Ushirikiano wa JICA katika uendelezaji wa miundombinu ya usafirishaji Tanzania

Muktasari:

Shirika la Maendeleo la Kimataifa la Japan (JICA) ni miongoni mwa mashirika makubwa sana duniani ambalo hutoa misaada yake kupitia njia mbalimbali zikiwamo: misaada ya kiufundi, utoaji wa mikopo yenye masharti nafuu, kutoa misaada isiyokuwa na masharti ya kulipa na pia kupitia mpango wa kupeleka vijana wa kujitolea kutoka Japan kwenda kujitolea nchini Tanzania.

Utangulizi

Shirika la Maendeleo la Kimataifa la Japan (JICA) ni miongoni mwa mashirika makubwa sana duniani ambalo hutoa misaada yake kupitia njia mbalimbali zikiwamo: misaada ya kiufundi, utoaji wa mikopo yenye masharti nafuu, kutoa misaada isiyokuwa na masharti ya kulipa na pia kupitia mpango wa kupeleka vijana wa kujitolea kutoka Japan kwenda kujitolea nchini Tanzania.

Pamoja na hayo hivi karibuni JICA imepanua majukumu yake na kusaidia uwekezaji katika sekta binafsi. JICA ina ofisi 96 duniani kote, 28 miongoni mwa hizo zikiwa Kusini mwa Jangwa la Sahara. Tanzania ni miongoni mwa nchi zinazoongoza katika kupata misaada mikubwa katika eneo hilo.

Nchi nyingine zinazopata misaada mikubwa kutoka Japan ni Kenya, Ghana, Senegal na Zambia. Uendelezaji wa sekta ya usafirishaji ni moja ya sekta muhimu sana katika ushirikiano wa JICA nchini Tanzania kwani ushirikiano huo unachangia asilimia 27 katika ushirikiano wote wa JICA hapa nchini.

Ushirikiano huu unachangia sana katika ukuaji wa uchumi na upunguzaji wa umaskini. Uimarishaji wa sekta ya usafirishaji na utekelezaji wa lengo la 9 la Maendeleo Endelevu ya Kimataifa lisemalo “ujenzi wa miundombinu, kuimarisha viwanda na kuimari-sha ubunifu”.

Aidha ushirikiano huu unatekeleza malengo namba 11 na 17 yanayosisitiza umuhimu wa kuweka miji yetu na sehemu tunazoishi kuwa safi na salama na hivyo kuendeleza ushirikiano wa kimataifa kwa ajili ya maendeleo endelevu ya wote.

Ushirikiano wa JICA hauangalii tu wingi wa kitu kinachotolewa bali ubora wa kile kinachotolewa. Hivyo ushirikiano wa JICA unajali sana uimara na ubora wa kinachotolewa.

Hii ni kwa sababu kama msaada utatolewa kwa mfano wa kiwango cha chini katika eneo la miundombinu, miundombinu hiyo inaweza kuathiri maendeleo ya nchi katika kipindi cha muda mfupi/mrefu ujao.

Kutokana na ukweli huu JICA inatekeleza miradi yake kulingana na “Kanuni za Uwekezaji Bora katika Miundombinu” ambazo zilikubaliwa katika Mkutano wa Mataifa yaliyoendelea kiviwanda uliofanyika Osaka Juni 2019, yaani G20 Osaka Summit.

Aidha JICA inasaidia kuimarisha uhusiano kati ya mabara mawili ya Afrika na Asia kupitia bahari za Hindi na Pasifiki kwa kuwa eneo huru la bahari hizo mbili ni muhimu katika maendeleo ya kijamii na ya kiuchumi katika mabara hayo.

Kanuni za Uwekezaji Bora zilizokubaliwa katika Mkutano wa G20 Osaka Summit 2019

• Kutumia vizuri miundombinu kwa maendeleo endelevu

• Kuinua uchumi kutokana na hali halisi ya maisha

• Kuingiza mambo ya mazingira katika uwekezaji katika miundombinu

• Kujenga utayari dhidi ya majanga ya asili na majanga mengine kama hayo

• Kuingiza mambo ya kijamii katika uwekezaji katika miundombinu

• Kuimarisha usimamizi wa miundombinu

Uendelezaji wa usafirishaji mijini

Ujenzi wa msingi wa maendeleo ya usafirishaji Dar es Salaam

Ushirikiano wa kwanza wa JICA katika sekta ya usafirishaji hapa nchini ulianza na mradi wa ujenzi wa daraja la Selander jijini Dar es salaam mwaka 1980 – 1982.Mradi huu ulianza sanjari na ufunguzi wa Ofisi ya JICA hapa Tanzania mwaka huo huo wa 1980.

