Magufuli 2015

Rais Jakaya Kikwete akikumbatiana na Rais Mteule, Dk John Magufuli alipokuwa akimpongeza baada ya Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Jaji Mstaafu Damian Lubuva kutangaza rasmi matokeo ya Uchaguzi Mkuu, ambako walifuatilia kwa pamoja matangazo hayo ya moja kwa moja kupitia vituo vya televisheni wakiwa Ikulu, Dar es Salaam jana. Picha na Ikulu

Muktasari:

Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Jaji Damian Lubuva alimtangaza Dk Magufuli kuwa Rais katika siku ambayo kada huyo wa CCM alikuwa akiadhimisha miaka 56 ya kuzaliwa kwake, ikiwa pia ni siku ya 108 tangu apitishwe na Mkutano Mkuu wa CCM kuwania urais, Julai 12.

Dar es Salaam. Dk Magufuli ndiye Rais mpya wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania atakayeongoza Serikali ya Awamu ya Tano baada ya kuwashinda wagombea wengine kutoka vyama 10 vilivyosimamisha wagombea saba katika uchaguzi uliokuwa mbio za mafahari wawili.

Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Jaji Damian Lubuva alimtangaza Dk Magufuli kuwa Rais katika siku ambayo kada huyo wa CCM alikuwa akiadhimisha miaka 56 ya kuzaliwa kwake, ikiwa pia ni siku ya 108 tangu apitishwe na Mkutano Mkuu wa CCM kuwania urais, Julai 12.

Jaji Lubuva aliwaambia watu waliokuwa kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere kuwa Dk Magufuli alipata kura 8,882,935, ambazo ni sawa na asilimia 58.46, ikiwa ni pungufu ya asilimia takribani tatu ya ushindi wa Rais Jakaya Kikwete wa mwaka 2010, lakini mkubwa kwa tofauti ya takribani kura milioni 3 alizopata kiongozi huyo wa Serikali ya Awamu ya Nne.

Mgombea wa Chadema, Edward Lowassa, ambaye alikuwa akiungwa mkono na vyama vya NLD, CUF na NCCR Mageuzi, alishika nafasi ya pili, akiweka rekodi ya kuzoa kura 6,728,480, ambazo ni asilimia 39.97, kiwango ambacho hakijawahi kufikiwa na wagombea kutoka vyama vya upinzani tangu siasa za ushindani zirejeshwe mwaka 1992.

Kwa mujibu wa Jaji Lubuva, jumla ya kura halali zilizopigwa ni 15,193,862, huku kura 402,248 zikiharibika. Alisema waliojiandikisha kupiga kura walikuwa 23,161,440 na waliopiga kura walikuwa 15,589,639, idadi ambayo ni mara mbili ya watu waliojitokeza mwaka 2010. Wapiga kura hao walitoka katika majimbo 264.

Hakukuwapo na shamrashamra ndani ya ukumbi huo wa kisasa uliopo makutano ya barabara ya Shaaban Robert na Garden Avenue.

Ndani ya ukumbi huo, CCM iliongozwa na katibu wake mkuu, Abdulraham Kinana pamoja na mjumbe wa kamati ya kampeni ya chama hicho, January Makamba. Vyama vingine vitano vilikuwa na uwakilishi, isipokuwa Chadema, ambayo awali iliwasilisha malalamiko yake, lakini ikaagizwa iyapeleke ofisi za NEC.

Nje ya ukumbi huo kulikuwa na ulinzi mkali wa polisi ambao waliweka vizuizi kwenye barabara zinazopita karibu na ukumbi huo, na hivyo kufanya eneo hilo kuwa tulivu tofauti na siku nyingine.

“Tumeridhishwa na imani kubwa ya wananchi kwa CCM,” alisema Kinana mara baada ya matokeo kutangazwa.

“CCM ina kazi ya kutekeleza ilani yake kikamilifu ili kuwaletea wananchi maendeleo ambayo tumeyaahidi.”

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Ualimu cha Chang’ombe (Duce), Dk Kitila Mkumbo alisema Dk Magufuli alipitia njia ngumu kupata mafanikio hayo.

