KUTOKA MEZA YA MHARIRI WA JAMII: Kufukuzwa wabunge CUF, nani anafaa zaidi?

Muktasari:

Inadaiwa wamefukuzwa. Kwamba siyo wabunge tena wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na nafasi zao tayari zimezibwa kwa uteuzi mpya wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).

Wabunge wanane wa Chama cha Wananchi (CUF) wameondolewa kwenye orodha ya uwakilishi wa chama hicho.

Inadaiwa wamefukuzwa. Kwamba siyo wabunge tena wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na nafasi zao tayari zimezibwa kwa uteuzi mpya wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).

Nimewahi kuandika, katika safu hii, juu ya umuhimu wa mwandishi kushtuka, kushangaa na kujenga shaka. Hili ni jambo au tendo au tukio la kushtua.

Kinacholeta mshtuko na mshangao huleta hamu na sababu ya kutafuta zaidi – kuchunguza kwa nini kimetokea, kwa nini kimetendwa au kwa nini kinastusha na kushangaza.

Mwandishi anajua kuwa mbunge ni mwakilishi. Aweza kuwa amechaguliwa na wananchi katika jimbo lake; ameteuliwa na Rais au amepatikana kwa mfumo wa viti maalumu unaotokana na nguvu ya ushindi wa chama na uchaguzi ndani ya chama husika.

Ukishakuwa mbunge, kwa njia yoyote ile iliyotumika, wewe ni mbunge tu. Hakuna anayeweza kusema huyu ni mbunge zaidi ya mwingine. Kuchagua au kuteua, ni mfumo tu au utaratibu wa kumpata mbunge. Akishapatikana basi wabunge wote ni sawa – hakuna cha mwanamke au mwanamume.

Hapa basi, kwa wanaonukuu, wanaochambua na wanaotafiti matukio, taarifa na habari; ndipo kuna mshtuko. Ndipo kuna mshangao. Ndipo pa kutilia shaka. Hapa ndipo ilipo kazi ya mwandishi wa habari.

Kwa nini kuwe na mshutuko, mshangao na shaka? Kwanza, wote wanaofukuzwa ni wabunge wanawake. Pili, baadhi ya madai dhidi ya wabunge ni “kashfa” dhidi ya viongozi na “hujuma” wakati wa uchaguzi wa marudio wa madiwani wa 22 Januari mwaka huu.

Mwenyekiti ambaye inadaiwa kuwa anakashifiwa ni Profesa Ibrahim Lipumba ambaye bado “anapambana” kuhakikisha anakubalika na kutambulika kuwa amerudi kwenye nafasi yake ya uenyekiti aliyojiuzulu miezi miwili kabla ya Uchaghuzi Mkuu wa Oktoba 2015.

Inadaiwa ni Lipumba huyohuyo ambaye ameandika barua kwa Spika Job Ndugai akiorodhesha majina ya wabunge wanaopaswa kufukuzwa.

Kwenye orodha ya watuhumiwa na wanaodaiwa kufukuzwa, hakuna mbunge mwanamume. Waandishi waweza kuanzia hapa. Je, wabunge wanaume hawakashifu? Hawakuhujumu chama wakati wa uchaguzi wa marudio wa madiwani?

Je, ni kweli “makosa” waliyotwishwa wabunge wanawake hayawahusu wabunge wanaume au wanawake wanasimama kwa niaba ya wanaume?

Je, ni kweli hakuna wabunge wanaume wenye msimamo kama wanaodaiwa kuwa nao wabunge wanawake? Kama wapo, kwa nini wameachwa?

Je, huu waweza kuwa mkakati wa kupambana na wote – wabunge wanawake na wanaume; isipokuwa kinachodaiwa kuwa “kufukuza” wanawake ni mwanzo tu wa tufani? Hapa ndipo ilipo kazi ya mwandishi wa habari.

Je, tuhuma za kashfa si zina mahali pake – mahakamani; na tuhuma za “hujuma” kwa chama zaweza pia kusikilizwa hukohuko kwa kuwa chama kina hadhi ya kisheria ya kuweza kushtaki na kushtakiwa?

Katika nchi yenye utawala wa kidemokrasia, Bunge ni nguzo kuu ya wananchi ya kulinda na kutetea, pamoja na mambo mengine, uhuru wa wananchi wa kufikiri, kuwa na maoni na kutoa maoni hayo bila kizuizi.

Hapa ndipo ilipo kazi ya mwandishi wa habari: Kumtafuta anayedaiwa “kufukuza” wabunge na kumhoji: Huoni kuwa unaongeza mtibuano ndani ya chama chako na kupunguza nguvu na mshikamano, kwa jumla?

Waandishi wasonge mbele na kudadisi: Je, wanaoteuliwa kuziba nafasi za wabunge wanaodaiwa kufukuzwa wameandaliwa vipi? Wameandaliwa na nani? Waliandaliwa lini?

Je, kuna mpango gani wa kuandaa wale ambao hawajaandaliwa ili washike na kuzingatia msimamo wa watawala wao ambao wana uwezo wa ama kuwatiisha au kuwafukuza wakati wowote?

Waandishi waulize viongozi, watafute, watafiti na kuchambua, kwa nini kuna fukuzafukuza leo? Kwa nini haikuwapo jana au mapema mwaka huu?

Ni waandishi wadadisi ambao wanaweza kupata, kutoka kwa Profesa Lipumba, sababu za hatua ya sasa kabla ya kumalizika kwa mashauri yao mahakamani, kati ya pande mbili zinazopingana.

Chama cha Wananchi kimo katika mvutano. Huku ni wanachama wanaounga mkono Lipumba kurejea na kuwa mwenyekiti; kule ni wanaosimama na Katibu Mkuu Maalim Seif Shariff Hamad na kudai Lipumba aliishakimbia chama na kwamba hawezi kuwa kiongozi wao.

Waandishi watueleze: Ilikuwaje zoezi la kuondoa wabunge wa CUF lilitekelezwa kwa kasi, labda kwa wepesi na kukamilika kuweka wapya katika saa 72? Au ni mpango wa siku nyingi?

Wasiliana na Mhariri wa Jamii kwa namba: 0713 614 872/0763 670 229