Imani potofu bado mwiba utokomezaji malaria

Tabora, Kagera, Shinyanga. “Nimeanza kutumia kinyesi kikavu cha ng’ombe miaka mingi, nikichoma nafunga mlango moshi unajaa ndani kama kuna mbu wanakufa au wanakimbia kupitia uwazi mdogo uliopo. Vyandarua tutakuwa navyo vingapi, nyumba ina watu zaidi ya wanane?”

Ni kauli ya Kgaka Boyo, mkazi wa Kijiji cha Igagala wilayani Kaliua Mkoa wa Tabora ambayo inawiana na nyingine zenye mwelekeo huo zilizotolewa na watu kadhaa waliozungumza na Mwananchi kuhusu hatua wanazochukua kujikinga na mbu waenezao malaria.

Katika uchunguzi uliofanywa na gazeti hili kwenye mikoa ya Tabora, Kagera na Shinyanga inayoongoza kwa ugonjwa huo nchini, imebainika kwamba uelewa mdogo unachangia kukwamisha matumizi sahihi ya vyandarua.

Tabora inaongoza kwa maambukizi ya malaria nchini, ukiwa na asilimia 23.4 kwa mujibu wa Ripoti ya Utafiti wa Afya ya Uzazi na Mtoto pamoja na Viashiria vya Malaria nchini ya mwaka 2022 (TDHS- MIS). Mkoa unaofuata ni Mtwara (asilimia 19.7), Kagera (asimilia 17.5) na Shinyanga (asilimia 15.6).


Majani ya mkaratusi

John Mgongo, mkazi wa Kata ya Igagala, Wilaya ya Kaliua mkoani Tabora, ni miongoni mwa wanaotumia majani ya mkaratusi kufukuza mbu. Huyachoma ndani kisha hufunga mlango ili kuua wadudu hao.

“Hii dawa nzuri sana mama, hata wewe ukiijaribu utakubaliana na mimi. Inaushinda hata mwarobaini ambao wenzangu wengi huutumia kuua mbu,” anasema huku akiwasha majani hayo.

Anasema anapohisi mwili umechemka  hunywa mwarobaini mchana na jioni kwa siku mbili na huwa sawa.

“Ninyi huko mjini ndiyo mnatumia vitu hivyo (vyandarua) kwa sababu hata mikaratusi mliyonayo si kama ya kwetu, ya kwenu ni ya kisasa haina dawa,” anasema.

Anasema vyandarua hutolewa kwenye vituo vya afya, lakini ana miaka mingi hajaenda kwa kuwa hajaugua.

“Niliwahi kuzidiwa miaka kama minane au 10 iliyopita nikapelekwa kituo cha afya na watoto wa kaka yangu. Nililazwa siku mbili wakaniongezea maji.

“Kuanzia hapo nimekuwa makini kuchoma haya majani kujikinga na homa, hasa wakati wa masika ambao mbu wanakuwa wengi,” anasema.


Kupumua, kunguni

Mkazi wa Kijiji cha Usinge wilayani Kaliua, Kimweri Kayowa anaeleza alipokwenda kituo cha afya kwa  matibabu hakuwa na malaria, lakini aliambiwa kila aliyefikisha miaka 60 anapewa chandarua, hivyo akapewa.

“Nina wake watatu, nikilala nyumba nyingine nitakifunga, nikienda kwa mwingine sitakuwa nacho. Hata hivyo, nilipojaribu kukitumia nilipata shida kupumua, pia kinaleta sana kunguni, ukilala unawaona wanatembea juu ya chandarua na wanang’ata tofauti na nisipokitumia,” anasema.

Anaeleza huwa haugui malaria mara kwa mara ila familia yake, wakiwamo wajukuu husumbuliwa na ugonjwa huo.

“Kuna kajukuu kangu kalifariki mwaka juzi, sikumbuki kalikuwa na miaka mingapi ila kakubwa kakubwa kakutuma kabisa, aliumwa kama siku tatu homa haishuki.

“Alipopelekwa hospitali akachomwa sindano ndiyo kama walimmalizia, alifariki wakasema ni malaria, ila mimi sijasumbuliwa na ugonjwa huo mpaka nimefikia umri huu,” anasema Kayowa.