“Amepambana na ushindani mkubwa,” alisema Dk Kitila aliyeongea na Mwananchi baada ya kutangazwa kwa matokeo hayo ya uchaguzi ambao ulikuwa ni vita baina ya Dk Magufuli na Lowassa, ambaye ni Waziri Mkuu wa kwanza kukihama chama tawala na kugombea urais kwa tiketi ya upinzani.

“Huu uchaguzi ulikuwa ni tofauti na ile ya miaka iliyopita. Sasa ana kazi kubwa ya kutuunganisha ili tuwe wamoja tushiriki kufanya kazi kwa maendeleo ya nchi yetu.”

Vyama vingine vilivyoshiriki ni ACT-Wazalendo, ambacho kilimsimamisha Anna Mghwira, ambaye ameshika nafasi ya tatu, akiwa pia ni mwanamke wa pili kupitishwa na chama chake kuwania urais.

Mwanamke wa kwanza kugombea urais nchini ni Anna Claudia Senkoro kupitia PPT Maendelea ambaye alipata asilimia 0.17 katika uchaguzi wa mwaka 2005.

Lakini, Mgwira ambaye pia ni mchambuzi wa masuala ya kisiasa, alipata kura 98,763, sawa na asilimia 0.65, wakati mgombea wa ADC, Chief Lutalosa Yemba alipata kura 66,049 sawa na asilimia 0.43.

Mgombea wa Chaumma, Hashim Rungwe alipata kura 49,256 sawa na asilimia 0.32, huku Janken Kasambara wa NRA akipata kura 8,028 sawa na asilimia 0.05.

MacMillan Lyimo wa TLP alipata kura 8,198 sawa na asilimia 0.03 na mgombea wa UPDP, Fahmi Dovutwa alipata kura 7,785 sawa na asilimia 0.05.

Ilivyokuwa

Kabla ya kumtangaza mshindi, Jaji Lubuva alisema Chadema na Chaumma hawakutia saini hati ya kuridhia matokeo. Chadema haikubaliani na matokeo hayo kwa madai kuwa yanatofautiana na matokeo yaliyotangazwa vituoni.

Lakini Jaji Lubuva alisema kitendo cha vyama hivyo viwili kutosaini hati hiyo, hakuizuii NEC kumtangaza mshindi wa urais.

Jaji Lubuva alisema kuwa kwa mujibu wa ibara ya sita ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano, mgombea urais atatangazwa kwa wingi wa kura, atatambulika kisheria na mgombea mwenza atakuwa Makamu wa Rais.

Ilipotimu saa 10:05 jioni, Jaji Lubuva alimtangaza waziri huyo wa zamani wa Ujenzi kuwa mshindi wa mbio za urais na Samia Suluhu Hassan kuwa Makamu wa Rais, akiwa ni mwanamke wa kwanza kushika nafasi hiyo tangu nchi ipate uhuru mwaka 1961.

Baada ya kumtangaza mshindi, Jaji Lubuva alisema tume yake itakamilisha mchakato huo leo kwa kumkabidhi mshindi cheti chake kabla haijaliacha jukumu kwa wizara husika ili iandae sherehe za kumuapisha kabla hajaanza majukumu yake ya kiofisi.

Mkurugenzi wa uchaguzi, Kailima Kombwey aliwatangazia wajumbe waliokuwepo ukumbini hapo kwamba shughuli hiyo itafanyika kwenye ukumbi wa Diomond Jubilee.

“Tume imekamilisha wajibu wake. Kila mmoja atakayekuwa na nafasi anakaribishwa kuhudhuria dhifa ya kuwakabidhi washindi vyeti vyao,” alisema.

Katibu wa Chaumma wa Mkoa wa Dar es Salaam, Amiri Kaluta alikuwapo ukumbini, licha ya kutoridhia matokeo hayo.

“Wananchi wa Zanzibar wamefutiwa uchaguzi wao ilhali walimchagua rais anayetangazwa leo (jana). Naamini kwenye kutochanganya haki na batili na kwa taarifa tulizonazo ni kwamba NEC haikuwa na maofisa wake kule (Zanzibar),” alisema Kaluta akirejea uamuzi wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar kufuta matokeo ya uchaguzi.

Wawakilishi wa vyama vya siasa waliokuwepo walisaini matokeo hayo ikiwa ni moja ya hatua muhimu za kumtangaza rais.