Baada ya mradi huo barabara nyingine kama ile ya Morogoro ilijengwa mwaka 1984 – 1987 ikifuatiwa na ujenzi wa barabara kadha wa kadha ambazo ziliunganisha eneo la kati ya Jiji upanuzi na uboreshaji wa barabara hizi uliimarisha sekta ya usafirishaji jijini kwa manufaa ya watumiaji wa barabara hizo.

JICA ilisaidia utekelezaji wa mradi huu baada ya mashauriano ya kina na Serikali ya Tanzania pamoja na vyombo vyake vya utekelezaji kama vile Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) ili kubaini mahitaji halisi ya uendelezaji wa miundombinu.

Kutokana na mashauriano hayo na Serikali ya Tanzania, JICA imetekeleza miradi mbalimbali ya barabara katika maeneo mbalimbali yaliyopo katika maeneo ya kuishi na ya biashara.

Miradi hiyo ilihusu sehemu zilizopo katikati ya Jiji la Dar es Salaam, Mtaa wa Mwinyijuma, barabara za Upanga, New Bagamoyo, Nelson Mandela na Morogoro.

Aidha barabara zilizopo maeneo ya Chang’ombe, Kariakoo, Mwananyamala, Ilala na Sinza zilirekebishwa. Barabara hizi zilikua msingi mzuri wa kusaidia maisha ya wakazi wa Dar es salaam kwa miongo kadhaa.

Mpango kabambe kwa maendeleo endelevuUshirikiano wa JICA hauishii tu katika ujenzi wa miundombinu. Ushirikiano huo unahusisha nyanja zote kuanzia upangaji wa mipango miji hadi uendelezaji wa rasilimali watu kwa kutumia uzoefu wake mkubwa kutoka nchi nyingine za dunia.

Kwa mfano mwaka 2007, JICA kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais (Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa – TAMISEMI), ambayo wakati huo ilikua inaitwa Ofisi ya Waziri Mkuu – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa – TAMISEMI) ilisaidia katika kutayarisha Sera na Mpango Kabambe wa Usafirishaji wa Dar es Salaam (2007 – 2008).

Ili kuhakikisha kwamba miradi iliyoainishwa katika mpango huo inatekelezwa, mashauriano yalifanyika baina ya wadau mbalimbali kwa madhumuni ya kuwa na msimamo wa pamoja katika utekelezaji huo.

Kutokana na jitihada hizo kwa sasa tunaweza kuona miradi mbalimbali ambayo ni zao la Mpango huo ikiwa katika hatua mbalimbali za utekelezaji.

Kwa mfano Mradi wa Mabasi ya Mwendo Kasi Dar es salaam (BRT) ulianzishwa mwaka 2016 ukihusisha Barabara ya Morogoro. Aidha ujenzi wa daraja Jipya la Selandar unaendelea na litakapomalizika litapunguza msongamano wa magari katika Barabara ya Ali Hassan Mwinyi.

Isitoshe barabara ya Bandari iko katika mpango huo wa Mabasi ya Mwendo kasi. Ujenzi wa barabara muhimu ya juu ya Mfugale Mradi wa hivi karibuni ambao ulijengwa kwa ushirikiano wa JICA ni mradi wa Ujenzi wa Daraja la Juu eneo la Tazara (2015 – 2018).

Chini ya mradi huu daraja la juu la kwanza nchini Tanzania liitwalo Mfugale lilijengwa ili kuondoa msongomano wa magari katika makutano ya Barabara za Nyerere na Nelson Mandela katika eneo la Tazara.

Kabla ya mradi huo ilichukua muda wa saa mbili kutoka Uwanja wa Ndege kufika Mjini. Kwa sasa inachukua chini ya dakika 30 kusafiri njia hiyo hiyo. Pamoja na mafanikio hayo ya kutia moyo ubora wa uendeshaji wa mradi huo pia ulithibitika.

