Madhara ya vumbi kwa afya, namna ya kujikinga

Muktasari:

Kutokana na hali ya hewa ilivyo nchini kwa sasa, hewa tunayotumia imechafuliwa na vumbi pamoja na taka nyingine hivyo tunapaswa kuchukua tahadhari.

Katika siku za karibuni, baadhi ya maeneo nchini yamekumbwa na ukame wa muda mrefu, huku kukiwa na upepo mkali unaosababisha udongo na taka mbalimbali kupeperuka. Hali hii inasababisha hewa wanayovuta watu kuwa na vumbi.

Uwepo wa viwanda, vyombo vya usafiri, upepo na shughuli nyingine za kiuchumi imekuwa ni chanzo cha uchafuzi wa hewa tunayoihitaji kwa ajili ya kuendeleza uhai.

Vumbi ni moja ya vitu ambavyo uwapo wake katika hewa huchukuliwa kama ni uchafuzi wa hewa. Vumbi ni chembechembe ndogo zinazoweza kupeperuka na kuenea kirahisi katika hewa na hapo baadaye likawapata wanadamu wanaofanya kazi au wanaoshi jirani na chanzo cha vumbi.

Vumbi linaweza kutokana na vitu visivyo hai ikiwamo mawe, mchanga, madini, moshi au taka zinazotokana na masalia ya vitu mbalimbali vilivyosagika.

Vilevile, vumbi linaweza kusababishwa na kuungua kwa vitu au milipuko mbalimbali, kemikali za madawa ya kuulia wadudu na magamba ya mimea yenye kemikali.

Magonjwa ambayo mara kwa mara yamekuwa yakihusishwa na mavumbi ni pamoja na saratani ya mapafu, vikohozi sugu, kuharibika kwa tishu za mapafu, pumu, mzio, kifua kubana na mafua.

Haya ni matatizo yanayotokana na mfumo wa hewa na ukiyachunguza unaweza kubaini kwa sasa yanawakumba watu wengi kutokana na hewa kuchafuka.

Ukiacha matatizo ya mfumo wa hewa yapo matatizo mengine yanayoweza kujitokeza ikiwamo saratani mbalimbali na sumu inayosababisha uharibifu wa figo na ini na magonjwa ya ngozi.

 

Mfumo wa hewa

Mfumo wa hewa umeundwa kwa namna ambayo huweza kudaka chembe za vumbi zilizovutwa pamoja na hewa.

Hewa inapoingia puani kuna vinyweleo na tando laini ya tishu zenye ute ambazo huweza kudaka vumbi na taka zingine zisiweze kufika ndani ya mapafu.

Taka hizo zinaweza kutoka nje ya mwili kwa kupiga chafya, kukohoa au kutoka pamoja na ute uliopo njia ya hewa puani kwa kupengwa.

Inapotokea vumbi likashindwa kudakwa eneo la puani na hufanikiwa kwenda mpaka ndani katika mapafu ambako nako ndani yake kuna mfumo ambao unaweza kuchuja taka hizo na kuzitoa.

Sehemu ya ndani kuna mapafu mawili, ndani yake na kuna mirija midogo kwa mikubwa inayopitisha hewa. Ndani ya mirija hii huwapo na seli zilizotanda katika kuta za mirija hiyo zenye vinyweleo na hutoa ute mzito.

Vumbi linapoingia katika mapafu hudakwa na ute na vinyweleo vilivyomo katika mirija ya hewa na huweza kusukumwa kurudi nje mpaka kooni pale mtu anapokohoa au kupiga chafya.

Zile chembe za vumbi ambazo zimeshindwa kutolewa huweza kufika sehemu ndani ya chini ya mapafu ambako kuna vifuko vijulikanavyo kama alveol ambavyo ni muhimu kwa ajili ya kupokea hewa ya oksijeni na kuingiza katika mzunguko wa damu na kutoa hewa ya chafu ya kabondayoksaidi.

Vifuko hivyo havina ulinzi wakutoa chembe za vumbi kama ilivyo kwa wa mirija ya hewa bali ina seli maalumu zinazotoa ulinzi. Hivyo uwapo wa kitu kigeni husababisha askari mwili kuamka na kukikabili.

Seli hizo hujulikana kama macrophage huweza kuvamia chembe za vumbi na kuzimeza na huweza kubingirika nazo mpaka katika eneo lenye vinyweleo ambako hutolewa nje ya mapafu kirahisi.

Pale seli hizi zinaposhindwa kufanya kazi ya kuzitoa chembe hizo kutokana na kurundikana kwa wingi huweza kupasuka na kufa. Zinapokufa hutoa vitu ambavyo huweza kusababisha uharibifu wa tishu za mapafu na kuacha makovu mabaya.