Alipoulizwa baada ya kifo cha mjukuu haoni umuhimu wa kutumia chandarua, alijibu, “haya mambo nahisi yana wenyewe. Kuna wakati tunahamia porini kutafuta malisho ya mifugo, huko nako nitafunga chandarua? Kwa umri huu sioni haja ya kuhangaika tena, mbu wakizidi tunatumia njia zetu za asili kuwafukuza na inasaidia.”

Mkazi mwingine wa kijiji hicho, Kasanga Kalangu anasema, “Tena sikufichi kijana eti umwambie atumie chandarua asipotumia atapata malaria na atakufa, hakusikilizi kabisa, tena baadhi huku vijijini wanaamini inapunguza nguvu za kiume.”


Kauli za wataalamu

Akizungumzia hali ya Malaria, Ofisa Afya na Mazingira wa Wilaya ya Kaliua, Brycesm Kalatwa anasema ugonjwa huo bado unaathiri jamii na katika magonjwa 10 yanayoongoza, Tabora unashika nafasi ya pili ukitanguliwa na magonjwa ya njia ya hewa.

Anasema kutokana na hatua walizochukua wamefikia hapo, lakini kuanzia mwaka 2013 ulikuwa unaongoza kwa takwimu za wagonjwa waliofika hospitalini na kwenye vituo vya afya na kupimwa.

“Changamoto ipo katika kata zote 28 kutokana na taarifa tunazozipata kutoka vituo vya afya, tunaendelea kuweka mikakati ya kupambana na hali hiyo, ikiwamo kutoa elimu kwa jamii,” anasema Kalatwa.

Anasema elimu inatolewa zaidi katika usafi wa mazingira ili kuharibu mazalia ya mbu kwa kushirikiana na viongozi wa kata.

Kuhusu kunguni kujitokeza kwenye vyandarua, anasema dawa ya kuua mbu iliyowekwa kwenye chandarua ndiyo huwatoa wadudu hao.

“Faida ya kuwapo kwa vyandarua vyenye dawa ni pamoja na kuibua wadudu wengine ambao unaweza kuwadhibiti kwa sababu umewaona,” anasema.

Akifafanua zaidi kuhusu hilo, mkuu wa kitengo cha kudhibiti wadudu wadhurifu kutoka Wizara ya Afya, Charles Dismas anasema kunguni huonekana kwa kuwa vyandarua vimewekwa sehemu walipo wadudu hao.

“Dawa iliyowekwa kwenye chandarua huwawasha, lakini hawafi kwa sababu wamejenga usugu. Ndiyo maana maeneo ambayo tulikuwa tunapulizia dawa ya ukoko kwenye kuta ndani ya nyumba tofauti na inayowekwa kwenye vyandarua, watu walikuwa wanafurahi kwa sababu ilikuwa ikiua kunguni.

“Hivi vyandarua vina dawa, hivyo kama kitanda kina kunguni hawezi kukaa anatoka nje kujiokoa, hapo ndipo hudhani kama wameletwa na vyandarua,” anasema Judestina Buyekera, muuguzi katika kituo cha afya Byekerwa mkoani Kagera.

Akilizungumzia hilo, mhudumu wa afya ngazi ya jamii mkoani Shinyanga, Azmina Nhaya anasema wengi wana imani potofu kuwa vyandarua vina kunguni.


Godoro la nyasi

Annastella Cosmo, mhudumu wa afya ngazi ya jamii Ngara mkoani Kagera anasema, “natamani elimu ifike mbali, kwani tunakutana na mengi huku kwenye jamii, mfano kuna kaya katika Kijiji cha Keza nilikuta familia nyingi za eneo hilo zinatumia vyandarua kama kifaa cha kutengenezea godoro.”

Anasema baadhi huunganisha vyandarua viwili, wakikosa hutumia kimoja ambacho huweka majani na kushona, hivyo kuwa godoro.

“Kaya nyingi nilikuta watoto wanalala chini, hivyo hawafunikwi na chandarua, wazazi wanaolala kitandani ndiyo hujikinga na mbu,” anasema.


