Uhaba kadi za leseni unawatesa madereva

Muktasari:

  • Leseni hizo hutolewa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ikishirikiana na taasisi nyingine kama Jeshi la Polisi.

Imekuwa kawaida kwa wanaotaka kubadili leseni baada ya walizonazo kwisha muda wake kutakiwa kusubiri kati ya miezi miwili hadi mitatu.

Leseni hizo hutolewa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ikishirikiana na taasisi nyingine kama Jeshi la Polisi.

Watu wengi walizowea kubadili leseni ndani ya wiki moja moja, lakini sasa ni tofauti na madereva wengi wanalazimika kutembea na karatasi za TRA zinazoonyesha leseni zao bado hazijabadilishwa.

Maelezo wanayopewa wengi wa madereva wanaosubiri kuhusu kuendelea kusubiri leseni hizo ni kukosekana kwa malighafi za kuzitengeneza.

Mpaka sasa changamoto hii imedumu kwa takriban mwaka mmoja. Kwa muda huo, wahusika wanapaswa kujitathmini, vinginevyo kuna ukweli ambao hauelezwi bayana kwa watu kuhusu kiini cha tatizo hilo.

Kama kungekuwa na mabadiliko ya utendaji yanayosababisha mchakato wa kubadili leseni kuchukua muda mrefu zaidi ingekuwa ni vyema yakatangazwa kwa umma.

Ni wazi kuwa kwa wamiliki wa vyombo vya moto na wale na madereva leseni ni miongoni mwa nyenzo zao muhimu katika utoaji wa huduma.

Nadhani mamlaka zinazohusika zinaangalia Sh40,000 (fedha mtu anazotozwa kama gharama ya huduma), lakini jambo hili linawagharimu madereva zaidi ya fedha hizo ukizingatia na muda wanaoutumia kufuatilia.

Kimsingi gharama anayotumia kmtu ufuatilia leseni sasa ni kubwa kuliko kwani leseni hizo hutolewa katika ofisi za TRA za mkoa husika au kituo kilichoanzishwa kwa ajili hiyo.

Hivyo watu wengi hutumia nauli kwenda kufuatilia na muda wanaotumia ungetosha kutumika katika shughuli nyingine za uzalishaji mali.

Jambo hili linaweza lisiwaguse sana wanaokaa mjini au karibu na ofisi za TRA, lakini huwasumbua sana walio nje ya mji hasa mikoani wanakolazimika kusafiri mpaka zaidi ya kilomita 300 kufuatilia.

Hivi karibuni niliambiwa na mtu mmoja aishiye Kabanga wilayani Ngara kuwa alipokwenda kuhuisha (ku-renew) leseni yake mjini Bukoba mwezi uliopita aliambiwa arudi baada ya wiki mbili na baada ya muda huo kupita aliambiwa arudi tena Agosti.

Kwa bahati mbaya tofauti na utaratibu ulivyo katika maeneo ya huduma kwamba suala likiwa tayari mhusika anaweza kujulishwa kwa ujumbe mfupi wa simu, kwa upande wa leseni za magari haipo hivyo. Ni lazima mtu ufuatilie ana kwa ana.

Safari ndefu kama hizo ukiachilia mbali nauli, kuna gharama za njiani na za malazi, na si rahisi kwenda kwa siku moja na kurejea katika makazi ya kudumu.

Hata kwa wakazi wa maeneo yaliyoko karibu na ofisi husika nao si rahisi kufuatilia mara kwa mara kwa kuzingatia gharama za usafiri na muda kwani licha ya uhitaji wa leseni, shughuli nyingine za kujiingizia kipato lazima ziendelee.

Mfano dereva wa daladala au gari ambaye malipo yake hutegemea kipato kilichoingia kwa siku, mazingira yanapomlazimu kupoteza siku mara kadhaa kufuatilia jambo moja ni kumrudisha nyuma kiuchumi.

Naamini jambo la kadi haliwezi kuwa kisiki cha mpingo kwa taasisi kubwa kama TRA ambayo imekuwa ikitoa huduma hiyo bila changamoto kwa kipindi kirefu. Na hata kama kuna tatizo wana uwezo wa kulitatua.

Kama kuna juhudi zinafanywa na TRA kutatua tatizo hilo ni vyema likatatuliwa haraka maana limekuwa kero kwa wengi na pia linawadhoofisha watu kiuchumi.

Huduma inayoweza kutolewa ndani ya wiki moja ikitolewa ndani ya miezi mitatu ni aibu na kama tatizo ni kadi hizo kama inavyodaiwa, basi ziagizwe au zitengenezwe za kutosha kwani sio kwamba zikihifadhiwa zitachacha. Muhimu ni kuzingatia udhibiti thabiti.

0756-939401