Ujenzi wa daraja la Juu la Mfugale ni uthibitisho tosha wa kuonyesha ubora wa ujenzi husika. Kwa ushirikiano kati ya mkandarasi wa Kijapani aliyejenga daraja hilo na wafanyakazi wa Kitanzania, ujenzi wa daraja hilo ulifanyika kwa saa milioni 2.5 (2.5 million man-hours) bila kutokea ajali yoyote.

Utekelezaji wa mradi huu si tu kwamba uli-toa ajira kwa Watanzania bali pia uliwawezesha Watanzania hao kupata uzoefu kutoka kwa wakandarasi wa Kijapani.

Uendelezaji wa lango la Uchumi (Economic Corridor)

Kuanzia miaka ya 2000, ushirikiano wa JICA ulisambazwa nje ya Dar es salaam. Pamoja na kushughulikia changamoto mbalimbali za miradi husika, JICA pia ilisambaza ushirikiano wake katika kutayarisha Mpango Kabambe wa Usafirishaji na Biashara wa mwaka 2013.

Mpango huu ulizingatia umuhimu wa kuunganisha mikoa na pia nchi za jirani ili kusukuma maendeleo ya kiuchumi na biashara na hivyo kuifanya Tanzania iwe kitovu cha uchumi katika ukanda huu.

Isitoshe katika mkutano uliofanyika Tokyo mwaka 2013 kuhusu maendeleo ya Afrika (TICAD V) JICA iliazimia kusaidia maendeleo ya kiuchumi ya kanda (economic development corridors).

Kutokana na maazimio hayo miradi kadhaa ilitekelezwa kama vile Trans African Highway No. 4, Mtwara Corridor na Central Corridor n.k. Maendeleo ya lango la Mtwara (Mtwara corridor) Lango la Mtwara (Mtwara Corridor) huunganisha maeneo ya kusini mwa Tanzania na Bandari ya Mtwara ambayo ni bandari ya tatu kwa ukubwa nchini Tanzania.

Maeneo haya yana rasilimali kubwa katika sekta za madini na kilimo. Kutokana na ukweli huu miradi kadhaa ilitekelezwa. Miradi hiyo ni pamoja na: Barabara ya Masasi – Mangaka (2007-2010), mradi wa kusaidia Sekta ya barabara I (2010 – 2016), Mradi wa Kusaidia Sekta ya Barabara II (2013 – 2017), Kutokana na miradi hii barabara za lami zenye urefu wa kilomita 450 zilijengwa na hivyo kupunguza muda wa usafirishaji na gharama mbalimbali kwa asilimia 30 hadi 40.

Barabara ya Trans African Highway No. 4 inaunganisha bara la Afrika kuanzia mwaka 2007, JICA, kwa kushirikiana na Benki ya Maendeleo ya Afrika ilifadhili ujenzi wa barabara kuu ya kutoka Iringa hadi Namanga mpakani mwa Tanzania na Kenya chini ya miradi kadha wa kadha.

Miradi hiyo ni pamoja na: Mradi wa Barabara ya Arusha-Namanga Athi River (2007 – 2014), Mradi wa Kusaidia Sekta ya Barabara (2010 – 2016), na Mradi wa Kusaidia Sekta ya Barabara Awamu ya II (2013 – 2017).

Chini ya miradi hii jumla ya barabara za lami zenye urefu wa kilometa 550 zilijengwa ambazo zilipitia katikati ya jiji la Dodoma. Kumalizika kwa miradi hii kulikua na umuhimu wake sio tu kwa Tanzania bali pia kwa Afrika nzima.

Hii ni kwa sababu kubwa kuwa kwa kupitia miradi hii sehemu kubwa za Afrika ziliunganishwa kupitia hiyo Trans African Highway No. 4. Wazo la kuwepo na Trans African Highways tisa lilia-sisiwa na Tume ya Uchumi ya Umoja wa Mataifa kwa Afrika (UNECA) mwaka 1970 ili kuwezesha usafirishaji wa haraka wa watu na mizigo katika bara la Afrika.

