Ulevi, sigara vyatajwa sababu ya kuzaa njiti

Muktasari:

Shirika la Chakula Duniani (WHO) limeeleza kwamba mtoto yoyote anayezaliwa na uzito chini ya 2.5kg (2500gm) yupo chini ya uzito wa kawaida (Prematurity).

Wajawazito wameshauriwa kuacha starehe na kuhudhuria kliniki mara kwa mara ili kuepuka tatizo la kujifungua watoto njiti

Shirika la Chakula Duniani (WHO) limeeleza kwamba mtoto yoyote anayezaliwa na uzito chini ya 2.5kg (2500gm) yupo chini ya uzito wa kawaida (Prematurity).

Inakadiriwa asilimia sita hadi saba ya watoto wanaozaliwa wapo chini ya uzito wa kawaida yaani 2500gm na kuhusisha asilimia 70 ya vifo vya watoto ndani ya siku 28 (neonate) pamoja na asilimia 50 ya watoto ndani ya mwaka mmoja (infants).

Hali ambayo mtoto ambaye bado hajazaliwa ni mdogo kuliko kawaida kwa sababu hakuwi ndani ya mfuko wa uzazi, ni moja ya chanzo kikubwa watoto kuzaliwa chini ya uzito wa kawaida hasa katika nchi zinazoendelea.

Watoto wanaozaliwa chini ya uzito wapo katika hatari ya utapiamlo, maradhi yanayojirudia kwani kinga inakuwa haijakomaa vya kutosha na pia kuchelewa kukua kwa mfumo wa fahamu.

Sababu ya kwanza mtoto kuzaliwa kabla ya muda chini ya wiki 37 za ujauzito kamili, huchangiwa na mama mjamzito hasa wanapokuwa na uzito mdogo, umri mdogo chini ya miaka 17, juu ya 35, kubeba mimba yenye zaidi ya mtoto mmoja ndani ya uzazi (mapacha).

Historia ya kujifungua mtoto chini ya uzito kipindi cha nyuma, matatizo katika shingo ya uzazi, kujifungua kabla ya muda kutokana na sababu mbalimbali kama vile maradhi mfano UTI, kisukari, magonjwa ya moyo, kiharusi na matatizo katika mfuko wa uzazi.

Mtoto ndani ya uzazi hakuwi kwa kawaida hivyo husababisha kuzaliwa na uzito mdogo (Intrauterine Growth Retardation) husababishwa na lishe mbovu kwa mama mjamzito kabla na hata baada ya kupata ujauzito.

Pia, sababu nyingine ni mama kuwa na kiharusi, au uwepo wa mtoto zaidi ya mmoja ndani ya mfuko wa uzazi (mapacha), malaria sugu, uvutaji sigara na matumizi ya vilevi (pombe) kupita kiasi wakati wa ujauzito.

Matatizo katika mfumo wa hewa husababisha mtoto kushindwa kupumua vizuri (birth asphyxia), kiwango cha chini cha sukari, maradhi kama vile Niumonya (kwenye mapafu) na Utandoubongo (meningitis). Hii ni kwa sababu kinga inakuwa haijakomaa kikamilifu, matatizo katika mfumo wa chakula, matatizo ya macho (retinopathy of prematurity), kiwango kikubwa cha bilirubini kwa sababu Ini halijakuwa kikamilifu kuweza kufanya kazi yake ya kuiondoa, matatizo ya kusikia, matatizo ya moyo na matatizo katika mfumo wa fahamu likiwamo tatizo la kisaikolojia.

Pia, kuna alama hatarishi kwa mtoto aliyezaliwa kabla ya muda chini ya uzito wa kawaida

Miongoni mwa alama hizo ni kuwa na uchovu mara kwa mara, kukataa kula chakula chochote, kuvimba tumbo, uso , miguu na kuharisha.

Lakini, hata hivyo tatizo hili linaweza kuepukika kwa kufanya kwa kuacha uvutaji sigara na kunywa pombe wakati wa ujauzito.

Pia, ikiwa mtu anashauriwa kuzingatia lishe bora, kwa wenye kisukari hakikisha kiwango cha sukari kipo sawa wakati wa ujauzito, ikiwa ni pamoja na kujikinga dhidi ya maradhi ya njia ya mkojo yaani (UTI).

Mwanamke anatakiwa kujikinga dhidi ya ugonjwa hatari wa malaria kwa kutumia chandarua kilicho salama pia ajitahidi kuepuka mimba katika umri mdogo hasa chini ya miaka 17 na mimba hasa juu ya miaka 35.

Daktari bingwa wa magonjwa ya wanawake nchini Cuba, Dk Jose Hernandez, anasema asilimia 80 ya sababu hizo zinaweza kudhibitiwa ikiwa mama atajipanga mapema kushika ujauzito miezi sita kabla, huku akitunzwa vema kwa kipindi chote mpaka kujifungua.

Dk Jose anasema matumizi yasiyo sahihi ya dawa ikiwamo dawa za magonjwa mbalimbali, pombe, dawa za kulevya yameongeza idadi ya wanawake kujifungua watoto njiti duniani. Anasema matumizi ya Cocain, Heroin, bangi, mirungi, sigara au kupata moshi kutoka kwa mtu anayevuta ni sababu tosha zinazosababish mjamzito kujifungua mtoto njiti.

Anasema wanaume wengi wamekuwa wakivuta sigara mbele ya wake zao, jambo linalohatarisha wajawazito.

Mambo mengine yanayoweza kusababisha tatizo hilo, anasema ni magonjwa mbalimbali kama shinikizo la damu na malaria. “Kuna ugonjwa wa malaria; ikiwa mama atapata wale wadudu, moja kwa moja wanakwenda kushambulia kwenye kondo ambalo ni utumbo maalumu unaomlisha mtoto kutoka kwa mama.

Kwa kuwa atakuwa ameshambuliwa na bakteria, atakuwa dhaifu na hatimaye kusababisha mazingira yatakayomlazimisha mtoto azaliwe kabla ya wakati.

Pia, anasema tatizo lingine ni upungufu wa vitamini mwilini, shambulio la bakteria kwenye njia ya mkojo maarufu kama UTI na upungufu wa damu. Iwapo damu ya mama ni ndogo inakuwa haimtoshelezi yeye na mtoto hivyo, mazingira hayo yatalazimisha azaliwe kabla ya muda wake kufika.

Sababu nyingine ni uwepo wa magonjwa ya zinaa kama kaswende, kisonono na virusi vya ukimwi (VVU). “Kujifungua mara kwa mara hasa bila kupitisha miaka miwili, huchangia kwa kiasi kikubwa kujifungua kabla ya wakati kwa kuwa kizazi chake kinakosa muda wa kupumzika na kujiandaa kwa ajili ya utungwaji wa mimba nyingine,” anasema.

Kinachoweza pia kusababisha mama kujifungua mtoto njiti, anasema ni mjamzito ambaye anapendelea kula vyakula vya vyenye sukari kwa wingi na wakati mwingine chumvi inapozidi.

Keneth Kammu, 0759 775788 (KENKAM)