MAONI: Mikakati thabiti ya kiuchumi inahitajika kuipata Tanzania ya viwanda

Muktasari:

Licha ya uchumi wa Uingereza kuwa imara, lakini Cameron aliona hataweza kukabiliana na changamoto za kiuchumi zitakazotokana na uamuzi wa kujitoa kutoka kwenye umoja huo. Aliona pumzi zake hazitoshi kukabiliana nazo. Akampisha mwenye uwezo huo.

Baada ya Waingereza kuridhia kujitoa kwenye Umoja wa Ulaya (EU), David Cameron alijiuzuku uwaziri mkuu na kumpisha Theresa May ili kulivusha kiuchumi taifa hilo kubwa barani Ulaya.

Licha ya uchumi wa Uingereza kuwa imara, lakini Cameron aliona hataweza kukabiliana na changamoto za kiuchumi zitakazotokana na uamuzi wa kujitoa kutoka kwenye umoja huo. Aliona pumzi zake hazitoshi kukabiliana nazo. Akampisha mwenye uwezo huo.

Tanzania inakimbizana na mpango wa kujiondoa kwenye kundi la nchi maskini duniani ili iwe ya kipato cha kati ifikapo mwaka 2025. Pato la kila Mtanzania liwe zaidi ya Dola 3,000 za Marekani (zaidi ya Sh6 milioni) kutoka Sh3.52 milioni za sasa kwa mwaka.

Miaka tisa imebaki ili tufike mwisho wa muda tuliojiwekea kufanikisha lengo hilo ambalo linatutaka kufanya kazi kwa juhudi na maarifa ya kutosha. Ikiwezekana; usiku na mchana.

Katika sekta nyingi, uchumi wetu unazalisha kwa saa 12. Siyo wa saa 24. Kutokana na changamoto za usalama na mambo mengine, mabasi ya abiria hayawezi kusafiri usiku, inawezekana hili nalo ni chanzo cha umaskini unaowaandama wengi.

Tafiti mbalimbali zinathibitisha umaskini wetu na kubainisha sababu. Ripoti iliyotolewa mwezi huu na Ofisi ya Takwimu ya Taifa (NBS) inaeleza asilimia 74 ya watoto nchini wanaishi kwenye umaskini. Hiyo ni sawa na watoto nane kati ya 10 waliopo mtaani na popote nchini.

Ripoti za Benki ya Dunia (WB) zinabainisha, Mtanzania mmoja kati ya kila wanne anaishi chini ya mstari wa umaskini. Anatumia chini ya Dola moja ya Marekani ambayo ni kiasi kipatacho Sh2,000. Yaani hiyo inaitumika kwa kila kitu; chakula cha kuanzia asubuhi mpaka jioni, nauli kama anatumia usafiri wa aina yoyote na chochote kingine anachopaswa kufanya.

Ingawa matumaini ya kufanikisha ndoto hiyo ni dhahiri, tunayo kazi ya kufanya. Ukweli kwamba uchumi wa gesi unaotegemewa kutoa mchango mkubwa kwenye Pato la Taifa na kuwezesha uwekezaji wa miradi endelevu ya maendeleo, unahitaji umakini haujatuonyesha mafanikio tunayoyasubiri. Hapa panahitaji busara na ushirikishwaji Watanzania wote kuainisha vipaumbele vya muda mrefu.

Gesi inaisha, hivyo ni lazima taifa lijipange kuendelea na maisha baada ya muda huo. Uchimbaji utakapogota na mtiririko wa fedha za kigeni kukauka Watanzania wanapaswa kuweka mikakati ya shughuli zitakazoendelea kuingiza fedha mifukoni na kufanikisha uzalishaji wa mali na huduma muhimu.

Kufika huko tunahitaji siasa safi zenye maridhiano. Wazo la kila mmoja wetu ni muhimu kwa kipindi hiki kuliko muda mwingine wowote.

Kwa hali ya kisiasa ilivyo nchini, sielewi ni nani anaipa kipaumbele hali na mwenendo wa uchumi wetu. Zinasikika harakati za kufanya maandamano kutoka Chadema huku CUF wakishindwa kufanya uchaguzi wao wa ndani kutokana na kutoelewana.

Jeshi la Polisi nalo, linashuhudiwa likifanya mazoezi yanayoelezwa kwamba ni ya kawida kutoka kila pembe ya nchi.

Wanaharakati na viongozi wa dini wamenyamaza, hakuna aliyesimama na kujaribu kuingilia kati majibizano yanayoendelea na kuongeza wingu juu ya nani yupo macho juu ya mwenendo wa uchumi wetu.

Haya yote yanatokea baada ya Serikali kutangaza kufuta mikutano na maandamano ya kisiasa, mpaka mwaka 2020 na kuwataka Watanzania wajikite kwenye ujenzi wa uchumi.

Labda wanasiasa na wataalamu wa fani hiyo wanajua zaidi kinachoendelea. Kwa mwananchi wa kawaida kama nilivyo tunakuwa kwenye wakati mgumu kutafakari kitakachotokea Septemba Mosi, endapo kila upande utakaza kamba.

Hata wasomi na wanazuoni wetu wamenyamaza kana kwamba hawaoni kinachoendelea bila kujali kuwa utekelezaji wa mikakati hii iliyopo baina ya Serikali na upinzani utaleta madhara kwa wote. Huenda yakawa ya muda mfupi au ya kudumu.

Chadema wakiingia barabarani na polisi wakatumia nguvu kuwazuia bila shaka uchumi utasimama kwa muda. Haieleweki ni muda gani ila itategemea na madhara yatakayotokea. Yakiwa madogo bila shaka muda utakuwa mfupi, lakini yakizidi sijajua itakuwaje.

Hili la pili likijiri, nawaona Watanzania kadhaa wakishindwa kumudu maisha yao. Uchumi utakuwa umeegesha kwenye foleni ndefu mpaka suluhu itakapopatikana. Nadhani ni busara suluhu hiyo ikapatikana kabla ya hatua hiyo haijafikiwa.

Nimuombe mtu au taasisi yenye dhamana na uchumi wa Tanzania, kuchukua hatua mapema na kuepusha ghasia hii ambayo huenda ikawa na madhara tusiyoyatarajia ili tupate nafasi ya kujadili namna tunayotoka hapa tulipo kuelekea Tanzania ya viwanda na uchumi wa kati.

Mwandishi anapatikana: 0759 354 122