Jinsi vyama vingine vinavyoshiriki uchaguzi Kinondoni/Siha

Muktasari:

  • Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) ilitangaza uchaguzi wa Februari 17 na wagombea kutoka vyama 12 walichukua fomu za uteuzi na kuzirejesha kwa Msimamizi wa Uchaguzi wa jimbo la Kinondoni, wanne walifanya hivyo katika Jimbo la Siha.

Ikiwa zimebaki siku 10 kabla ya uchaguzi mdogo katika majimbo ya Siha, Kilimanjaro na Kinondoni, Dar es Salaam pamoja na kata 10 za Tanzania Bara, vyama vinane kati ya 12 vilivyosimamisha wagombea havijafanya mikutano ya kampeni.

Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) ilitangaza uchaguzi wa Februari 17 na wagombea kutoka vyama 12 walichukua fomu za uteuzi na kuzirejesha kwa Msimamizi wa Uchaguzi wa jimbo la Kinondoni, wanne walifanya hivyo katika Jimbo la Siha.

Wagombea waliorejesha fomu Kinondoni ni Maulid Mtulia (CCM), Godfrey Malisa (TLP), Johnson Mwangosi (SAU), John Mboya (Demokrasia Makini), Mwajuma Milando (UMD), Mary Mpangara (DP) na Rajab Juma (CUF).

Wagombea wengine ni Mwalimu Salum (Chadema), Mohamed Majaliwa Mohamed (NRA), George Kristian (CCK), Bashiri Kiwendu (AFP) na Ally Abdallah (ADA).

Hata hivyo, Pamoja na wagombea hao kuingia katika kinyang’anyiro hicho, wengi wao hawajaonekana wazi kwenye mikutano ya kampeni zao kulingana na ratiba zao.

Kwa zaidi ya wiki mbili sasa kulingana na kampeni zinazoendelea ushindani unaonekana kati ya wagombea wa vyama viwili pekee kwa upande wa Kinondoni, Mtululia wa CCM na Salimu Mwalimu wa Chadema. Mgombea wa CUF, Rajabu Salim na wa TLP, Godfrey Malisa wanafuatia kwa mbali.

Kwa upande wake CUF mgogoro uliopo ndani yake unaonekana umeendelea kukitafuna na mpaka sasa chama hicho, licha ya upande mmoja kusimamisha wagombea katika majimbo yote mawili, Kinondoni na Siha, upande mwingine unaunga mkono wagombea wa Chadema kupitia Ukawa.

Mgombea wa CUF Kinondoni, Rajab Salim ambaye alikuwa Meneja Kampeni wa Mtulia mwaka 2015, mara chache ameonekana katika majukwaa akifanya kampeni.

Katika moja ya mikutano yake, mgombea huyo anasema akichaguliwa atahakikisha Serikali inatenga fedha za chakula cha wanafunzi shuleni.

Katika moja ya mikutano yake ya kampeni katika eneo la Hananasif aliahidi kuwa akichaguliwa atasimamia suala la elimu kwa kuhamasisha Serikali kutenga bajeti ya chakula kwa wanafunzi wa shule za msingi.

Pia mgombea huyo amewahi kunukuliwa akisema kuwa atashughulikia kuondolewa gharama za kuhifadhi maiti mochwari kwa kuwa wananchi wanaingia gharama kubwa za matibabu na mazishi.

Wakati mgombea huyo akichanja mbuga, viongozi wengine wa CUF wa ngazi mbalimbali wanaendelea kumpigia kampeni Mwalimu wa Chadema chini ya mwavuli wa Ukawa.

Mwenyekiti CUF Wilaya ya Kinondoni, Juma Mkumbi amewataka wananchi wa jimbo hilo kuhakikisha wanachagua mgombea Mwalimu, baada ya aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo, Mtulia kuwatia aibu kubwa ya kujiuzulu ubunge na kujiunga na CCM, kisha kuomba tena nafasi hiyo.

Nkumbi anasema wameamua kumuunga mkono mgombea wa Chadema na ana imani atashinda.

Vyama vingine kimya

Mgombea wa TLP, Dk Godfrey Malisa licha ya kwamba alionekana moja tu akijinadi, yeye anasema amefanya mikutano mingi ila waandishi ndio hawajamuona.

Mathalan, Jumamosi wiki iliyopita Dk Malisa alipaswa kufanya kampeni katika Kata ya Makumbusho lakini waandishi wa gazeti hili walipofika katika eneo ulikopaswa kufanyia mkutano huo hakuwapo na kukuwa na maandalizi yoyote ya kampeni.

Alipopigiwa simu alisema yuko katika msiba wa Kingunge Ngombale-Mwiru na kwamba angekwenda baada ya muda mfupi.

“Tulieni sisi ndiyo wenye kampeni, wasiwasi wa nini tunakuja hapo,” hata hivyo ilipotimu saa 12 jioni ambapo ni mwisho wa mkutano mgombea huyo na timu yake hawakutokea.

Akizungumza katika mkutano wa kampeni uliofanyika eneo la stendi ya zamani Mwenge, Dk Malisa amesema hawezi kufanya kitendo alichokifanya mgombea wa CCM, Maulid Mtulia aliyejivua uanachama CUF na kupoteza ubunge wa Kinondoni.

