Maprofesa janga, wabunge wachambua hali halisi vyuo vikuu

Mbunge wa kasulu Mjini, Profesa Joyce Ndalichako akizungumza bungeni wakati akichangia mjadala wa kupitisha makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa mwaka wa fedha 2024 / 2025, jijini Dodoma leo Mei 8, 2024. Picha na Edwin Mjwahuzi

Muktasari:

  • Mwaka 2017, utafiti uliofanywa na Chama cha Wafanyakazi wa Elimu ya Juu (THTU), ulibaini  kuwa asilimia 53 ya watumishi wanataaluma katika ngazi ya uandamizi na kuendelea, waliokuwa vyuoni walishastaafu.

Dodoma. Wabunge wametema nyongo kuhusu mustakabali wa elimu nchini, akiwamo mmoja aliyeonyesha wasiwasi wa ubora wa elimu, kwa vyuo vikuu kuwa na uhaba wa wahadhiri kwa ngazi ya uprofesa.

Mbunge wa Viti Maalumu, Dk Tea Ntala amedai  kwa sasa nchini kuna maprofesa 93, huku vyuo vilivyopo vikihitaji maprofesa 516.

“Kwa sasa nchini tunao maprofesa 93 ambao wakifika miaka 70 tunataka wastaafu huku wengine hamjawajenga. Nashauri tuongeze muda wa miaka ya kustaafu na tuhakikishe tunaongeza wengine kutoka nje ya nchi,” amedai Dk Ntala pasipo kutaja rejea aliyoitumia kutoa takwimu hizo.

Naye Mbunge wa Muleba Kusini, Dk Oscar Ishengoma amedai janga hilo la upungufu wa maprofesa,  limekikumba Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ambacho kilitakiwa kuwa na maprofesa 161, lakini kwa sasa wapo  93.

Kilio cha wahadhiri vyuoni ni cha muda mrefu Mwaka 2017, utafiti uliofanywa na Chama cha Wafanyakazi wa Elimu ya Juu (THTU), ulibaini  kuwa asilimia 53 ya watumishi wanataaluma katika ngazi ya uandamizi na kuendelea waliokuwa vyuoni walishastaafu,   hivyo walikuwa wakifanya kazi kwa mikataba.


Maprofesa wavichambua vyuo

Maprofesa kadhaa ambao ni wabunge leo Jumatano Mei 8, 2024 wametoa hoja mbalimbali za kuboresha mfumo wa elimu, ikiwamo kuanzisha kituo cha maarifa ya asili.

Pia, wasomi hao wamesema kunapaswa kufufuliwa vyama vya kitaaluma, ushauri unaotolewa na wathibiti ubora wa elimu ufanyiwe kazi na vyuo vikuu visitanue kwa kufungua kampasi mikoani.

Maprofesa hao, Palamagamba Kabudi, Sospeter Muhongo, Joyce Ndalichako, Patrick Ndakidemi na Shukrani Manya,  wamesema hayo wakati wakichangia makadirio ya mapato na matumizi ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa mwaka 2024/25, iliyowasilishwa na Waziri wake, Profesa Adolf Mkenda.

Makadirio hayo ya Sh1.9 trilioni ambapo Sh637.2 bilioni ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida na Sh1.3 trilioni kwa ajili ya miradi ya maendeleo,  yamepitishwa leo na Bunge, huku ikishuhudiwa wabunge mbalimbali wakionesha kasoro za ubora wa elimu na kutoa mapendekezo.

Ukimwacha Profesa Ndakidemi, maprofesa wengine Kabudi, Muhongo, Ndalichako na Manya wamewahi kushika nafasi za uwaziri katika Serikali ya awamu ya tano ya hayati John Magufuli pamoja na ya sasa ya Rais Samia Suluhu Hassan.

Maprofesa Kabudi na Muhongo kwenye michango yao walifanya rejea ya mabadiliko ya sekta ya elimu tangu Serikali ya awamu ya kwanza iliyoongozwa na Mwalimu Julius Nyerere, huku wakisema nchi imepuuza maarifa ya asili ambayo ni utajiri uliopo Tanzania, lakini unachukuliwa na mataifa ya kigeni.

