Wastaafu wageukie ujasiriamali

Muktasari:

Maandalizi na mipango mizuri inahitajika kufanikisha jambo lolote baada ya kuzikabili changamoto zitakazojitokeza.

Ujasiriamali hauna umri. Vijana na wazee wote wanaweza kuchangamkia fursa zilizopo sokoni.

Maandalizi na mipango mizuri inahitajika kufanikisha jambo lolote baada ya kuzikabili changamoto zitakazojitokeza.

Kampuni na wajasiriamali wanafanikiwa na kufika mbali kutokana na mipango na kuwekeza kwenye utekelezaji na ufuatiliaji wa malengo waliyojiwekea.

Wastaafu wengi nchini huishi maisha ya dhiki baada ya kumaliza mafao waliyolipwa baada ya utumishi wa muda mrefu. Ni ukweli usiopingika kuwa wazee hawa huingia kwenye matumizi mabovu ya fedha pindi wanapopata malipo yao ya kustaafu kwa mkupuo.

Fedha hizo huingizwa kwenye matumizi mabovu, uwekezaji usiokuwa na uzoefu kuleta tija iliyokusudiwa kabla ya kuishiwa na kumfanya mzee kuanza kuishi bila matumaini yoyote ya kujinasua. Hapa watoto huanza kutegemewa, kama wapo. Vinginevyo ndugu huhusika kusaidia kulisongesha gurudumu la maisha kwa wapendwa hawa.

Kuna ulazima mkubwa wa kuwaandaa wazee hawa kisaikolojia kuwekeza kwa manufaa pindi watakapostaafu kujiingizia kipato cha kutosha kumudu gharama za maisha. Hili lina umuhimu mkubwa kwa sababu bado viwango vinavyotolewa havikidhi mahitaji.

Ni wakati muafaka kwa mifuko ya hifadhi ya jamii kuwa na madawati au kitengo cha ubunifu kitakachotoa mafunzo ya ujasiriamali ya kuwaandaa wazee hawa miaka michache kabla ya kustaafu kwao.

Kitengo hiki kinatakiwa kuundwa na wataalamu wa fedha na mipango, ujasiriamali na ubunifu, waangalie miaka ambayo mzee amebakiza kustaafu ili kuanza kuwa naye karibu na kumuweka kwenye njia sahihi ya maisha baada ya kazi hasa kwenye kuandaa miradi midogo ya uzalishaji.

Kinachohitajika ni kuwajengea uwezo wazee waliolitumikia Taifa enzi za ujana wao kufahamu kitu wanachoweza kufanya baada ya kumaliza utumishi kutoka sekta zote za uwekezaji na uchumi kuanzia kilimo, usafirishaji, biashara, masoko, mawasiliano na kokote ambako mhusika ana ufahamu nako.

Baada ya kufahamu na kushauriana vizuri na wazee hawa waandaliwe mafunzo ya vitendo ambayo yataendana na mazingira halisi ya uwekezaji. Lakini kuandaliwe mpango biashara ulioshiba ambao utakuwa muongozo wa uwekezaji wao.

Kazi hii inatakiwa ifanywe kwa ustadi kwa kutumia wataalamu hawa kutoka kwenye ofisi hasa za hifadhi za jamii ambazo zitaendelea kufanya kazi na wazee hawa mpaka biashara na shughuli zao zitakapokuwa zimetengamaa na kusimama vizuri.

Kiasi kidogo cha fedha kitumike kuwekeza na kutoa nafasi ya kutumia kinachobaki kwa matumizi mengine yakiwamo ya familia. Kuanzisha vituo hivi na madawati haya si gharama kubwa ukilinganisha na manufaa ambayo wazee na taifa watapata kwa kuweka mazingira mazuri ya kuendelea kunufaika na uwekezaji mdogo.

Tukifanya hivi hakika tutakuwa tumewapunguzia gharama za maisha na changamoto ya fedha baada ya kustaafu lakini Serikali itakuwa imepunguza idadi ya wazee ambao mara nyingi wanashindwa kutumia vizuri fedha hizi na kuanza kuilalamikia kuwalea upya.

Ni rahisi kwa mashirika makubwa kutoa mafunzo yenye tija na kuendelea kuwajengea wazee uwezo wa uwekezaji kwenye biashara na ujasiriamali.

Wazee wanatakiwa kuonyesha ushirikiano kwa hifadhi hizi endapo kutaanzishwa programu za namna hii ambazo kwa hakika zitakuwa na mchango wa kustawisha uchumi wa wao na Taifa kwa ujumla.

Wale wanaotarajia kustaafu wanaweza kuanza kufanya bishara wazipendazo.