi na Stadi (VETA) Shinyanga kufanya kozi fupi ya uendeshaji wa mitambo mikubwa.

Mwaka wa 2019, alitaka kufanya mafunzo ya vitendo katika mgodi wa dhahabu wa Geita (Geita Gold Mining) lakini haikuwa rahisi kwa sababu, Veta hakukuwa na barua rasmi anayotakiwa kupewa mhitimu wa mafunzo ya kozi fupi. Alimshawishi mkuu wake wa chuo kumuandikia barua na kumsainia ili aweze kupata fursa ya mafunzo ya vitendo GGML.

Anakiri kwamba, haikuwa rahisi kwa sababu GGML haikuruhusu wanafunzi kufanya mafunzo ya vitendo katika maeneo ya kazi. “Idara zote mbili za mafunzo na madini hazikutaka nifanye mafunzo ya vitendo kwenye mashimo.

Kwa kuwa GGML inachukulia usalama kama kipaumbele chake cha kwanza katika utendaji wa kazi, walihofia kutokea kwa ajali kwa sababu nililazimika kuanza kutumia mitambo mikubwa,” anaelezea.

Mwishowe aliruhusiwa kufanya mafunzo yake ya vitendo kwenye shimo la GGML Nyankanga kwa miezi minne ambapo alikuwa akifanya kazi pamoja na wanaume tofauti.

Haikuwa rahisi kwa sababu alikuwa akikatishwa tamaa wakati wote, lakini mwisho wa siku kila mtu alivutiwa na kushangazwa na uharaka wake na ari ya kujifunza aliyokuwa nayo.

Baada ya mafunzo yake ya vitendo, alianza kuishi Geita akitafuta ajira ya kudumu huko GGML. Haikuwa rahisi kwa sababu alituma maombi na kuorodheshwa kwenye orodha fupi ya watu waliochaguliwa kufanya usaili wa kazi mara mbili lakini hakufanikiwa hata mara moja.

Baada ya miezi minne aliona tangazo juu ya kazi ya usimamizi wa shughuli za migodi chini ya ardhi (Dispatch underground) na yeye akaomba. Mwishowe aliorodheshwa kwa usaili na kufanikiwa kati ya waombaji wawili waliochaguliwa.

“Ninawashauri wanawake wenzangu, unapofanya kazi usiwe 50-50 jitoe kabisa ili uone hicho unachokifanya ni kikubwa na kitu ambacho jamii inaweza kuona unafanya nini hivyo usifanye tu ilim-radi, fanya kitu kionekane na usiseme wewe ni mwanamke huwezi kufanya hapana, kazi zote zinafanyika vizuri na hakuna kazi ya mwanamke wala mwanaume,” anasema Sophia.

Anasema, “Leo hii mimi nafanya kazi kwenye machimbo na mimi ni mmo-ja wa viongozi wa timu ya uchimbaji wa chini kwa chini GGML, naendesha mitambo mikubwa kama motagreda, kijiko kinachotumika kwenye ujenzi wa barabara na ni Ofisa Mwajiri na pia nafanya kazi ya kuchoronga miamba.”

“Unadhani hizi kazi mimi naziwezaje, ni kujitoa kima-somaso na kuamua kwamba mimi ninaweza na sio kusema ni kujaribu, hakuna kujaribu katika maisha ni kufanya tena kwa weledi na uwajibikaji mkubwa, sasa hivi mimi natambulika na serikali yangu inanitambua kutokana na kazi yangu.”

Anawashauri wazazi kuwapeleka watoto wao shule kama Veta wakasome mambo ya miamba, wasiwaache kwa kusema kazi kama hizi ninazofanya ni ngumu hapana, kazi zote zinafanyika hata katika migodi ya dhahabu ya Geita wapo wanawake ambao ni wahandisi wakubwa na wanafanya kazi vizuri.

“Sasa hivi jamii inayonizunguka wanaona kitu ninachofanya, hata Serikali yangu ya Jamhuri ya Muungano ya Tanzania inaona ninafanya nini, inajua kile ambacho nina kifanya, hivyo tujivunie mabinti zetu kufanya mambo makubwa,”

“Leo wanawake tunafanya mambo makubwa kuliko hata wanaume ambao waliaminika zaidi hapo kipindi cha nyuma, leo Serikali ya Rais Magufuli inatupa kipaumbele wanawake, ninawashauri wanawake wenzangu tuen-delee kufanya kazi kwa nguvu zote ili tusimwangushe Rais wetu,”

“Watu wengi walikuwa wakinishangaa na kunikatisha tamaa, wengine wakaniambia namna nilivyo siwezi kufanya kazi katika mgodi ule lakini pia wakaniambia elimu yangu ni ndogo, kwa sababu ilikuwa ni ndoto yangu niling’ang’ana mpaka nikafikia kwenye ndoto zan-gu” “Hakuna mafanikio bila kujituma, hata kupata kazi katika mgodi wa GGML ni kutokana na bidii zangu kuonekana na naushukuru sana uongozi mzima kwa kuniona ni mwanamke ambaye nawe-za kufanya mambo makubwa,”

“Nawapongeza sana GGM kwa sababu wamekuwa wakijali wafanyakazi na hata maeneo ya kufanyia kazi yana usalama mkubwa kuliko sehemu yoyote ambayo nimeshawahi kufanya kazi, usalama ni kitu cha kwanza katika mgodi huu wa GGML,”

“Ninaendelea kujifunza vitu vingi sana katika mgodi huu hawataki kuona mtu ameumia sehemu yoyote ile ni usalama kwanza, mimi kama mwanamke najivunia kufanya kazi na GGML maana sijawahi ona watu wanaojali wafanya kazi sehemu nyingine yeyote ile nilikowahi kupita,”Pia, Sophia anamshauri Rais Magufuli kuendelea kuwapa kipaumbele wanawake kwa sababu anaamini ukimpa nafasi mwanamke hawezi kukuangusha.

“Namshukuru sana Rais Magufuli kwa kuona wanawake tunaweza na anaendela kutoa nafasi mbalimbali kwenye uongozi wa wanawake, hili anafanya vyema sana, wanawake wengi leo hii wanapambana kufanya kazi katika migodi ya madini maana mazingira yetu kwa wanawake ni mazuri kwa kweli, Rais amekuwa akinibariki sana, wanawake wa Tanzania sisi tuna nguvu na tukipewa nafasi tunafanya kweli kweli,” anasema Sophia.

Sophia ana ndoto ya kuwa kama Agnes Madili, Mhandisi wa Madini wa chini ya ardhi ambaye kwake ni kioo. “Agnes anafanya kazi nzuri, nimekutana naye huko Star na Comet na amekuwa akinitia moyo nisikate tamaa kamwe. Siku moja nataka kuwa mhandisi kama yeye, “anafafanua Sophia.