Makato ya benki kwa wateja akaunti za akiba yanakera

LAUDEN MWAMBONA

Muktasari:

  • Taarifa zinaeleza kuwapo kwa watu wanaoficha fedha maeneo mbalimbali ikiwamo kwenye magunia, mapipa, kuzichimbia shimoni au kuweka kwenye mito na wengine wanachimbia plastiki chini ya ardhi katika mashamba yao.

Kwa nchi zilizoendelea, suala la kutunza fedha hufanywa benki lakini kwa upande wa nchi za dunia ya tatu watu wengi bado wanaendelea kutunza kwenye maeneo wanayoyajua wao.

Taarifa zinaeleza kuwapo kwa watu wanaoficha fedha maeneo mbalimbali ikiwamo kwenye magunia, mapipa, kuzichimbia shimoni au kuweka kwenye mito na wengine wanachimbia plastiki chini ya ardhi katika mashamba yao.

Hali hiyo ipo licha ya maofisa wa benki na mitandao ya simu kuhamasisha watu kufungua akaunti za kutunza fedha.

Uchunguzi unaonyesha watu wengi wanasita kuweka fedha zao benki au kwenye mitandao ya simu kutokana na makato kuwa makubwa na mengi yasiyozingatia haki.

Wakitoa maoni yao kuhusu sababu za watu wengi kuendelea kutunza fedha kwa kutumia njia za kijima badala ya kuweka benki, baadhi ya wananchi wanasema ni kutokana na kuwapo kwa makato ya fedha yasiyozingatia uhalisia.

Mkurugenzi wa kampuni ya AB & ANN Security Service Limited inayofanya kazi zake mikoa ya nyanda za juu kusini, William Mwanjala anasema huduma za benki nyingi si rafiki kwa wateja wanaotaka kutunza fedha.

Mwanjala ambaye aliwahi kufanya kazi benki miaka ya 1990, anasema kitendo cha benki kukata fedha kila mwezi kwenye akaunti za akiba kwa wateja wanaodunduliza kidogokidogo kinawakatisha tamaa watu wengi.

Kwa mfano, mtu akiweka Sh20,000 kwenye akaunti ya akiba na kuziacha baada ya mwaka mmoja atakuta fedha zake zimebaki Sh5,000 jambo ambalo wengi wanaamini si sawa.

Hoja hiyo pia inaungwa mkono na Gwamaka Abel wa Soko Matola jijini Mbeya ambaye anasema miaka ya 1980 na 1990, benki zilikuwa zinawaongezea fedha kidogo wateja kila Desemba lakini sasa hivi hicho kitu ni nadra.

Anasema tofauti na miaka hiyo, benki nyingi sasa zinawakata wateja wanaotunza fedha kila mwezi ambazo huitwa gharama za uendeshaji wa akaunti husika. Nilifanya mjadala na baadhi ya maofisa wa benki nne tofauti kuhusu makato hayo na haya ndiyo yalikuwa majibu yao kuhusu suala hili ambalo wanasema ni gharama za utunzaji wa fedha kila mwezi.

Mmoja alisema, “kwa mfano benki ninayoitumikia inakata Sh3,540 kila mwezi, mwingine akasema wao hukata Sh1,888 na ofisa wa benki ya tatu akasema wanakata Sh1,900 na wa benki ya nne naye akasema wanakata Sh1,300 kila mwezi kutoka kwenye kila akaunti ya mteja.

Lakini ofisa mwinginne wa benki alisema benki yao haikati makato hayo badala yake hutoa faida kila mwisho wa mwaka kulingana na kiwango kitakachokutwa kwenye akaunti ya mteja.

Kutokana na ukweli nilioubaini kwa mazungumzo yangu na maofisa wa benki hizo tofauti, napenda kuzishauri benki nyingine ziache kuwakata wateja wanaodunduliza fedha kwenye akaunti za akiba.

Kitendo cha kukata fedha za wateja kila mwezi ni kuwakatisha tama hasa wenye kipato cha chini kwani wengi tunaamini benki ni mahali salama pa kutunzia fedha ingawa nazo zinafanya biashara.

Kutokana na akiba ndogo za masikini wengi, benki zitafute namna ya kuongeza mapato badala ya kuwaumiza wananchi hao. Hili likifanyika, ni dhahiri watumiaji wataongezeka kutoka asilimia 17 waliopo sasa kwenda juu zaidi.

Licha ya kuwapo kwa benki zaidi ya 50 nchini, watumiaji bado ni wachache. Wadau wanasema miongoni mwa sababu za wengi kuzikwepa huduma za fedha ni gharama zilizopo.

Bila shaka wateja wanaopohifadhi fedha zao, benki zinafanya biashara kwa kutumia akiba hizo hivyo si busara kuzikata tena kila mwezi badala yake ziangalie namna ya kuwahamasisha wengi kufungua akaunti kwa kutoa faida ya kila mwaka.

Haingii akilini kuona mtu aliyeenda nje ya nchi kwa miaka miwili akiacha akiba ya Sh100,000 kwenye akaunti yake, anaporudi anaambiwa fedha zimeisha.

Benki zikumbuke kwamba tabia ya kuweka makato mengi na makubwa yasiyo na tija yanachangia watu wazidharau na kupuuza huduma zake.

Makato ya benki yasiyo na kichwa wala miguu ni kichocheo cha Watanzania wengi kuendelea kujitunzia fedha zao nyumbani au kwenye magunia.

Benki ziondoe makato badala yake zitoe motisha kwa wateja wanaotunza fedha nyingi kwa kipindi kirefu.

Wananchi wengi kutotumia huduma hizi ni kupunguza ushiriki wao kwenye ujenzi wa uchumi wa kisasa unatarajiwa kuendeshwa na viwanda wakati Tanzania ikijiandaa kuwa na uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025.

Tuwasiliane kwa 0767 338897