Safari ya Dk Magufuli

Magufuli alianza rasmi safari yake kuelekea Ikulu Alhamisi ya Juni 4, mwaka huu kwa kuchukua fomu ya kuomba uteuzi ndani ya chama chake, akiwa miongoni mwa wagombea wengine 38.

Tofauti na wagombea wengine walioenda kuchukua fomu wakizungukwa na wapambe, Magufuli alifanya kazi hiyo kimyakimya.

Alienda kwenye ofisi za makao makuu ya CCM mjini Dodoma akitokea kwenye kikao cha Bunge la Bajeti wakati likiwa kwenye mapumziko.

Julai 11, alipitishwa na Kamati Kuu ya CCM kuwa mmoja wa makada watano waliotakiwa kupitishwa na Halmashauri Kuu kabla ya kupelekwa Mkutano Mkuu, uamuzi ambao ulipingwa na baadhi ya wajumbe wa kamati hiyo ambao walisema katiba ilikiukwa.

Hata hivyo, licha ya mzozo mkubwa uliotokea kwenye Halmashauri Kuu kupinga uamuzi wa Kamati Kuu kutompitisha Lowassa, waziri huyo wa zamani wa Ujenzi alishika nafasi ya kwanza kati ya makada watatu na alipata kura nyingi kutoka kwa wajumbe wa Mkutano Mkuu.

Walioingia katika hatua ya tano bora ni Dk Asha-Rose Migiro, Amina Salum Ali, January Makamba na Bernard Membe.

Baadaye ulifanyika mchujo uliowamwaga Membe na Makamba na baada ya chujio la NEC, wajumbe wote wa Mkutano mkuu wa chama hicho, walimpa kura 2104 sawa na Asilimia 87.1.

Agosti 3, Dk Magufuli alichukua fomu ya kuwania urais kupitia CCM na kuanza kazi ya kusaka wadhamini mikoani.

Tangu azindue kampeni Agosti 22, Dk Magufuli amekuwa akisisitiza neno “sitawaangusha”, akiwasihi wananchi wenye itikadi tofauti kumpigia kura ili afanye mabadiliko.

Aliwashangaza wengi kwa kutotanguliza jina CCM kwenye kampeni zake na badala yake kutumia zaidi neno “Serikali ya Magufuli” hadi siku za mwisho za kampeni zake alipoanza kukinadi chama hicho.

Kampeni zake zilipambwa na kauli mbiu ya “hapa kazi tu” ikinogeshwa na mazoezi ya “push up” kuonyesha utimamu wake wa afya.

Mtazamo

Akizungumzia matokeo hayo, mwakilishi wa NRA, Salum Joseph alisema wamepokea kwa mikono miwili na wanatarajia ushirikiano kati ya Serikali ya Dk Magufuli na vyama vya siasa. “Kwenye kampeni zake, Magufuli amekuwa akiahidi kwamba akishinda urais atashirikiana na vyama vyote. Ninaamini atatusikiliza na kuchukua mawazo yetu ambayo tunaamini ni mazuri katika ujenzi wa taifa,” alisema.

Kwa upande wake, mwakilishi wa UPDP, Felix Makuwa alilalamikia ukata unaovikabili vyama vya siasa wakati wa kampeni kwa sababu havipati ruzuku kwa ajili ya kuzunguka nchi nzima kunadi sera zao ambazo alisema anaamini ni nzuri.

Magufuli kukabidhiwa cheti

Sherehe ya kumkabidhi cheti cha ushindi Dk Magufuli itafanyika leo katika Ukumbi wa Diamond Jubilee na zitahudhuriwa na viongozi mbalimbali, akiwamo Rais Jakaya Kikwete ambaye anamaliza muda wake.

Wengine ni Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda na Mawaziri wakuu wastaafu.

Viongozi wengine walioalikwa kwenye hafla hiyo ni wagombea urais na wagombea wenza, makamu wa kwanza wa rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad, Spika wa Bunge la Muungano, Anna Makinda na Spika wa Baraza la Wawakilishi, Pandu Amir Kificho.

Imeandikwa na Joyce Mmasi, Julius Mathias na Peter Elias.