Hawa wamegoma kuchuja kwenye muziki

Muktasari:

Ni kweli muziki unabadilika kutokana na wakati. Mabadiliko haya yamewaacha njiani wanamuziki wengi waliogoma kubadilika, lakini wapo wabishi waliotoboa na hata baada ya miaka 15 bado wanatamba.

Muziki mgumu, muziki unabadilika, kwenye muziki kuna kujuana, wanamuziki tunabaniwa na mengine mengi ni baadhi ya kauli za visingizio pale msanii anapopotea katika ramani ya muziki.

Ni kweli muziki unabadilika kutokana na wakati. Mabadiliko haya yamewaacha njiani wanamuziki wengi waliogoma kubadilika, lakini wapo wabishi waliotoboa na hata baada ya miaka 15 bado wanatamba.

Wasanii hawa wameendelea kutamba siyo kwa kubahatisha nyimbo mbili tatu, katika kipindi hiki wamemudu kubaki katika chati, kutwaa tuzo, kutoa nyimbo kali karibu kila mwaka.

Mgumu Fid Q, Malkia Lady Jay Dee, Prince Dully Sykes, Mzee wa Komesho AY, Bingwa wa Mapozi Mr Blue, Mkongwe Profesa Jay na Binamu Mwana FA wanaingia katika orodha hii.

Jina- Fid Q

Kuanza muziki- Mwaka 2000

Albamu- Fid Q.Com

Vina Kati Mwanzo na Mwisho

Propaganda

Akiwakilisha vyema kutoka Mwanza, mkongwe katika muziki wa Hiphop na mwenye mashairi kuntu, Fid Q amekuwa akitoa nyimbo kali kila kukicha licha ya kukaa kwenye tasnia kwa muda mrefu sasa.

Alitambulishwa na nyimbo Huyu na Yule, Fid Q. Com na Binti Malkia. Kwa zaidi ya miaka 10 ametamba kwa kuachia nyimbo zilziofanya vizuri zikiwamo I am a Proffessional, Sihitaji Marafiki, Bongo Hiphop, Propaganda, Ni Hayo Tu, Kitaaolojia na Neno.

Rapa huyu aliachia wake “Work it off” Februari mwaka huu na

Agosti 13, ikiwa ni siku ya kuzaliwa kwa mkongwe huyo,alitoa wimbo mwingine Roho ambayo amemshirikisha Christian Bella.Nyimbo hii imekuwa tofauti pia kwakuwa maudhui yake yalijikita kwenye mapenzi,hata hivyo imezidi kumpandisha chati kwenye muziki wa Hiphop.

Lady Jay Dee (1999)

Wasanii wengi wa kike maisha yao katika muziki yamekuwa mafupi kuliko kipindi cha masika…baada ya kutoa wimbo mmoja na kuchuja nao walipotea katika ramani ya muziki.

Kwa Lady Jay Dee ni tofauti. Unaweza kumwita Komando Jide, Binti Machozi au Anaconda.

Lady Jay Dee amekuwa na safari ndefu yenye mafanikio katika muziki kwa kutoa nyimbo zenye kukonga hisia za wapenzi wa burudani. Alitamba na nyimbo kama Machozi, Siwema, Binti, Umuhimu Wako, Siku Hazigandi, Natamani Kuwa Malaika, Teja, Mshika Mbili, na nyinginezo.

Akiwa na bendi yake aliyoiita Machozi alitoa nyimbo kama Nilizama na Mtarimbo.

Mwanzoni mwa mwaka huu alitoa wimbo Ndi Ndi Ndi ambao ulithibitisha Umalkia wake katika muziki wa Bongo Fleva nchini. Mwezi ulipita alitoa wimbo mwingine Sawa na Wao unaendelea kufanya vizuri katika chati za muziki nchini.

Mr.Blue (2003)

Albamu 2

Mr Blue

Yote Heri

Kutokea enzi za Blue Blue adi leo Mboga Saba msanii huyu ameendelea kung’ara katika muziki wa Bongo Fleva. Licha ya kuwa na tabia ya kutulia kidogo kutoa ngoma lakini lazima isumbue kwenye Chati mbalimbali za muziki.

Nyimbo zilizomuweka kwenye orodha ya wanamuziki waliofanya vizuri muda mrefu ni pamoja na Mapozi, Tabasamu ,Tilalila, Baki na Mimi na Pesa.

Baada ya kuachia wimbo ya Mboga Saba aliomshirikisha Ali Kiba Juni mwaka huu, amekuwa gumzo kila kona ya mtaa na kuzidi kumpa mashabiki wengi, pamoja na shoo ikiwamo Fiesta.