Profesa Muhongo ambaye naye alimtumia zaidi Mwalimu Nyerere katika kufanya rejea zake,  alimuomba Profesa Mkenda kufufua vyama vya kitaaluma kama vile chama cha Hisabati na chama cha Fizikia, kwamba matatizo yaliyopo kwenye masomo hayo yangeshughulikiwa na vyama hivyo.

Mbali na maprofesa Kabudi na Muhongo, maprofesa Ndalichako na Manya walisisitiza ubora wa elimu vyuoni.

Kabudi ambaye ni Profesa wa Sheria wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) hadi mwaka 2017 alipoteuliwa na Rais Magufuli kuwa mbunge na kuteuliwa na baadaye waziri,  alisema maarifa ya asili ni eneo la utajiri katika bara la Afrika na hasa Tanzania.

“Lakini ni eneo ambalo tumelipuuza na leo tunapoteza maarifa ya asili yetu yote yanakwenda kuhifadhiwa Marekani, yanakwenda kuhifadhiwa Ulaya, sisi tunayapuuza, wao wanakuja kuyachukua tubadilike,’’ amesema na kuongeza:

“Sasa hivi Uswisi wanaandaa dawa ya kutibia kifafa na mimea hiyo wameitoa Tanzania, maarifa haya wametoa kwa wataalamu wa tiba ya kiasili wa Kinyamwezi. Pia, kwa kutumia mimea kutoka kwetu wanatengeneza dawa ya kutibia saratani. Sasa wanachukua dawa na wanachukua mali.’’

Mbunge wa Musoma Vijijini, Profesa Sospeter Muhongo.

Profesa Kabudi, ambaye alihudumia pia Wizara ya Mambo ya Nje na baadaye kurejea kwenye Wizara ya Katiba na Sheria,  alishauri Tanzania iige mfano wa nchi za  India na China kwa kuanzisha vituo vya maarifa ya asili kwenye vyuo vikuu.

“Nashauri tuige mfano wa India wanakwenda anga za juu, wametua kwa mara ya kwanza na kutua mwezini, lakini wana kituo cha maarifa ya asili.

“Napendekeza vyuo vyetu vianzishe vituo vya maarifa ya asili na twende kujifunza India na China, tuanzishe pia maktaba ya utamaduni ya kidijitali ambayo inaweza ikatunzwa na Costech (Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia nchini Tanzania),” amesema

“Lakini twende kwenye ilani ya CCM, imehamasisha kuanzisha mashamba ya mimea dawa na kuanzisha kiwanda kikubwa cha dawa za mimea dawa, na sisi ni mabingwa wa kuanzisha taasisi ambazo baadaye zinakufa, lakini wenzetu wanakuja kujifunza mambo ya mimea dawa hapa kwetu,” amesema Profesa Kabudi.

Profesa Kabudi pia ameomba Taifa liwekeze kwenye utafiti na maendeleo kwa kutenga bajeti kwa ajili hiyo ili nchi iweze kufanya tafiti zake ambazo zinaendana na mahitaji ya nchi.

Pia, Profesa Kabudi aliyekuwa mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba,  alishauri somo la michezo libadilishwe jina na kuitwa sayansi ya michezo,  kwa sababu wanafunzi hao watasoma fiziolojia, anatomia, saikolojia na wa ili watu wasiseme ni michezo tu iwe ni sayansi ya michezo.


Mhongo azishangaa tahasusi 65

Profesa Muhongo, ambaye aliwahi kuwa Waziri wa Nishati na Madini, ametaka wizara ifufue vyama vya kitaaluma ili matatizo kwenye masomo yapelekwe kwa wanachama ambao inakuwa rahisi kushauri na kwa gharama nafuu.