Seli hizi husababisha kutokea kwa kovu baya katika tishu za mapafu, hali hii hujulikana kitabibu kama Fibrosis. Kovu baya katika tishu za mapafu huweza kushusha utendaji kazi wa mapafu.

Pamoja na uwezo huu mkubwa wa mapafu na mfumo mzima wa hewa pale inaopotokea mtu amekuwa akivuta hewa yenye vumbi kwa kipindi kirefu mfumo huo unaweza kuzidiwa na kushindwa kuziondoa chembe za vumbi hivyo kuendelea kurundikana.

Kushindwa huku kuziondoa taka vumbi zilizoingia katika mapafu ndipo kunapojitokeza matatizo mbalimbali ya kiafya ambayo yanaweza kusababisha kifo.

 

Madhara yanavyojitokeza

Kiujumla uwapo wa vumbi katika mapafu ndipo kunapozaliwa maradhi katika mapafu miongoni ukiwamo nimonia au homa ya mapafu.

Tatizo hilo la kiafya la mapafu ndiyo linalowapata wafanyakazi au watu wanaoishi katika maeneo yenye vumbi linalotokana na uchimbaji madini/mchanga/kokoto mawe na makaa ya mawe.

Madhara ya kiafya yanayoweza kujitokeza yanayoweza kuwa ya muda mfupi yanayoisha au ya kudumu ya muda mrefu.

Madhara ya muda mfupi ni pamoja na kupata shambulizi katika tishu za pua hivyo kupata dalili za mafua, mwasho puani na koo, kukohoa, kupata chafya na kupumua kwa shida.

Matatizo mengine ni kupata mzio na vilevile baadaye pumu inaweza kujitokeza.

Vumbi linalovutwa linaweza likawa limechanganyika pamoja na sumu mbalimbali ikiwamo madini ya risasi na kuleta madhara ya kiafya maeneo mengine mwilini ikiwamo figo na ini kushindwa kufanya kazi.

Vilevile mwili kuguswa na vumbi kwa kiasi kikubwa inaweza kuwa chanzo cha kupata matatizo ya ngozi ikiwamo mwasho mkali, kubabuka ngozi, vilevile kuwa makaribisho wa vimelea wanaoshambulia ngozi.

Madhara ya muda mrefu yanayoweza kusababisha ulemavu wa kudumu wa mapafu ni pamoja na uharibifu wa tishu za mapafu na kutengenezwa kwa kovu baya.

Vumbi la taka zisizotokana na viumbe hai linalosababisha kutokea kwa uharibifu wa aina hii ni pamoja na vumbi la mchanga, vumbi la makaa ya mawe na vumbi la Asbestos.

Kwa upande wa vumbi litokanalo na mimea na wanyama zinazoleta uharibifu wa mapafu ni pamoja chembe za vumbi la nafaka, vumbi la manyoya ya ndege na wanyama na vumbi la sukari guru.

 

Namna ya kuzuia

Inashauriwa ukiwa sehemu yenye vumbi mfano viwanda, shughuli za uchimbaji madini, upepo wenye vumbi au ukiwa barabarani vumbi linapotimuliwa na vyombo vya usafiri, mtu anapaswa kufunika pua kwa kitambaa ili kichuje hewa inayovutwa.

Kwa wafanyakazi wali katika mazingira ya vumbi kutimka wakati wote kwa kawaida hupatiwa vifaa maalumu vilivyotengenezwa kwa ajili ya kujikinga.

Pia, kuna mashine zenye mfumo wa kunasa vumbi na kulimwagia unyevu ili lisipeperuke. Matumizi ya vifaa vya kuvaa na kukinga vumbi kwa wafanyakazi liwe chaguo la mwisho baada ya mbinu nyingine za kisasa kuonekana kushindwa kudhibiti vumbi.

Vifaa maalumu vya kukinga mwili usipate vumbi ni pamoja buti, nguo maalum, kofia na vifaa vya kukinga pua.

Kusafirisha na kuhifadhi vitu vinavyosababisha vumbi kwa uangalifu ikiwezekana viweke katika mifuko au vyombo maalum vinavyozuia vumbi kutimka.

Maeneo ambayo yanayokumbwa na hali ya vumbi ni vizuri kutumia mashine zinazofagia vumbi kwa kunyonya kwa shinikizo kubwa.

Makazi ya kuishi yawe mbali na viwanda au shughuli za machimbo zinazosababisha kutokea kwa vumbi.

Pamoja na kuwa na kinga dhidi ya vumbi, ni vizuri kwa wale wanaofanya kazi au kuishi katika mazingira hayo yenye vumbi kujenga utamaduni wa kufanya uchunguzi wa kiafya mara kwa mara.