Wimbo huo ulishika nafasi ya pili kwenye chati 20 Bora chati za Radio Clouds wiki iliyopita.

Prince Dully Sykes (1999)

Historia ya Kweli (2003)

Handsome (2004)

Hunifahamu (2005)

Aliwahi kutamba na nyimbo nyingi kama Julieta, Dhahabu, Nyambizi, Hi, Asha Mapromise, Salome,

Unaweza kusema ni msanii anayeendana na nyakati na mabadiliko ya muziki ili kukidhi matakwa ya mashabiki wake.

Baada ya kimya cha muda mrefu Dully ameibuka na wimbo mpya “Inde” aliomshirikisha msanii kutoka kundi la WCB, Harmonize.

Wimbo huu umepata mafanikio makubwa ikiwa na historia ya kupigwa katika vituo vya televisheni vya kimataifa kama vile MTV Base, Hip TV, Sound City na Muziki.

Profesa J (1994)- Machozi Jasho na Damu

Mapinduzi Halisi

J.O.S.E.P.H

Alunta Kontinua

Licha ya kuwa mbunge wa Jimbo la Mikumi, Mwanahiphop Joseph Haule maarufu kwa jina la Profesa J ni moja ya wasanii ambao wana wamedumu katika tasnia ya muziki. Kwa miaka zaidi ya 15 hajaacha kutoa nyimbo ambazo zimekuwa na mashiko kulingana na muda.

Alianza na kundi la Hard Blasters na kuachia albamu Funga Kazi iliyobebwa na wimbo maarufu Chemsha Bongo.

Siyo zali la mentali kwa msanii huyu kuzidi kung’ara, alitoa nyimbo kadhaa ambazo kwa kipindi hicho zilibamba kama Zali la Mentali, Hapo Vipi, Nikusaidiaje na Sauti ya Ghetto.

Baada ya kutoa wimbo na Diamond Platinumz Kipi Sijasikia mwaka 2014, Alidhihirisha kuwa umahiri wake na kuwa siyo bahati wala ngekewa.

Miezi miwili iliyopita aliachia wimbo wa mahadhi ya Singeli, Kazi Kazi akimshirikisha Sholo Mwamba. Wimbo huo unafanya vizuri katika chati mbalimbali nchini.

Ay (1996)-

Raha Kamili

Hisia Zangu

Habari Ndio Hiyo

Ni msanii asiye na makuu lakini kazi zake zinamtambulisha vilivyo. Ndiye mwasisi wa kufanya kazi na wasanii wa kimataifa kabla kijiti hicho hakijapokelewa na Diamond Platnumz.

Alianza muziki mwishoni mwa miaka ya 1990 akiwa na kunzi la S.O.G. Raha Tu, Raha Kamili, Machoni Kama Watu, Binadamu, Mikono Juu ni baadhi ya nyimbo zinazotambulisha ukali wake.

Ay ameshirikiana na wasanii wengi wa kimataifa akiwamo Morice Kirya, Prezzo, Jose Chameleone, Bebe Cool, Lamyia, Miss Triniti, Lil Romeo, Sean Kingston na wengine wengi waliomshirikisha katika nyimbo zao.

Mbali na kutoa nyimbo zake, AY amekuwa akishirikiana na swahiba wake Mwana FA kutoa nyimbo kali karibu kila mwaka ambazo zimeendelea kuwaweka kwenye chati.

Baadhi ya nyimbo hizo ni Nangoja Ageuke, Usije Mjini, Bila Kukunja Goti na Naongea na Wewe.

Mwana FA (2000)- Mwanafalsafani

Toleo Lijalo

Unanitega

Anajulikana kwa mashairi ya kusifu wa warembo mpaka akajipachika jina la Binamu. Mabinti Dam Dam, Yalaiti, Kiboko Yangu, Unanitega, Hawajui Tulipotoka ni baadhi ya nyimbo za mapenzi zinazompa ufalme wa mashairi makali ya mapenzi.

Mwanzoni mwa miaka ya 2000 ndipo jina Mwanafalsa lilipoanza kuchomoza baada ya kuachia ngoma kali zikiwamo Ingekuwa Vipi, Alikufa kwa Ngoma, Tuliza Boli, Sitoamka, Mabinti Dam Dam, Bado Nipo Nipo, Binamu13 na nyingine nyingi kutoka katika albamu zake tatu.

Mwana FA ambaye alizaliwa mwaka 1984,kwa kushirikianna na rafiki yake wa karibu,Ambwene Yessaya walifanikiwa kutoa Albamu moja iitwayo”Habari ndio hiyo”,ambayo ndani yake kulikuwa na nyimbo kama Asubuhi, Nangoja Ageuke, Usije Mjini, Bila Kukunja Goti na Naongea na Wewe.