Profesa Muhongo ambaye kutokana na ufaulu wake wa juu alipata ufadhili kwenda kusoma shahada ya uzamili katika Chuo Kikuu cha Guttingen, Ujerumani na baada ya kuihitimu, aliendelea na Shahada ya Uzamivu (PhD) katika Chuo Kikuu cha Ufundi cha Berlin akibobea katika eneo jiolojia,  amesema tahasusi 65 mpya zilizoanzishwa na Serikali hazilitayarishi Taifa kwenda kwenye maendeleo ya  sayansi.

“Tahasusi za kidato cha tano na sita, yaani tahasusi nimeangalia yaani profesa unazo 65 kwenye ‘High school’. Ukichukua vyumba viwili vya sanaa na sayansi, hatutayarishi Taifa kwenda kwenye sayansi, wanafunzi wengi watajaa vyuo vikuu, lakini katika hawa watakaokuwa wanasoma sayansi yenyewe ni asilimia 10 tu. Kama tunataka kwenda kwenye sayansi na teknolojia hii,  lazima tubadilishe,” amesema Profesa Muhongo ambaye ni Mbunge wa Musoma Vijijini, Mkoa wa Mara.

Pia, ameshauri wizara katika kipindi cha baada ya miaka mitatu iwapime wanafunzi kwa kutumia vipimo vya kimataifa na kipimo cha kwanza ambacho anataka Tanzania ishiriki kinaitwa ‘PISA’ (Program for International Student Assessment).

“PISA, hii inapima watoto wenye umri wa miaka 15 kama mambo waliyojifunza shuleni wanaweza kutatua matatizo yaliyowazunguka duniani, twende huko,” amesema.

“Kipimo cha pili, ni TIMSS (Trends in International Mathematics and Science Study), hii inachukuwa watoto walioko kwenye hatua ya nane wanaangalia ujuzi wao na maarifa waliyopata shuleni.

“Sasa haya ni mashindano yanayofanywa kitaifa na Tanzania naomba baada ya miaka miwili, mitatu profesa hebu nenda Pisa na Timss ndio tutajua tuko sahihi, vijana wetu wa miaka 15 wakapambane kule,” amesema.

Pia, amesema vyuo vikuu vya sasa vimekuwa vya Kitanzania mno.

 “Havina afya kitaaluma kwa sababu huwezi kukuta maprofesa wametoka nchi nyingine kuja kufundisha kwenye vyuo vyetu,” amesema.

Kwa upande wake, Profesa Patrick Ndakidemi,  ametaka Serikali kuwekeza kikamilifu kwenye uendeshaji wa vyuo vikuu hapa nchini ili viweze kutoa wahitimu waliopata elimu bora watakaoweza kupambana kwenye soko la ajira.

“Ushauri wangu kwa Serikali tuwe na programu ya kuwasomesha vijana wetu hadi shahada za uzamivu  za uhakika tena wakasomeshwe nje wapate uzoefu wa kimataifa,” amesema Ndekidemi, ambaye ni Mbunge wa Moshi Vijijini.


Ndalichako aigusa mitalaa, wathibiti ubora wa elimu

Profesa Ndalichako ambaye amewahi kuwa Waziri wa Elimu kwa zaidi ya miaka mitano kabla ya kumwachia kijiti Profesa Mkenda,  amesema utekelezaji wa mitalaa unahitaji mambo mengi, ikiwamo mwanafunzi mwenyewe, mwalimu, mazingira ya shule, vifaa vya kujifunzia na kufundishia pamoja na mfumo wa ufuatiliaji na uthibiti wa elimu.

“Upande wa walimu, mwalimu ndiyo nguzo na nyenzo katika ufanisi wa utekelezaji wa mitalaa. Niombe pamoja na kuwapa mafunzo walimu,  bado hayatoshi, niombe mafunzo hayo yawe endelevu.

“Serikali iangalie shule ambazo zina uhaba wa walimu iendelee kuajiri, elimu inataka mafunzo kwa vitendo na mafunzo kwa vitendo lazima uwe na walimu wa kutosha, uwe na vifaa vya kutosha na uwe na rasilimali katika kutekeleza mtalaa kwenye mkondo wa amali,” amesema Ndalichako, aliyewahi pia  kuwa  Katibu Mtendaji  wa Baraza la Mitihani Tanzania (Necta).

