Dakika 268, pointi nane vyapotea

Muktasari:

Ukipiga hesabu, Yanga imepoteza dakika 268 na pointi nane kati ya tisa muhimu katika mechi zake tatu za Kombe la Shirikisho la Soka Afrika.

Ukipiga hesabu, Yanga imepoteza dakika 268 na pointi nane kati ya tisa muhimu katika mechi zake tatu za Kombe la Shirikisho la Soka Afrika.

Ni kama hesabu zisizohesabika kufuzu kwa sababu, baada ya mchezo dhidi ya TP Mazembe, ambao Yanga ilipigwa bao 1-0, Pluijm alisema, wamepoteza mbili, matumaini yatakuwa mechi ya marudiano dhidi ya Medeama na mchezo wa juzi wamepoteza pointi mbili.

Yanga ilitumia dakika 180 kwa mechi ya Mo Bejaia na ile ya TP Mazembe ambazo walifungwa bao 1-0 lakini ilitumia dakika mbili kupata bao la kwanza kwa mchezo na Medeama na ilishindwa kufanya chochote ndani ya dakika nyingine 88.

Kimahesabu, Yanga ina nafasi ngumu kwa kuwa, ina ‘advantage’ ya mchezo mmoja dhidi ya Mo Bejaia nyumbani baada ya dakika 268 kwa nyumbani na ugenini.

Pamoja na matokeo hayo, kocha wake, Hans Pluijm anasema, matumaini ya Yanga yapo na ana imani itashinda mechi zilizosalia.

Kwa upande mwingine, Yanga imetumia dakika 180 kwa mechi za nyumbani, ikitoka sare moja na kufungwa moja na inasubiri kutimiza dakika 270 kati ya Agosti 12, 13 na 14 kwa kupambana na Mo Bejaia kwenye Uwanja wa Taifa.

Mechi za ugenini za Yanga zitakuwa kati ya Julai 26 na 27 itakaporudiana na Medeama na baadaye TP Mazembe kati ya Agosti 23 na 24 na hapo Yanga itakuwa imekamilisha dakika 540 kwa mechi zote sita. Mpaka sasa imebakisha dakika 270 za kudhihirisha kuwa iliteleza katika dakika 268 ilizokwisha kucheza.

 

Yanga vs Medeama

Wachezaji wa Yanga walionekana kukosa kujituma, kujiamini, hawafahamiani pamoja na kupoteza mipira kirahisi.

Eneo la kujiamini na kupoteza mipira kirahisi; wachezaji walikuwa wakiharibu mipira kwa kutoa pasi butu, kila mara, Simon Msuva, Vincent Bossou na Amiss Tambwe hawakuwa makini. Tambwe alitolewa na nafasi yake kuchukuliwa na Juma Mahadhi.

Msuva alianza vizuri, lakini baadaye akapotea kwenye ramani sajari na Juma Abdul ambaye hakuwa katika ubora wake wa kunyunyiza majalo.

Kutokujiamini ni ugonjwa ambao tiba yake ni mechi za kimataifa za mfululizo. Inatakiwa Yanga ipate mechi nyingi za kimataifa za kirafiki ili kujenga kujiamini, kucheza kwa kujiachia kitu ambacho hakipo kwa Yanga.

Kukosekana kwa hayo, kunawafanya Yanga kucheza mpira mgumu na wa wasiwasi kiasi cha kushindwa kudhibiti mipira ambayo ama ilipotea au ilitoka nje.

Kushindwa kufahamiana ni kumpelekea mtu mpira wakati hayuko kwenye njia (penetration pass). Pasi zilipitishwa kwa kuhisiwa, na ziliishia kupotea kwa kuwa anayehisiwa kuwa atakuwa kwenye njia ama hakuwa na mawazo au kushindwa kuufikia mpira.

Yanga ilijaribu kutumia mfumo wa 3:5:2 na 2:5:3 huku Kelvin Yondan akipanda, lakini ilishindikana na kuonekana mfumo kuwa mgumu.

Mfumo huo uliruhusu kushambulia kupitia pembeni kwa kuwatumia Msuva na Juma Abdul na wakati mwingine Obrey Chirwa na pia kupitia katikati kazi aliyoifanya Kelvin Yondani. Hata hivyo, staili ya Medeama ya kupaki basi ilikuwa ngumu na wenyewe kukosa ujanja wa kuwavuta na kufanya shambulizi la kushtukiza kwa kutumia mipira mirefu.