Julie Gichuru: Mjasiriamali na mwanahabari mahiri

Muktasari:

  • Hivi sasa anajihusisha na uzalishaji wa vipindi vya televisheni kupitia kampuni yake ya Arimus baadhi ya vipindi anavyoandaa ni pamoja na vile vya masuala yanayotokea ulimwenguni (current affairs), mahojiano na viongozi wa Afrika na kipindi cha Shinda Washinde.

Unapowazungumzia wanawake wenye mafanikio Afrika Mashariki huwezi kuacha kulitaja jina la Julie Gichuru. Ni mjasiriamali na mwanahabari mahiri nchini Kenya anayejihusisha na biashara mbalimbali ikiwamo duka la mavazi mtandaoni na mmiliki wa kampuni ya Arimus.

Hivi sasa anajihusisha na uzalishaji wa vipindi vya televisheni kupitia kampuni yake ya Arimus baadhi ya vipindi anavyoandaa ni pamoja na vile vya masuala yanayotokea ulimwenguni (current affairs), mahojiano na viongozi wa Afrika na kipindi cha Shinda Washinde.

Miaka 15 katika masuala ya habari imekuwa ya mafanikio kwake. Kati ya 2000-20002 aliendesha Jarida la Quest kabla ya kuhamia katika utangazaji wa redio alipofanya kazi ya kutangaza taarifa ya habari katika redio Capital kabla ya kuhamia katika televisheni.

Mafanikio yake katika televisheni yanaonekana katika vipindi mbalimbali alivyovianzisha ama kuviendesha.

Akishirikiana na wafanyakazi wenzake katika kituo cha televisheni, Citizen walianzisha kipindi cha Sunday Live ambacho ni maarufu na hutazamwa na watu wengi hivi sasa Afrika Mashariki.

Anasema kipindi hicho kilichoanzishwa mwaka 2008 kilileta mapinduzi katika uwasilishaji wa habari nchini Kenya.

Mafanikio yake mengine katika televisheni yalionekana mwaka 2009, alipoanzisha kipindi cha Fist to Five for Change, kilichoratibu makubaliano ya kuponya majeraha ya machafuko yaliyotokea baada ya uchaguzi wa mwaka 2008 nchini humo.

Jina lake lipo katika mafanikio ya vipindi mbalimbali vinavyorushwa na na kituo cha televisheni KTN na NTV vyote vya Kenya.

“Kuanzia kipindi cha kwanza cha uchunguzi, The Inside Story kinachorushwa KTN na vingine vya habari nilishiriki kuvianzisha,” anasema.

Akiwa katika kituo cha NTV alishiriki kuanzisha na kutangaza vipindi vya Showdown, On the Spot, You the Jury, The People’s Voice na Voices of Reason.

Taasisi ya The Footprints Africa Foundation (FAF) iliyoanzishwa na Anthony (mumewe) na Julie Gichuru ikiwa na lengo la kuielimisha juu juu ya ustawi wake nchini Kenya ni moja ya mafanikio ya mwanamke huyu katika kuwawezesha Wakenya.

FAF inasaidia kuzalishwa kwa vipindi vya Great Debaters Contest na Africa Leadership. Vipindi vyote huzungumzia na kubadilishana mawazo juu ya changamoto na fursa zilizopo Afrika.

Taasisi hiyo pia imesaidia kampeni ya Natembea iliyoanzishwa na kundi la vijana liitwalo Gisma Group.

Kikundi hiki hushiriki kutoa elimu juu ya masuala ya usafi na kugawa viatu kwa watoto wasio na uwezo.

Mbali na mfanikio katika biashara na kazi, ni mwanamke anayeipenda familia yake.

Ameolewa kwa mjasiriamali mwenzake Anthony Gichuru na ana watoto watano.

“Pamoja na kila kitu nina wajibu wa kulea na kukuza kizazi kipya, wajibu huu unaanzia katika familia,” anasema.

Kuwa na watoto watano pia kumemfanya avutiwe na masuala ya afya uzazi na ni balozi wa AMREF akisimamia kampeni ya Stand Up for African Mothers yenye malengo ya kuwafundisha wakunga 15,000 Afrika Mashariki.

Utambuzi, Tuzo na Fellowships

Martin Luther King Salute to Greatness 2008

Julie ndiye mwanamke wa kwanza kupokea tuzo Martin Luther King Salute to Greatness kwa kuzungumzia jinsi ya kutuliza ghasia bila kutumia nguvu baada ya uchaguzi wa mwaka 2007 nchini Kenya.

Fellow of the Africa Leadership Initiative & Aspen Global Leadership Network 2008

Kiongozi kijana duniani

Julie aliteuliwa kama kiongozi kijana duniani katika mkutano wa dunia wa Uchumi (World Economic Forum) mwaka 2010.

Tuzo ya Order of the Grand Warrior

Mwaka 2011 alitunukiwa tuzo ya Order of the Golden Warrior na Rais Mwai Kibaki kutokana na mchango wake kwenye ujenzi wa taifa.

Programu ya Askofu Desmond Tutu

Mwaka 2013 Julie aliteuliwa kuwa mwanakamati kwenye programu ya ya uongozi wa Askofu Desmond Tutu ambayo pia hujilikana kama Watoto wa Tutu (Tutu’s Children).

Wanawake 20 wenye nguvu Africa

Julie alitambuliwa na Jarida la Forbes kama moja wapo wa wanake 20 wenye nguvu Afrika.

Wanawake 60 Wakiafrika wenye ushawishi duniani. Mwanamke huyu alitambulika na Shirika la Wanawake kwenye Biashara ndani ya orodha ya wanawake 60 wakiafrika wenye ushawishi mkubwa duniani

Gichuru alihitimu masomo yake katika Chuo cha Harvard Kennedy School na Oxford University’s Saïd Business School.

Mwaka 2016 Julie alichaguliwa kwenye jopo la UN Foundation Global Journalist Corps, akiungana waandishi wa habari mahiri kutoka pembe zote za dunia.