Tuachane na kilio cha vyumba vya madarasa sasa

Muktasari:

  • Si hivyo tu, kwa mujibu wa mwalimu mkuu wa shule hiyo, Jacob Joshua, kuna zaidi ya wanafunzi 170 wanaosomea kwenye chumba kimoja,

Wanafunzi 1,154 wa Shule ya Msingi Bugire iliyopo katika Kata ya Ikoma wilayani Rorya wanategemea vyumba saba vya madarasa.

Si hivyo tu, kwa mujibu wa mwalimu mkuu wa shule hiyo, Jacob Joshua, kuna zaidi ya wanafunzi 170 wanaosomea kwenye chumba kimoja,

Mwalimu Joshua anasema madarasa 16 yanahitajika ili kukidhi idadi ya wanafunzi wote, hiyo ikiwa na maana kwamba kuna upungufu wa madarasa tisa.

“Vyumba hivi vikikamilika vitapunguza msongamano uliopo madarasani na kuturahisishia utendaji kazi wetu, maana kwa kipindi hiki tunahangaika sana kutekeleza majukumu yetu,” anasema Joshua.

Tatizo lililopo katika shule ya Bugire limekuwa likiripotiwa katika maeneo mbalimbali nchini ambako simulizi za wanafunzi zaidi ya 60 kutumia darasa moja badala ya 45 wanaotakiwa, zimekuwa zikisikika.

Si hivyo tu, lakini pia simulizi za wanafunzi wa madarasa tofauti kutumia chumba kimoja kwa kubadilishana ni za kawaida na hii ni kutokana na uhaba au uchache wa vyumba unaokuwa katika shule husika.

Simulizi juu ya vyumba vya madarasa haziishii hapo, kuna maeneo fulani yamewahi kuripotiwa kuwa wanafunzi wa awali au wa shule ya msingi wanasomea nje, chini ya miti au ndani ya majengo chakavu. Kwa ujumla hizi ni changamoto zisizohitajika kusikika katika ulimwengu wa sasa.

Tunasema changamoto hizi, kama Taifa tunapaswa kuondokana nazo kutokana na mwamko uliopo nchini wa uandikishaji wanafunzi wa awali na msingi, hivyo tunahitaji kujipanga vyema kwa ajili ya kuwa na vyumba vingi zaidi vya madarasa katika shule zetu.

Ni vyema tukaondokana na upungufu wa madarasa tukizingatia kwamba karibu kila mwaka kutakuwa na ongezeko la wanafunzi litakalosukumwa na elimu ya bila malipo inayotolewa na Serikali, ambayo kwa kiasi kikubwa mpaka sasa imehamasisha uandikishaji wa wanafunzi shuleni.

Katika kukabiliana na tatizo hilo, Serikali isiishie katika shule za msingi tu, lakini pia iliangalie suala hili katika sekondari zetu ambako vyumba vingi zaidi vya madarasa vinahitajika katika miaka michache ijayo kutokana na msukumo uleule wa Serikali kusamehe ada kwa wanafunzi wanaofaulu kujiunga na elimu hiyo.

Mfano rahisi wa mahitaji haya ni ule wa mwishoni mwa wiki iliyopita Serikali ilipotangaza wanafunzi 58,927 waliochaguliwa kujiunga na kidato cha tano.

Wakati akitangaza matokeo hayo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Tamisemi), Selemani Jafo alisema wanafunzi 21,808 kati ya 92,630 waliofaulu mtihani wa kidato cha nne na kuwa na sifa za kujiunga na kidato cha tano, vyuo vya ufundi na vya elimu wamekosa nafasi.

Kukosa kwao nafasi kunamaanisha kwamba, kama Taifa hatuna vyumba vya madarasa au miundombinu mingine ili kuwawezesha kuendelea na masomo yao.

Ingawa Serikali imekuja na mpango wa ujenzi wa haraka wa vyumba vya madarasa kwa ajili ya kuhakikisha wanafunzi hao wanaendelea na masomo, lakini hautakuwa tiba ya kudumu kwa miaka mingi ijayo, maana unalenga kutatua tatizo lililopo sasa.

Tunaishauri Serikali ianze kuja na mpango wa muda mrefu utakaojibu kilio cha miaka mingi ijayo cha namna ya kukabiliana na idadi kubwa ya wanafunzi wanaoandikishwa kila mwaka pamoja na idadi kubwa ya wahitimu hususan kwa ngazi ya awali, msingi na sekondari.

Suala la kuwaagiza wakuu wa mikoa, wilaya, wakurugenzi wa miji, manispaa, halmashauri na majiji kuhakikisha kuwa azma ya Serikali ya kila tarafa kuwa na shule ya kidato cha tano au kata kuwa na sekondari ni zuri lakini haliwezi kuwa ufumbuzi wa kudumu wa tatizo la uhaba wa shule au vyumba vya madarasa.

Ni vyema tukawa na mkakati wa kujenga shule nyingi zaidi na zilizopo ziongezwe miundombinu maridhawa ili kukidhi matakwa ya sasa na baadaye.