Wasomi waeleza sababu mawaziri kuanguka

Muktasari:

Wananchi wanataka viongozi wa kuwatumikia kulingana na hali ya mabadiliko

Dar es Salaam. Wasomi nchini wametoa maoni tofauti kuhusu kuanguka kwa baadhi ya mawaziri na wabunge maarufu, kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka huu, kwamba hali hiyo inadhihirisha wananchi wanataka mabadiliko kwenye utendaji.

Pia, wamesema anguko hilo lililotoa nafasi zaidi kwa wabunge wa upinzani ni ishara ya kukua kwa demokrasia ya vyama vingi.

Tangu yalipoanza kutangazwa matokeo ya uchaguzi mkuu uliofanyika Jumapili, mawaziri na naibu mawaziri zaidi ya watano na wabunge wengine maarufu kwenye Bunge la Kumi wameshindwa kutetea majimbo yao.

Mawaziri hao walioanguka ni Stephen Wasira, Anne Kilango, Dk Steven Kebwe, Christopher Chiza, Aggrey Mwanri na Godfrey Zambi.

Akizungumzia matokeo hayo jana, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Richard Mbunda alisema wananchi wamefanya uamuzi huo kwa sababu viongozi hao wamekaa madarakani muda mrefu kwa hiyo hata utendaji wao umepungua.

“…Wameona muda wao wa kukaa bungeni umetosha, wanataka mabadiliko ya wabunge wapya na ndiyo maana wamefanya maamuzi ya kuwachagua wabunge wapya kwenye majimbo ambayo yalikuwa na wabunge waliotumikia majimbo yao kwa muda mrefu,” alisema Mbunda.

Mbunda alisema kudondoka kwa mbunge wa Bunda, Wasira siyo kazi ndogo. “Lazima uwe umejipanga kisera, ndiyo maana aliyepambana naye ameshinda kwa sababu wananchi wa jimbo hilo wameona anafaa,” alisema.

Kauli hiyo iliungwa mkono na Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Ruaha, Profesa Gaudence Mpangala ambaye alieleza sababu tatu za ‘vigogo’ hao kuangushwa kwenye majimbo yao akisema uchaguzi wa mwaka huu umebebwa na kaulimbiu ya mabadiliko, ndiyo maana wananchi wameamua kufanya uamuzi huo.

“Labda wameona wazee hawataweza kuendana na mabadililo wanayotaka,” alisema Profesa Mpangala aliyetaja sababu ya pili kuwa ni mwamko wa kisiasa hasa kwa upinzani na kukua kwa demokrasia ya mfumo wa vyama vingi.

“…Hii ya sasa ni mara mbili zaidi ya uchaguzi wa mwaka 2010. Ukilinganisha namna ambavyo upinzani umechukua nafasi hizo ni wazi nafasi yao inazidi kupanuka kila uchaguzi,” alisema Mpangala.

Alitaja sababu ya tatu kuwa ni mahitaji ya jimbo husika huku akitolea mfano wa mbunge teule wa jimbo la Bunda, Ester Bulaya kwa kuonyesha ukaribu zaidi na wananchi, jambo lililochangia kutwaa ushindi wa jimbo hilo dhidi ya Wasira, ambaye alikuwa mbunge wa jimbo hilo kwa zaidi ya miaka mingi.

Profesa Damian Gabagambi wa Chuo Kikuu cha Sokoine (SUA) alisema ongezeko la wabunge wa upinzani na kuanguka kwa baadhi ya wabunge waliokuwa wanashikilia majimbo kwa miaka mingi ni ishara ya kukua kwa demokrasia.

“Hii itakuwa chachu ya maendeleo kwa sababu hao wabunge waliochaguliwa watafanya kazi kwa bidii kwa kuwa hawatakuwa na uhakika wa kuchaguliwa tena baadaye,” alisema Profesa Gabagambi.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu Huria Tanzania (OUT) Hamad Salim alisema, “Wazee wanashindwa kwenda na kasi ya maendeleo ndiyo maana wananchi wamewachagua hao walioona wanafaa.”

Alisema nyakati zimebadilika na kwamba wale waliokuwa wanaamini uzee ni hekima siyo hivyo tena, wananchi wanataka viongozi wa kuwatumikia kulingana na hali ya mabadiliko.

Akichangia hoja hiyo, Profesa Bakari Mohammed wa UDSM, alisema siasa inabadilika na upinzani wa kisiasa ni mkubwa.

“Wanasiasa wanatakiwa kujifunza kutokana na hili, kwamba nafasi wanazopata siyo za kudumu. Wanapopata nafasi wanatakiwa kwa miaka mitano wanatakiwa kuonyesha utendaji mzuri,’’ alisema.