Tiba asili

Anasema wilayani Ngara wananchi hutumia tiba asili kwa ajili ya Malaria. Dawa hiyo hutengenezwa kwa kutumia mchanganyiko wa majani maarufu mushana.

Akizungumza huku akianika dawa hiyo, Juliana Kashangaki, mkazi wa kata ya Keza, wilayani Ngara, akifafanua ni kwa nini wanaamini dawa hiyo inatibu malaria, anasema ameitumia kwa miaka mingi na hata anapoitumia kama mwili umechemka kwa homa hupata nafuu.

Muuguzi katika kituo cha afya Byekerwa aliyefanya kazi katika kitengo cha mama na mtoto kwa zaidi ya miaka 10, Judestina Buyekera anasema hilo hutokana na mazoea.

“Wengine huitumia kama dawa ya UTI kwa sababu wakiinywa hupata haja ndogo mara kwa mara, hivyo huamini inasafisha mkojo mchafu, lakini mara kadhaa tunapata wagonjwa wakiwa wameshambuliwa sana na UTI au malaria, ukiwauliza kwa nini hawakuchukua hatua mapema ya kuja hospitali hata baada ya kuona dalili wanasema walikuwa wanakunywa mushana. Hivyo, hata baada ya kuitumia huendelea kuumwa,” anasema.

Anasema elimu imekuwa msaada kwa wananchi ambao baadhi hawakuwa wakikubali kutumia vyandarua na wajawazito hawakuwa wakimaliza matumizi ya dawa ya ASP, wakisema inawafanya walale na kuhisi kichefuchefu.

Agnes Mayunga, mkazi wa Kijiji cha Ibingo, kata ya Samuye, anasema kina mama wengine hawatumii vyandarua.

“Wakifika nyumbani wanasema vina dawa wanavifua kwanza kuipunguza. Kaya nyingine nilikuta wamekitandaza vizuri ukutani, nilipowauliza wakasema chandarua kina dawa, hivyo wanavyokitandaza dawa inazunguka ndani na kuua mbu,” anasema Agnes.

Sophia Chamba, mhudumu wa afya ngazi ya kata Masewe anasema changamoto ni elimu duni kwa kaya nyingi vijijini.

“Mfano, mtoto anaumwa wanajikita kwenye matumizi ya mitishamba. Matumizi ya vyandarua kwa jamii bado yapo nyuma, watoto wanalala bila chandarua, huku wazazi kwa maana wakuu wa kaya wao wanalala kwenye vyandarua,” anasema.

Kuhusu matumizi ya dawa ya ASP kwa wajawazito, anasema hawapendi kupima na hujifungulia vijijini wakidai chanjo husababisha watoto kuzaliwa wakiwa na ulemavu.

“Alinipa na ushahidi ndugu yake kazaa mtoto hana baadhi ya viungo kwa sababu ya kufuata chanjo za hospitali na vipimo vya kila mara, hivyo haendi na amezaa watoto sita, ila wawili walifariki kwa sababu za kishirikina na si kuumwa malaria,” anasema Sophia.

Naye Ndutiwe Mabula, mhudumu wa afya kitongoji cha Magushi, Kata ya Ibingo anasema, “niliwahi kufukuzwa kwenye kaya ya wafugaji wakinituhumu kuwapa vyandarua vinavyowaletea malaria.

“Tena niliambiwa nisifike kabisa, kwani baada ya kutumia vyandarua na kupata elimu ndiyo wameanza kuugua malaria, lakini huko nyuma walikuwa salama kabisa,” anasema Mabula.

Anasema wanaendelea kutoa elimu, lakini changamoto ni nyingi, hasa vijijini ambako vyandarua hutumika kuzungushia wigo wa kufugia kuku, kwenye bustani na kuanikia dagaa.

“Ukiwauliza kwa nini wanavitumia kwa matumizi yasiyo rasmi wanasema kimechanika au vimechanika, hapo unakosa la kusema,” anasema Mabula.

Abunery Rutakyamirwa, mvuvi katika mwalo wa Nyamkazi kata ya Miembeni manispaa ya Bukoba, anasema chandarua kilichanika ndipo akaamua kuanikia dagaa.


Imeandaliwa kwa msaada wa Bill & Melinda Gates