Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Wadau waeleza sababu maprofesa kuwa wachache

Muktasari:

  • Wakati Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia hadi kufikia mwaka 2022 Tanzania kulikuwa na maprofesa 226, kati yao 163 ni maprofesa washiriki huku 63 ni maprofesa kamili, wadau waeleza mbinu za kuongeza wasomi hao.

Dodoma. Wadau wa elimu wametaja mambo matano yanayosababisha uwepo wa idadi ndogo ya maprofesa nchini ikiwemo kukosa fedha za kufanya utafiti wenye tija na utakaokubalika.

 Mengine ni kukazwa kwa masharti ya kupanda hadi kuwa profesa, taratibu za kiserikali kuwa si rafiki kwa mazingira ya wanataaluma kutimiza majukumu yao, ugumu wa kazi za kitaaluma usioendana na motisha na tambo pamoja na majigambo miongoni mwa wahadhiri wenyewe.

Kwa mujibu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia hadi kufikia mwaka 2022 Tanzania kulikuwa na maprofesa 226, kati yao 163 ni maprofesa washiriki huku 63 ni maprofesa kamili.

Akizungumza na Mwananchi digital leo Oktoba 13 jijini hapa, Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyakazi wa Elimu ya Juu, Dk Paul Loisulie amesema ukosefu wa fedha za utafiti ni miongoni mwa mambo yanayokwamisha wengi kutafuta uprofesa.

“Utafiti mwingi unahitaji fedha ambayo nchi za kiafrika hazina. Feda nyingi za kufanyia utafiti zinategemewa kutoka kwa wafadhili,” amesema.

Akielezea kuhusu kukwazwa kwa masharti ya kupanda hadi kuwa profesa, Dk Loisulie amesema vyuo vina miongozo inayoelezea taratibu za wahadhiri kupanda kuwa maprofesa.

Amesema taratibu hizo ni pamoja na kuwa na machapisho ya makala kwenye majarida yenye hadhi, kuvutia miradi yenye pesa, kufanya ushauri elekezi, kuhudhuria makongamano ya kitaifa na kimataifa, uandishi wa vitabu na kufundisha.

“Pamoja na kwamba masharti haya yanasaidia kutunza heahima ya taaluma na uanazuoni, wahadhiri wengi wanapambana kutimiza masharti haya na huwa wengi wanachelewa kuzitimiza. Wengine hata wanastaafu hawajafikia,” amesema.

Pia Dk Loisulie amesema taratibu za kiserikali si rafiki kwa mazingira ya wanataaluma kutimiza majukumu yao na kutoa mfano kuwa mwanataaluma hawezi kupanda daraja kuelekea kwenye uprofesa kwa kukaa miaka mitatu kama watumishi wengine.

Amesema mhadhiri atapanda kuwa profesa hadi akitimiza vigezo hata kama ni kwa miaka 10 na kuwa wakati mwingine hata mtu akitimiza vigezo Serikali inaibua masharti mengine ya mtu kusubiri bajeti ipatikane ili apandishwe.

Amesema hali hiyo inawafanya wanataaluma wapoteze munkari kufanya jitihada za kupata uprofesa.


Kuhusu, ugumu wa kazi za taaluma kutoendana na motisha inayotolewa kama taasisi nyingine Serikalini, Dk Loisulie ambaye pia ni Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom) amesema wahadhiri wanatumia muda wao mwingi kujiendeleza na kuandaa wengine.

“Ikifika muda wa kustaafu wanajikuta wako hoi kiuchumi pamoja na sifa lukuki za kitaaluma. Ndiyo maana siku hizi baadhi wanajaribu kukwepa au kupunguza uwekezaji kwenye taaluma na kuchomekea na mambo mengine ya kimaisha. Matokeo yake wanachelewa kufikia ngazi ya uprofesa,” amesema.

Kwa upande wa tambo na majigambo miongoni mwa wahadhiri wenyewe, Dk Loisulie amesema wale waliofanikiwa huwa wanakuwa na majigambo na hivyo kukosoa machapisho ya wenzao kiasi cha kuwakatisha wengine tamaa au hata kuwachelewesha.


Uanzishwe mfuko wa utafiti

Naye Mbunge wa Manyoni Mashariki aliyewahi kuwa mhadhiri wa elimu ya juu, Dk Pius Chaya amesema kufanya utafiti ni gharama na kuwa tafiti moja ya kawaida inahitaji Sh30 milioni hadi Sh 50 milioni na za kisayansi zinafika hadi Sh1 bilioni.

“Ukiangalia kwa haraka haraka bado Serikali haijawekeza vyakutosha kwenye utafiti na ni eneo tunahitaji kuishauri Serikali. Lakini Serikali imeanza kuongeza bajeti katika suala la utafiti lakini bado tunahitaji kuja na kitu mbadala. Kwa mfano mimi ninashauri tuje na mfuko wa utafiti,” amesema.

Amesema mfuko huo, ujumuishe fedha zote za utafiti zikiwemo zinazotokana na ufadhili kutoka maeneo mbalimbali na zitawanywe kwenye vyuo vyote nchini vinavyotokana na maeneo ambayo wafadhili wanataka ziende.

“Kuna tatizo jingine hata aina ya tafiti, zinazoandikwa na watu wetu, ukuta dokta anaandika tafiti nyingi lakini hazikubaliki…Kama tutawekeza vizuri kwenye fedha vijana wengi watashawishika kufanya utafiti wenye tija matokeo ya utafiti yatawawezesha kuandika paper,”amesema.

Amesema wapo shahada ya uzamivu kwa miaka 10 lakini hajawahi kuandika tafiti hata moja ambayo inawezesha kuchapishwa katika majalida ya kimataifa.

Dk Chaya ameshauri ufike wakati ambapo vyuo vikuu nchini vitauza tafiti zinazofanya kwa taasisi zinazohusika na aina ya utafiti utakaofanyika ili kuwezesha mzunguko wa fedha za kufanyia shughuli hiyo.

Septemba 5 mwaka huu Mbunge wa Muleba Kusini (CCM), Dk Oscar Ishengoma, alitaka kufahamu na Serikali inampango gani wa kuongeza fedha ili kuvutia vijana wengi kusoma kufikia ngazi hiyo na hivyo kufanya tafiti na kufikia hatua ya uprofesa.

Pia alitoa mfano katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), wanahitajika maprofesa 161 lakini waliopo hivi sasa ni tisa tu.


Akijibu swali hilo, Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Omary Kipanga alisema kuongezeka kwa idadi ya maprofesa kunategemea zaidi jitihadi za mtu binafsi katika utekelezaji wa majukumu yake na kukubalika kwa jitihada hizo kwa wanataaluma wenziwe kwa kuzingatia miongozo waliyojiwekea.

Kwa mujibu wa Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda katika bajeti ya mwaka 2022/23 Serikali ilianza utaratibu wa kutenga fedha kwa ajili ya watafiti kutoka vyuo vikuu ambao watachapisha matokeo ya tafiti zao katika majarida yenye hadhi ya kimataifa.

Katika mwaka huo, Serikali ilitenga Sh1 bilioni moja, kwa ajili ya tuzo kwa watafiti

 waliokidhi vigezo katika mkondo wa afya, sayansi tiba pamoja na Sayansi asilia na hisabati, Tehama, uhandisi, sayansi ya kilimo na wanyama.