Barabara kuu ya Trans African Highway No. 4 inaunganisha bara la Afrika kutoka Afrika ya Kusini hadi Misri, umbali wa kilomita zaidi ya 10,000. Kutokana na miradi hii imeshuhudiwa kuwa hatimaye baada ya nusu karne bara la Afrika limeunganishwa kwa barabara nzuri.

Uanzishaji wa vituo vya huduma moja mipakani (One Stop Border Post (OSBP) Kwa madhumuni ya kuimarisha biashara katika kanda vituo ambavyo hutoa huduma zote mahali pamoja (One Stop Border Post (OSBP) vilianzishwa.

Katika vituo hivyo huduma zote za kuingia na kutoka nchi moja kwenda nyingine hutolewa katika sehemu za mpakani. Hivyo shughuli za watu wanaovuka mpaka, au mizigo na magari yanayovushwa hushughulikiwa katika sehemu moja tu.

JICA ilisaidia Jumuiya ya Afrika Mashariki katika uanzishwaji wa kisheria wa vituo vya OSBP. Aidha kuanzia mwaka 2007, JICA kwa ushirikiano na Shirika la Dunia la Forodha (World Customs Organization (WCO), ilifanya mafunzo ya kuongeza uwezo kwa wafanyakazi wa Mamlaka za Mapato za Jumuiya ya Afrika Mashariki ikiwemo Mamlaka ya Kodi Tanzania.

Pamoja na kuboresha utendaji wa kawaida, ushirikiano katika uendelezaji wa miundombinu ya usafirishaji uliongeza ufanisi katika usafirishaji na hivyo kuongeza biashara baina ya nchi husika JICA ilisaidia ujenzi wa kituo cha OSBP eneo la Rusumo katika mpaka wa Tanzania na Rwanda. Mradi huu ulipunguza kwa kiasi kikubwa muda wa kuvuka mpaka kutoka saa 8 na dakika 42 kabla ya mradi hadi saa 2 na dakika 20 baada ya mradi.

Mfano mwingine ni Namanga katika mpaka wa Tanzania na Kenya. Mizigo inayosafirishwa kutoka Tanzania kwenda Kenya kupitia Namanga imeongezeka kwa zaidi ya mara mbili (2.8%) katika muda wa miaka mitano iliyopita kutoka tani 145,000 mwaka 2014 hadi kufikia tani 409,000 mwaka 2018.

Ushirikiano wa JICA katika siku zijazo

Kuendeleza rasilmali watu Pamoja na kuendeleza miundombinu ya usafirishaji, ni lazima pia kuchukua hatua stahiki kuhakikisha kuwa miundombinu iliyoboreshwa inatumika vizuri.

Ili kuhakikisha kua miundombinu iliyojengwa inatumika vizuri JICA imekuwa inatoa mafunzo mbalimbali kwa watu wanaosimamia miundombinu hiyo. Kupitia mpango wa JICA wa mafunzo (KCCP) Watanzania wengi wamekua wakipewa mafunzo nchini Japan na katika nchi nyingine kuendeleza ujuzi wao.

Tangu mpango huu wa mafunzo uanzishwe zaidi ya Watanzania 21,000 wameshapokelewa kwa mafunzo mbalimbali nchini Japan. JICA itaendelea kutoa mafunzo hayo katika sekta ya usafirishaji na katika sekta nyingine katika siku zijazo.

Uendelezaji wa majiji ya Dodoma na Dar es Salaam

Idadi ya watu wanaoishi Dar es salaam inatarajiwa kuongezeka na inakadiriwa kwamba idadi hiyo itazidi milioni 12 ifikapo mwaka 2040 na kwa sababu hiyo mahitaji ya usafiri yataongezeka mara mbili ifikapo mwaka 2027.

Kutokana na ukuaji huo wa haraka wa idadi ya watu hivi karibuni JICA ilishirikiana na Serikali kuhuisha Mpango Kabambe wa Usafirishaji wa Dar es salaam wa mwaka 2018 kwa kuainisha miradi muhimu kadha wa kadha ikizingatiwa kuwa Dar es salaam itakua Jiji kubwa (Mega City).

