DC Ileje apiga marufuku vyandarua kujengea bustani

Mkuu wa Wilaya ya Ileje Farida Mgomi akiwa katikati ya wananchi (amevaa nguo rangi ya maziwa) akigawa vyandarua kwa wananchi waliohudhuria maadhimisho Siku ya Malaria jana.

Muktasari:

Mwaka 2024 Ileje inatarajia kugawa vyandarua vyenye dawa 32,500 ili kutokomeza Malaria


Ileje. Mkuu wa Wilaya ya Ileje, mkoani Songwe, Farida Mgomi amewaagiza viongozi wa vijiji  kusimamia wananchi kutotumia vyandarua kujengea bustani za mbogamboga.

Mgomi ametoa agizo hilo katika maadhimisho ya Siku ya Malaria Duniani ambayo kwa Wilaya ya Ileje yalifanyika jana Aprili 25, 2024 katika Zahanati ya Isongole, Kijiji cha Isongole, Kata ya Isongole.

Katika maadhimisho hayo, wamegawa vyandarua 480 kwa wajawazito, watoto chini ya  miaka mitano na watu wanaoishi na virusi vya Ukimwi (VVU).

Hata hivyo, imekuwa kawaida kwa baadhi ya watu kutumia vyandarua wanavyogawiwa kama uzio wa bustani za mbogamboga.

Mgomi amesema wakati Serikali inaendelea na jitihada za kupambana na Malaria kwa kugawa vyandarua vyenye dawa baadhi ya wananchi hugeuza matumizi yake na kukwamisha jitihada hizo.

Amesema kwa mwaka 2024 Ileje inatarajia kugawa vyandarua vyenye dawa 32,500 ili kutokomeza Malaria.

"Kuanzia sasa viongozi wa Serikali za vijiji simamieni agizo hilo na sasa ni marufuku kutumia chandarua kilichotengenezwa maalumu kwa ajili ya kuzuia Malaria chenye dawa kutengenezea bustani," amesisitiza Mgomi.

Ofisa Malaria wilayani hapa, Said Mnkaya amesema Ileja ina vituo 45 ambavyo hufanya vipimo vya damu kutambua watu wenye maambukizi ya Malaria.

Amesema kwa mwaka 2024, wajawazito 745 waliohudhuria mara ya kwanza walipatiwa vyandarua na wananchi 237 wanaoishi na VVU.

Mariamu Panja, mkazi wa Kijiji cha Isongole amesema ili kudhibiti matumizi holela ya vyandarua, zitungwe sheria ndogo zitakazowashughulikia wataobadilisha matumizi kama vile kuvulia samaki, kuweka kwenye magoli kama nyavu pamoja na kujengea bustani.

Agnesi Silwimba, mkazi wa Kijiiji cha Isongole alisema watakaobainika wanatumia vyandarua hivyo kwenye bustani za mbogamboga wachukuliwe hatua za kisheria.