Anza sasa kujiandaa kuishi bila ajira uzeeni

“Wapi unapokwenda?” Peter alipaza sauti kwa mkewe, Maria aliyekuwa akijiandaa kwenda kazini. Ilikuwa siku ya Jumatatu asubuhi Maria alifanya kila kitu kumfanya Peter ajisikie furaha awapo nyumbani peke yake.

Peter alistaafu kazi mwaka mmoja kabla uliopita. Aliamua kustaafu mapema kutokana na maumivu ya mgongo. Miezi 10 tangu astaafu kazi ilikuwa ya furaha kwake. Hakuwa anaamka asubuhi kuwahi kazini na mara kwa mara alitumia muda wake mwingi kukaa nyumbani akiangalia mpira kwenye runinga.

Utaratibu huo wa kupumzika muda mwili ulimsababishia Peter uzembe, ambapo mara nyingi alimshuhudia mkewe akijiandaa kwenda kazini huku nyuma akibaki peke yake.

Kwa upande wake, hali hiyo hatimaye iligeuka karaha hasa alipofikiria mkewe alikuwa na miaka kadhaa ya kuendelea kuwa kazini, jambo ambalo lingewatenganisha muda mwingi wa mchana katika kipindi kirefu cha maisha yao.

Ingawa Peter alikuwa na mawasiliano ya karibu na wafanyakazi wenzake wa zamani, hakuna simu alizokuwa akipigiwa mara kwa mara. Kuna wakati alishangaa kwa nini hakukuwa na yeyote mahali alikofanya kazi miaka mingi aliyekuwa akiukosa uwapo wake na hivyo kumpigia simu kama zamani.

Watu wengi hawapendi kuyaona madhara ya kustaafu mpaka wanapojikuta ndani ya hali hiyo. Ustaafu ni zaidi ya baridi kali ambayo humtenganisha mwajiriwa na taasisi aliyoitumikia.

Ni wazi kwamba, watu hutumia muda mwingi wa maisha yao katika sehemu zao za kazi. Hubuni urafiki fulani sehemu hizo, hupata vyeo, utambulisho na taswira ya kuvutia. Kwa wengi mahali pa kazi huwapatia kila wakitakacho. Pia huwapatia heshima na thamani maishani.

Hiyo ndiyo sababu inayoelezea uhusiano uliopo kati ya sehemu ya kazi na ustaafu pamoja, na madhara ya kisaikolojia anayokumbana nayo mstaafu, jambo ambalo watu wengi hawajiandai mapema kulikabili.

Sababu ya kustaafu au kuacha kazi pamoja na kiwango cha maandalizi baada ya kuondoka kwenye ajira hueleza uchungu anaokuwa nao mstaafu. Hata hivyo, muhimu kwa mwajiriwa ni maandalizi ya kustaafu.

 

Maandalizi kwa ajili ya kustaafu maana yake ni tathmini ya mambo kadhaa maishani - kubwa kuliko yote maandalizi ya kiuchumi (kifedha) kumwezesha mstaafu mtarajiwa kukabiliana na maisha yasiyokuwa na mshahara au posho anazopata kazini ambazo hatazipata.

Pia suala hilo huambatana na mipango ya awali ili hatimaye usiwe tegemezi wa kipato kilichokuwa kinakuja chenyewe kila baada ya kipindi fulani (hasa mshahara au posho).

Kustaafu huibua mambo mengi ambayo hata hivyo unaweza kuyakabili mapema. Chuki ya Peter iliyotokana na kuachwa nyumbani na Maria ilitokana na kutojiandaa mapema, maana aligeuka kuwa ‘mlinzi’ wa nyumba badala ya kuamkia katika kazi zingine binafsi.

Badala yake, licha ya ukweli kwamba alikuwa na tatizo la kiafya ambalo hata hivyo halikutishia maisha yake, alijikuta akishinda nyumbani bila kazi yoyote.

Pia hali ya ‘kutengwa’ kulikotokana na waliokuwa wafanyakazi wenzake ilimuongezea mzigo wa mawazo. Hali hiyo mara nyingi husababisha msongo wa mawazo na iwapo hutachukua hatua za kuikabili mapema inaweza kusababisha madhara zaidi ya kiafya.

Japokuwa katika ustaafu watu wengine huzowea unafuu na uhuru wa kufanya mambo yao zaidi kuliko ilivyo katika fungate la wanandoa, lakini athari zinazotokana na maadalizi duni pamoja na kutojiamini maishani husababisha afya za wastaafu wengi kuzorota baada ya muda mfupi.