Profesa Ndalichako ambaye alikuwa mhadhiri mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam akifundisha masuala ya vipimo vya kielimu na tathmini ya elimu, mbinu za utafiti na takwimu za kielimu alieleza kuhusu umuhimu wa uthibiti ubora katika shule.

“Wathibiti ubora ndio jicho la Serikali katika kuhakikisha elimu inatolewa kwa viwango ambavyo vimewekwa, ni muhimu sana wathibiti ubora waangaliwe kwa jicho la kipekee.

“Mageuzi ni makubwa kusipokuwa na usimamizi na ufuatiliaji wa umakini,  malengo yaliyokusudiwa yanaweza yasifikiwe,” amesema Profesa Ndalichako, ambaye ni Mbunge wa Kasulu Mjini, Mkoa wa Kigoma.

Pia, amesisitiza ushauri unaotolewa na wathibiti ubora wa shule ufanyiwe kazi, maana mara nyingi wamekuwa wakikagua na kuandika ripoti zao lakini zimekuwa ni kama kitu cha kawaida kwa kutofanyiwa kazi.


Idadi ya wanafunzi, hadhi ya maprofesa

Profesa Manya akichangia mjadala huo alisema miongoni mwa matatizo ni wanafunzi wa vyuo kuishi nje ya chuo ambako wanakumbana na changamoto za maisha kama kukosa kodi ya pango.

Profesa Manya ambaye ni mbobezi wa masuala ya jiolojia aliyesomea Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, kuanzia shahada ya kwanza (1994-1995), uzamili (1999-2001) na uzamivu (2001-2005) na alianza kuwa mhadhiri msaidizi wa UDSM mwaka 2001, alizungumzia pia tatizo la idadi kubwa ya wanafunzi vyuoni.

Alitoa mfano wa Chuo Kikuu cha Dar es Saalaam (UDSM) kwamba maabara zinazopaswa kuhudumia wanafunzi 20 kwa sasa zinahudumia wanafunzi 200 hadi 300

“Kwa mazingira haya, hayawezi kuleta ule ubora unaokusudiwa kwenye elimu ya mafunzo kwa vitendo.”

Profesa Manya, aliyewahi kuwa Naibu Waziri wa Madini amesema mhadhiri mmoja anajikuta na darasa la wanafunzi 800 hadi 1,000 ambao ni wengi na uwiano wa idadi ya wanafunzi kwa mhadhiri mmoja ndio kigezo cha kimataifa katika kupima ubora wa vyuo vikuu.

“Hata miundombinu ya vyoo katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, vyoo vinatakiwa kuhudumia watu 4,000 sasa vinahudumia watu 20,000 na havijaongezeka sana,” amesema Profesa Manya, aliyewahi pia kuwa Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini.

Pia, amesema wahadhiri hadi wanne wanachangia ofisi inayopaswa kutumiwa na mhadhiri mmoja kiasi cha mhadhiri  kukosa hata nafasi ya  kuzungumza na mwanafunzi wake.


Majibu ya Wizara

Akihitimisha hoja, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda,  amesema amepokea maoni, ushauri na mapendekezo yote yaliyotolewa na wabunge wakiwemo maprofesa na kwamba anayachukua kama yalivyo kwenda kuyafanyia kazi.

“Tunataka kuboresha mazingira ya wanafunzi chuo kikuu, tunataka walimu wawe na ofisi za kutosha, wakae kwa kujinafasi vizuri waendelee kufundisha,” amesema.

Profesa Mkenda amesema Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa sasa inatekeleza Mradi wa Mageuzi ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET), unaolenga katika kuboresha miundombinu.

Amesema mradi huo umewekeza Sh1 trilioni kwa ajili ya kugharamia uboreshaji wa miundombinu kwenye vyuo vikuu na kufungua kampasi nyingine kwa ajili ya kuondoa msongamano.