Usafirishaji wa umma wa mjini kwa kutumia njia ya reli pamoja na usafiri wa mabasi ya mwendo kasi (BRT) utaendelezwa ili kuhakikisha kuwa usafiri mjini unakua mzuri zaidi na wa kuaminika.

Aidha utumiaji wa zana za kisasa kabisa za usafirishaji (Intelligent Transport System) pamoja na ujenzi wa madaraja ya juu katika sehemu za makutano utasaidia kuhimili ongezeko la magari mjini.

JICA itaendeleza ushirikiano wake na Serikali ya Tanzania ili kufanikisha miradi iliyoainishwa katika Mpango Mpya Kabambe wa Usafirishaji Dar es salaam na hivyo kuisaidia Dar es salaam kutoka kwenye Jiji la kawaida na kuwa Jiji kubwa kabisa.

Katika Mpango huo, JICA pamoja na Serikali ya Tanzania walitoa pendekezo liitwalo “Transit-Oriented-Development (TOD)”. Pendekezo hili linasisitiza mabadiliko kutoka matumizi ya magari ya kawaida kwenda katika matumizi ya usafiri wa umma. Pendekezo hili linatokana na ukweli kuwa kuongeza uwezo wa barabara kuhimili ongezeko la matumizi ni gumu.

Aidha matumizi ya njia mbadala za usafirishaji kama vile MRT station na uboreshaji wa maeneo yaliyo karibu na vituo vya umma utasaidia kuboresha usafirishaji mijini. Mpango wa TOD utachangia katika kuongeza mapato ya MRT na MRT inaweza kutumia mapato hayo kuwekeza katika miradi mingine.

Pamoja na hayo, JICA inafikiria kuen-deleza ushirikiano wake katika Jiji la Dodoma, Mji mkuu wa Tanzania. Kutokana na jitihada kubwa za viongozi wa Serikali ya Tanzania, Jiji la Dodoma linakua kwa kasi sana.

Ili kuhimili ongezeko la hitaji la usafirishaji Dodoma, JICA kwa sasa inafanya upembuzi yakinifu kwa lengo la kujua mahitaji halisi ya barabara za katikati ya jiji hilo. Maendeleo ya malango ya uchumi (economic corridors) na uboreshaji wa huduma za usafiri salamaJICA itaendeleza ushirikiano wake katika kuendeleza miradi ya “corridor development”.

Kwa sasa miradi ambayo iko katika hatua za awali za mipango ni miwili: Mradi wa ukarabati wa Bandari ya Kigoma na Mradi wa Uboreshaji wa barabara ya Arusha hadi Holili. Miradi hii itagusa maswala ya usalama pamoja na uboreshaji wa usafirishaji katika malango hayo ya uchumi (economic cor-ridors).

Bandari ya Kigoma ni kituo muhimu cha usafirishaji katika ukanda wa kati ambayo unaunganisha Tanzania na nchi jirani za Burundi, na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kupitia Ziwa Tanganyika.

Wakati usafiri wa majini ni muhimu kwa wakazi wa maeneo husika sehemu ya abiria ya kusubiria meli (passenger terminal) iko katika hali mbaya na wasafiri hawawezi kupanda meli moja kwa moja.

Hivyo JICA imekua katika mazungumzo na Serikali ya Tanzania kwa lengo la kukarabati sehemu hiyo kwa usalama wa wasafiri hao.Barabara ya Arusha - Holili ni barabara kuu ya usafiri kati ya Arusha na Kenya.

Barabara hii itakapokamilika itaongeza uwezo wa usafirishaji katika eneo hilo kwa kupanua sehemu zilizo na msongamano mkubwa. Aidha mradi huu utakidhi hitaji la usalama katika daraja la Kikafu ambalo liko katikati ya Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro na mji wa Moshi. Eneo la Kikafu lina sehemu hatarishi kama vile maporomoko makali, n.k.

Ili kumaliza matatizo haya JICA na Serikali ya Tanzania wako katika mazungumzo kuhusu kujenga daraja jipya la Kikafu ambalo litakuwa na urefu wa mita 500.Inatazamiwa kwamba kwa kupitia miradi hii, ambayo inatarajiwa hivi karibuni, JICA itachangia katika maendeleo ya Tanzania na hivyo kukuza zaidi uhusiano wa muda mrefu kati ya Tanzania na Japan.