Thursday, July 12, 2018

Waziri Lugola fanyia kazi mawazo ya mtangulizi wako

 

Mapema wiki hii aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk Mwigulu Nchemba alikabidhi rasmi ofisi akiacha ushauri wa mambo matatu kwa mrithi wake, Kangi Lugola.

Dk Nchemba ambaye aliachwa katika mabadiliko madogo ya Baraza la Mawaziri, Julai Mosi, alitaja moja ya mambo hayo kuwa ni pamoja na utaratibu wa askari wa Jeshi la Polisi kufanya kazi kwa mikataba ya miaka 12, akishauri kwamba uondolewe.

Dk Nchemba alimshauri Lugola kuondoa utaratibu huo wa polisi kufanya kazi kwa mkataba wa miaka 12, jambo alilosema linalalamikiwa na askari wengi kwa kuwa linaathiri mafao yao.

Kwa mujibu wa Dk Nchemba, kwa utaratibu huo, askari akistaafu anahesabika amefanya kazi ya kudumu baada ya kumaliza miaka hiyo tofauti na waajiriwa wengine wa Serikali kama walimu.

Kimsingi, alichoshauri Dk Nchemba kina mantiki kwa kuwa kitasaidia askari wa jeshi hilo kufanya kazi bila kuwa na wasiwasi wa kupoteza ajira wangali vijana.

Mathalan, yamekuwapo malalamiko mengi ya chini kwa chini kutoka kwa askari hao kustaafu wakiwa bado na nguvu na kutokuwa na cha kufanya.

Kwa ujumla pamoja na mfumo huo awali kuonekana unafaa, umekuwa na changamoto kadhaa ikiwa ni pamoja na kuzalisha watu wengi wasio na ajira jambo linaloweza kuzorotesha harakati za kupambana na umaskini nchini.

Changamoto nyingine ni kupoteza rasilimali kubwa ambayo Serikali ilitumia katika kuwaandaa askari hao, lakini baada ya muda mfupi wamekuwa wakistaafu bila kufika umri wa uzeeni.

Wengi wetu ni mashahidi wa jinsi Serikali inavyowekeza katika mafunzo ya polisi kwa kutenga bajeti kubwa ya kuwaelimisha askari hawa wawapo vyuoni, lakini baada ya muda mfupi katika utumishi askari hao wanastaafu wakiwa bado na nguvu na ari ya kulitumikia Taifa.

Kwa kuondoka kazini wakiwa bado vijana huchangia kuongeza idadi ya watu wasio na ajira mitaani, jambo linaloweza kuchangia vitendo vya uharifu.

Tukumbuke kwamba askari wamepewa mafunzo ya kukabiliana na vitendo vya uhalifu ikiwamo kutumia silaha za moto, hivyo kuishi bila ajira katika umri mdogo ambao miongoni mwao hutoka nao kazini ni tatizo.

Tunasema hivyo kwa sababu kukaa bila kazi wapo baadhi yao ambao wanaweza kupata vishawishi na kujiingiza katika vitendo vya uharifu ikiwamo unyang’anyi na uporaji kwa kuwa tu wamekosa cha kufanya baada ya kustaafu wangali wadogo.

Kwa hili tunaiomba Serikali ilione kama changamoto na kulifanyia kazi haraka ili askari wetu nao wawe kama kada nyingine za utumishi serikalini katika suala la umri wa kustaafu.

Ni maoni yetu kuwa umri sahihi wa askari kustaafu kwa hiari ni bora uwe wanapofikia miaka 55 (kwa hiari) au 60 (kwa lazima) kama ilivyo kwa watumishi wengine wa umma, kwani ndiyo muda muafaka ambao mfanyakazi anakuwa ameshajiandaa kukabiliana na changamoto za uzeeni.

Tunaamini askari wetu wamefundishwa utii na nidhamu, ndiyo maana jambo hili limebaki kuwa siri miongoni mwao, lakini ukweli ni kwamba linawaumiza mioyoni mwao na hivyo kubaki na vinyongo ilhali wako kazini ni jambo lisilo la afya kwa mustakabali wa nchi yetu.

Ushauri huu wa Dk Nchemba ukizingatiwa utaongeza ufanisi na kuwa na jeshi imara lenye nidhamu litakalosimamia ipasavyo majukumu liliyokabidhiwa kisheria.

-->