Hali hiyo husababishwa mara nyingi na wastaafu hao kutokuwa na kazi nyingine ya kufanya wala mahali pa kujishikiza panapoweza kuifanya akili ifanye kazi ya ziada kuushurutisha mwili ujione uko kazini.

Ndiyo maana wakati huo (kwa wasiojiandaa mapema wawapo kazini) huanza kujiona hawana maana wala utambulisho waliouzowea na kuanza kuhoji uwapo wao duniani.

Hatua hiyo huashiria kwamba watu hao wanapaswa kurejea au kusaka malisho na utambulisho mpya. Kupata ajira na utambulisho mwingine humfanya mtu aondokane na upweke wa kukaa nyumbani akitazama runinga.

Hata hivyo, iwapo umri wake umegota na hawezi kupata kazi kwa urahisi, huo ndio unaweza kuwa mwisho wa kutamba au kuonekana kwa mstaafu.

Tofauti na wanaume, wanawake huweza kutengeneza mzunguko wa uhusiano na utambulisho nje ya kazi, ikiwamo kujiunga katika vyama vya kinamama vya kuendelezana, kusaidiana au urafiki. Uzoefu unaonyesha kwamba hata baada ya ajira, wanawake wanaweza kuendeleza uhusiano huo.

 

Pangilia maisha yako mapema

Hata hivyo lililo dhahiri ni kuwa mipango mizuri ya kustaafu inamtaka mfanyakazi aanze kujipanga na kupangilia maisha ya ustaafu tangu siku yake ya kwanza kazini.

Inashauriwa kwamba unapopata barua ya ajira pangilia pato lako utakavyoligawa kila linapoingia. Fahamu jinsi gani unavyopaswa ‘kusevu’ na kuwekeza ili kujiandalia ajira nyingine baada ya kuondoka kazini.

Watafiti wa mambo ya maisha wanasema kustaafu hakuwahusu wazee pekee, bali hata vijana maana kwa kuwekeza, kujinyima na kuanzisha miradi kunaweza kukufanya ukaachana mapema na ‘utumwa’ wa kuwatumikia watu wengine.

Hiyo ina maana kuwa mipango ya kustaafu ni kufanya maandalizi ya muda mrefu ya kifedha, kiafya na mambo mengine muhimu ya maisha.

Ni vyema ukajua kwamba matumizi yako ya fedha yatakuja kukuweka katika nafasi gani utakapofikia wakati wa kuondoka kazini. Pesa nyingi au chache unazopata wakati huu zitakuja kuamua hatma ya uzee wako iwapo utaishi miaka mingi zaidi (baada ya ajira) ama la.

Mara nyingi rika la ujana huwadanganya watu. Maneno ya “wakati ukifika nitafanya...”, “bado bado nipo” na “ngoja nipate milioni 50 ndipo nianze au niwekeze” huwasumbua na baada ya kujikuta hawana pa kushika, huanza kujuta. Ni vyema ikaeleweka kuwa, kila shilingi moja uipatayo unaweza kuigawa ikaja kukunufaisha zaidi uzeeni.

Ipo hoja nyingine katika maisha ya ustaafu. Hoja hiyo inahusiana na umri, jambo ambalo halikwepeki. Kila mtu umri wake unapofika miaka ya kuondoka kazini kisheria huondoka au kujiondoa katika ajira. Hata hivyo anapokuwa amefanya maandalizi ya kutosha ili kuhakikisha hatatetereka huko aendako, anaweza kuishi kama alivyokuwa kazini.

Shirika la Kazi duniani (ILO) liliwahi kupendekeza kwa mataifa wanachama kuwa na ukomo wa umri wa wafanyakazi. Katika mapendekezo hayo, ILO ilizitaka nchi hizo kusimamia matakwa ya ukomo wa ajira kisheria.

Suala hilo liliifanya Serikali ya Tanzania kuridhia na kutunga sheria mbalimbali za kazi, ikiwamo ya Ajira na Uhusiano Kazini namba 6 ya mwaka 2004, Sheria ya Taasisi za Usimamizi wa Kazi namba 7 ya mwaka 2004, Sheria ya Afya na Usalama Kazini namba 5 ya mwaka 2003 na Sheria ya Hifadhi za Jamii ya mwaka 2008.

Hata hivyo, changamoto inabaki katika maandalizi ya kustaafu, jambo ambalo limekuwa kikwazo kwa watumishi, kwani wengi hawajiandalii mazingira hayo mapema.

Inawezekana uzembe au matanuzi yakawa chanzo, lakini maisha ya baada ya ajira ndiyo ‘yanayomuanika’ mtu anapoondoka kazini. Huu ni wakati wako mfanyakazi kujiandaa kustaafu.