Miguna atua Canada, apokewa na kundi la watu

Muktasari:

Aulizwa kuhusu Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta na Makamu wake, William Ruto.


Toronto. Mtu aliyejitangaza kuwa ni jenerali wa Vuguvugu la Kuikaidi Serikali (NRM), Miguna Miguna aliyefukuzwa Kenya Februari 6, 2018 amewasili nchini Canada mapema leo Februari 8, 2018 na kupata mapokezi makubwa.

Miguna alisafirishwa kwa ndege ya Shirika la KLM Juzi usiku kutoka Nairobi kwenda Amsterdam, Uholanzi kisha Canada.

Kundi la watu lililokuwa likimsubiri katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Toronto, Canada limempokea mwanasiasa huyo na kumkabidhi maua.

 

“Karibu jenerali! Karibu nyumbani,” amesema mwanamke mmoja wakati akimkaribisha mwanasiasa huyo alipowasili.

Mwanamme mwingine amesikika akisema, “Miguna…. Miguna, vipi hujambo?”, kujibiwa na mwanasiasa hiyo, “Nimechoka.” Kisha mwanaume huyo akaendelea kuzungumza, “Wakenya wanakutazama wewe, wangependa kusikia neno kutoka kwako.”

 

Katika majibu yake kwa mwanamke huyo Miguna amesema, “Hapana, leo nataka nikaoge, sijaoga kwa muda wa siku sita au saba hivi. Hivyo nahitaji kupata wasaa wa kuoga vizuri, nimkumbatie mke wangu, watoto wangu na kisha nile vizuri. Sijala kwa wiki moja na baada ya hapo nitaweza kuzungumza chochote.”

 Katika mazungumzo hayo mwanamke huyo aliongeza neno, “Ungependa kuwaambia nini Uhuru (Kenyata-Rais wa Kenya), Ruto (William-Makamu wa Rais) na Matiang’i (Fred-Waziri wa Mambo ya Ndani)?” na kujibiwa na Miguna, “Njoo bibie, njoo,” amejibu Miguna na kuamsha kicheko kwa watu waliofika uwanjani hapo.

Serikali ya Kenya imesema imemnyang’anya uraia wa Kenya kwa sababu ameasi  uraia wake wa asili miaka kadhaa iliyopita na hakujishughulisha kuomba tena.

Miguna alijitangaza kuwa ni jenerali tawi la hamasa la muungano wa Nasa kundi ambalo limepigwa marufuku nchini humo.

Alikamatwa kwa kosa la kusimamia kiapo  cha kiongozi wa Nasa Raila Odinga katika viwanja vya Uhuru Park, Nairobi.