Utitiri wa vyuo: Nacte yabaini kuwepo kwa vyuo uchwara

Katibu Mtendaji wa NACTE, Primus Nkwera

Muktasari:

Hata hivyo, pamoja na nafasi na mchango mkubwa wa vyuo, hivyo, Baraza laTaifa la Elimu ya Ufundi (NACTE), linakiri kuwepo kwa ugumu kuvidhibiti baadhi ya vyuo.

Sio siri kuwa kila uchwao, Tanzania inapiga hatua katika kutanua wigo wa elimu hasa uanzishwaji wa vyuo vya kada ya kati vinavyotoa mafunzo kwa ngazi ya cheti na stashahada.

Hata hivyo, pamoja na nafasi na mchango mkubwa wa vyuo, hivyo, Baraza laTaifa la Elimu ya Ufundi (NACTE), linakiri kuwepo kwa ugumu kuvidhibiti baadhi ya vyuo.

Ukweli ni kuwa baadhi ya taasisi zimekuwa mstari wa mbele kujitangaza katika vyombo vya habari, kuwa zimesajiliwa na masomo yanayotolewa yanatambulika na vyombo husika, ilhali zikijua zinaudanganya umma.

Katibu Mtendaji wa Nacte,  Dk Primus Nkwera anasema ili kuhakikisha ubora wa elimu kwa vyuo vilivyo chini ya baraza, siku zote wamekuwa wakijaribu kuvibana vyuo ili vifuate taratibu zilizopo.

Anasema kuwa, mbali na kufuatilia vyuo hivyo kutokana na taarifa wanazozipata kupitia vyombo mbalimbali, wanavifuatilia pia vile ambavyo vinajitangaza kupitia vyombo vya habari.

“Tukigundua kuwa wanajitangaza kinyume na ukweli tunawashauri njia za kufuata ili wasajiliwe. Kwa kawaida inatakiwa hata kabla ya kupeleka tangazo  kwenye vyombo vya habari, walilete kwanza Nacte tuthibitishe kama wanachotangaza ni ukweli,” anasema.

Anasema kuwa, sheria inalipa baraza hilo nguvu ya kukifungia chuo chochote kinachokwenda taratibu na sheria zilizowekwa.

“Tatizo ni kuwa, kama chuo kipo Mwenge ukasema umekifungia, kesho kitahamia Kimara na wanafunzi watakwenda hukohuko, ukiwabana zaidi wanabadilisha na jina,” anasema.

Anaeleza kwamba mbali na chuo kuhamahama, wanafunzi nao wako tayari kukifuata popote kitakapohamia,  jambo  analosema ni changamoto kwa baraza.

Dk Nkwera anaeleza pia kuwa, changamoto nyingine inayowakabili katika kuvibana vyuo hivyo, ni kuwepo kwa zaidi ya taasisi moja yenye mamlaka ya kuvisajili.

“Wengine ukiwafuata wanakwambia wamesajiliwa na Veta, sasa zote hizi ni changamoto ndiyo maana tukaona badala ya kukimbilia kuvifungia tuje na njia nyingine itakayowavutia wenye vyuo kuvisajili,” anasema.

Kutokana na hali hiyo, anasema baraza lake hutumia zaidi njia ya kukishauri chuo husika,  ili kiweze kufuata taratibu za kusajili chuo.
Kwa kutumia njia hiyo,  anaeleza kuwa wamefanikiwa kuongeza  idadi ya vyuo vinavyosajiliwa kwa mwaka, kutoka  wastani wa vyuo 20 mpaka 30 kwa mwaka na kufikia  zaidi ya vyuo 100.

Anaeleza siri nyingine ya usajili wa vyuo kuongezeka kuwa ni uamuzi wa Serikali kukubali watu wenye stashahada kuweza kujiunga na vyuo vya elimu ya juu, baada ya vyeti vyao kuhakikiwa na Nacte.

“Kwa kiasi kikubwa wanafunzi wamekuwa walinzi wa kwanza wa kutaka kuhakikisha vyuo wanavyosoma vimesajiliwa, hii ni kwa sababu wanajua kama vyuo vyao havitambuliwi haitawezekana wao kuendelea na masomo ya juu,” anasema na kuongeza:

“Hata hivyo, wapo wengine ni wazembe, wanakaa mpaka wanamaliza chuo wanakuja hapa wanakuta chuo hakijasajiliwa. Hii haina maana, mtu kabla hujajiunga na chuo kitu cha kwanza lazima ujue kama kina usajili, tufanye kama ambavyo mzazi hajampeleka mtoto wake shule lazima kwanza aulize kama inafaulisha.”

Anasema kuwa wanafunzi na wazazi wakiwa watu wa kwanza kuvibana vyuo husika, tatizo la vyuo uchwara litakwisha kabisa nchini.

Kwa upande wake,  Mkurugenzi Ushauri wa Vyuo na Usajili wa Nacte, Timoth Manyaga anasema kwa kawaida baraza hilo linavipa vyuo mbalimbali mwongozo wa kuhakikisha elimu itakayotolewa inakidhi mahitaji.

Anaeleza kuwa, njia hizo zinahusisha pia namna ya kudhibiti ubora wa elimu hiyo na jinsi ya kuweza kujitathmini ili kuhakikisha vinatoa elimu itakayowasaidia walengwa.

“Kila chuo lazima kiwe na dira pamoja na dhima yake ambayo vitaeleza mipango yake, na tunavitaka vieleze ukweli kwa umma juu ya huduma zake,” anasema.

Anaongeza kusema  kuwa, Nacte pia inavibana vyuo hivyo ili viwe na mitalaa ambayo inazingatia soko la ajira.

Manyaga anasema kuwa ili kuhakikisha hilo linafutwa, Nacte hulazimika kukagua mitalaa hiyo na wakati mwingine kuvipa vyuo hivyo mitalaa  yenye viwango vinavyotakiwa.

“Tunahimiza mitalaa inayozingatia umahiri na mahitaji ya soko la ajira, kuangalia kama masomo husika yanahitajika sokoni kwenye nadharia pamoja na vitendo. Hivi ni vitu muhimu tunavyozingatia kwenye mitalaa ya vyuo vyetu,”anabainisha.