Dk Malisa alisema hasara itakayotokea katika uchaguzi huo ni kwa sababu ya Mtulia, hivyo safari hii achaguliwa yeye (Dk Malisa) ambaye hatadhalilisha wana Kinondoni kama alivyowafanyia mbunge aliyejiuzulu.

Alipoulizwa kwa nini amefanya mkutano mmoja mpaka sasa, mgombea huyo anasema chama chake kinaendelea na kampeni kama kawaida baada ya kuzindua Februari Mosi eneo la Mwenge.

“Tumefanya mkutano Mwenge, Tandale, Makumbusho stendi, Kata ya Ndugumbi. Tatizo lenu nyie waandishi tukiwaita hamji badala yake mnapendelea vyama vikubwa tu.

“Pia tunafanya kampeni za nyumba kwa nyumba, yaani mtu na mtu kuhakikisha tunapata kura za kutosha zitakazosaidia kuibuka kidedea,” anasisitiza.

Ukiachana na vyama hivyo, wagombea wengine wa vyama vya SAU,UMD, DP, NRA, CCK, ADA-Tadea, AFP na Demokrasia Makini hawajaonekana katika kampeni za wazi licha ya kudhibitisha ushiriki wao katika uchaguzi huo.

Baadhi ya wagombea hao wanasema sababu kuu ni kukosa fedha za kufanyia kampeni huku wengine wakidai kubadili mbinu za kampeni na kujikita katika kampeni za nyumba kwa nyumba.

Mgombea wa SAU, Johnson Mwangosi anasema ukimya wake kuhusu kampeni umesababishwa na kutokuwa na rasilimali fedha za kuendesha shughuli hiyo.

Hata hivyo, Mwangosi anaongeza kuwa SAU, haijakata tamaa badala yake inaendesha kampeni zake za nyumba kwa nyumba ili kuwafikia wa wakazi wa jimbo hilo na hatimaye kupata kura za kutosha.

“Rasilimali watu ipo lakini fedha ni tatizo hasa kwa sisi wenyewe vyama vidogo. Hali inatukwamisha sana, hivi ninavyoongea na wewe nipo Magomeni hapa nafanya kampeni ya nyumba kwa nyumba na timu yangu ya watu watano,” anasisitiza Mwangosi.

“Kama huna fedha kufanya kampeni ya mikutano ya hadhara ni utata sana. Hata hivyo nimepanga kufanya kampeni ya mkutano wa hadhara Februari 14 na 16.”

Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasi Makini Wilaya ya Kinondoni, Costantine Kibonde anaungana na Mwangosi kuwa vyama ambavyo havina ruzuku vinapata shida kuendesha kampeni zake kwa ufanisi ikiwamo mikutano ya hadhara.

“Bado tunasuasua katika kampeni za majukwaani kutokana na kukosa fedha. Ndiyo maana tumejikita kampeni za nyumba kwa nyumba ambapo pia tunapata fursa za kuona na watu wa kada mbalimbali na kueleza sera zetu,” anasema Kibonde.

Kibonde anasema mara kadhaa viongozi wa chama hicho huchukua jukumu la kuchangisha fedha kwa ajili ya kampeni ya mkutano wa hadhara lakini ikifika tarehe husika hujikuta hawafikii lengo.

Hata hivyo, Kibonde anasisitiza kuwa hawajakata tamaa badala yake wataendelea kujikita na kampeni za nyumba kwa nyumba kwa kuwa zina mwitikio mzuri kwao.

Yaleyle jimbo la Siha

Kwa upande wa Jimbo la Siha ambalo linafanyika uchaguzi wa ubunge na udiwani katika kata tatu za jimbo hilo, nako mchuano mkali zaidi umeonekana kati ya CCM na Chadema.

Vyama vinne ambavyo ni CCM, Chadema, CUF na Sauti ya Umma (Sau) vimesimamisha wagombea ubunge, lakini Chadema na CCM ndivyo vinavyoonekana kukamiana zaidi.

Chadema kimemsimamisha Elvis Mossi wakati CCM kimemsimamisha aliyekuwa Mbunge wa Jimbo hilo, aliyejiuzulu na kujiunga CCM, Dk Godwin Mollel.

Hoja kuu ya kampeni katika vyama hivyo imejikita katika kujiuzulu kwa Dk Mollel, huku Chadema kikiwaaminisha wananchi ni usaliti wa hali ya juu wakati CCM kikishawishi kuwa ni chaguo sahihi.

Mpaka sasa CUF haijazindua rasmi kampeni zake kumnadi mgombea wake Tumsifuel Mwanri. Kwa mujibu wa ratiba ya chama hicho, wiki hii mwenyekiti wa CUF, Profesa Lipumba atazindua rasmi kampeni.

Chama cha Sauti ya Umma (Sau) kwa upande wake kimemteua Azaria Mdoe kupeperusha bendera yake ingawa naye hadi jana alikuwa bado hajaonyesha cheche katika uchaguzi huo.

Imeandikwa na Tausi Mbowe, Daniel Mjema na Bakari Kiango.