Friday, February 17, 2017

KUTOKA MEZA YA MHARIRI WA JAMII: Waandishi wachunguze, kutathmini kutosambaza lolote lililopangwa

 

By Ndimara Tegambwage, Mwananchi

Wasomaji 162 wamenifikia kwa ujumbe wa simu (sms), kwa kupiga simu moja kwa moja na kwa maelezo ya ana kwa ana.

Hoja kuu katika makala hiyo ilikuwa umuhimu wa kuandika taarifa na habari kwa usahihi na bila kuweka “vikolezo” ama vya mtoa taarifa au vya mwandishi mwenyewe.

Tatizo la vikolezo vinaondoa hali halisi, vinaongeza au kupunguza utamu, ukali, uchungu au mchomo; vinatia moyo au vinadhoofisha na kudhalilisha.

Kukoleza kunaambatana na nia na shabaha nje ya hali, mazingira au tukio; lakini ndani ya utashi binafsi na lengo maalum. Somo hili lilitokana na taarifa zilizotolewa wiki iliyopita na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, akitwisha tuhuma mbalimbali baadhi ya wananchi zikiwamo kutumia, kuuza, kusafirisha au kufanya biashara ya dawa za kulevya.

Makala yangu ililenga kueleza kuwa kila mtoa taarifa ana lengo lake hata Makonda aliyeko kazini ana lengo lake. Je, mwandishi anajua lengo hilo? Amemhoji au anamnukuu tu na kusambaza?

Msomaji mmoja amesema “acha Makonda achape kazi yake;” wengine wawili wamesema “…waandishi waachwe kuripoti wanavyoona.” Ufuatao ni mrejesho wa baadhi ya wasomaji:

“Ulichosema ni kweli lakini wengi tumefungwa midomo. Sasa hivi ukisema kitu unafuatwafuatwa, hata kwenye mitandao binafsi kwenye intaneti, hata hili ulilojadili ni kama unatutega.

“Kama mkuu wa mkoa ameishasema na Rais amesapoti unataka sisi tuseme nini. Labda hilo ndilo somo. Ninyi mnaoandika mjifunze kuchuja vinginevyo mtafungwa au kupigwa faini mpaka mfilisike (tafadhali usiweke namba yangu).”

Benedict Kabadi, Sengerema (0787409200) anasema, “Asante sana kwa ushauri wako kwa waandishi wa habari (Mwananchi 10 Februari). Habari kuwa habari hutegemea uandishi. Zidi kuwaasa.”

Trasease wa 0656620772 anaandika, “Haitoshi kunukuu tu kile alichokisema mkuu wa mkoa. Mwende mbali zaidi. Je, alichosema ni kweli? Ni sahihi? Ana ushahidi? Kujiuliza maswali hayo kutazuia mwandishi na chombo chake kuulizwa maswali hayohayo hapo baadaye.

“Ninakumbuka madarasa yako wakati wa mafunzo juu ya uandishi wa habari za uchunguzi katika utawala bora ukiwa na Leah Mwainyekule miaka 10 iliyopita chini ya asasi ya Pact International.

“Wakati wote ulisisitiza kujenga shaka kwa taarifa yoyote au kauli yoyote na kuongeza kuwa hata kama mtoa taarifa alikuwa mama yako. Leo katika mazingira ya sasa ndiyo kuna umuhimu wa kujenga shaka zaidi. Hongera.”

Kutoka 0655614331 “Ujumbe wako uwafikie pia wanaoingiza maneno ya uongo katika mitandao ya kijamii kama vile Facebook, Twitter na Instagram.”

Edward Kitine (0652230523) Nimeipenda sana makala yako juu ya ‘Vita vya Makonda na waandishi wa habari wawe makini.’

“…kwa kweli umenichambulia kwa weledi suala la vita vya Makonda. Waandishi wa habari wawe makini. Wanatakiwa wawe na uelewa mpana na kuweka mizania siyo kunufaisha soko pekee. Wananchi tunahitaji kujua kiundani (0713937155).”

Ansbert Ngurumo anaandika, “…kwa vyombo vya habari; visipotafakari, visipochambua, visipotathmini, visipochunguza matukio au hatua zinazochukuliwa, vinaweza kutumika kupitishia lolote ambalo wenye nalo wanataka.

“Leo tunapotathmini matokeo ya Kikombe cha Babu (2011) tunasemaje? Tunaona ‘vigogo” wote walikimbilia Loliondo na umati wa wananchi ukawafuata kwa sababu (sisi waandishi wa habari) tuliwaelekeza huko.

“Walikufa wangapi njiani wakienda na kurudi kutoka Loliondo? Walikufa wangapi wakiwa Loliondo kwenye foleni? Walikufa wangapi nyumbani baada ya kutoroka hospitalini na kuacha dozi? Wakati tunahoji wengine, waandishi wa habari tuthubutu kujihoji ili kutimiza vema wajibu wetu (0767172665).”

Kutoka 0713489698 msomaji anaeleza, “…haitoshi kuwa kasuku. Mwandishi awe na shauku ya kujua kama alivyo msomaji au msikilizaji.

“Utaandikaje yale ambayo hata wewe mwenyewe huna majibu yake. Ok, umemaliza kuandika na msomaji yuko mbele yako anakuuliza kama una ushahidi wa ulichoandika. Huna. Unabaki kusema, ‘nilimnukuu mkuu.’

“Jakaya Kikwete alikuwa na mazoea ya kusema, ‘akili za kuambiwa changanya na zako’. Sasa mwandishi una majibu gani kwa maswali uliyoibua? Una uthibitisho kiasi gani? Kama huna majibu unatueleza nini?” Meza ya Mhariri wa Jamii itachapisha maoni ya wasomaji juu ya maudhui ya makala za kila Ijumaa na nyingne zinazotokea katika kurasa za gazeti hili. Tuandikie.

Mwandishi ni Mhariri wa Jamii wa vyombo vya habari vya Mwananchi Communications Limited wachapishaji wa magazeti ya The Citizen, Mwanaspoti na hili. Kwa maswali na hoja juu ya vyombo hivyo, wasiliana naye kwa simu: 0713614872 au 0763670229; e-mail: ndimara@yahoo.com au ntegambwage@tz.nationmedia.com

-->