KUTOKA LONDON : Chupa ya mvinyo na msosi maktaba

Muktasari:

  • Ananuka harufu ya kutooga wala kunawa muda mrefu. Alibeba mifuko mitatu. Akapanda ghorofa ya kwanza ambapo wahitaji maktaba hua na kompyuta zao kutumia huduma ya WiFi. WiFi (tamka “Waifai”) ni kifupi cha “wireless fidelity” -chombo kinachounganishwa na vingine bila kutegemea nyaya za umeme. Unapokuwa mitaani na simu yako ukawasiliana na wenzako kupitia simu unatumia WiFi. Teknolojia hii ni mzazi wa mawasiliano yetu leo.

Nilikuwa maktaba hapa London nikijisomea alipokuja Mzungu.

Tofauti na wengine. Mtu wa makamo.

Ananuka harufu ya kutooga wala kunawa muda mrefu. Alibeba mifuko mitatu. Akapanda ghorofa ya kwanza ambapo wahitaji maktaba hua na kompyuta zao kutumia huduma ya WiFi. WiFi (tamka “Waifai”) ni kifupi cha “wireless fidelity” -chombo kinachounganishwa na vingine bila kutegemea nyaya za umeme. Unapokuwa mitaani na simu yako ukawasiliana na wenzako kupitia simu unatumia WiFi. Teknolojia hii ni mzazi wa mawasiliano yetu leo.

Huduma hii ni bure maktaba za Ulaya

Hapa pia hujazana pia wanafunzi wa vidato vya sita kuendelea. Watoto wadogo zaidi wana sehemu yao chini. Na kadamnasi kubwa ya wasiokuwa na mashine hulundikana sebuleni kubwa penye tarakilishi kama 20 za bure. Unaruhusiwa (bure) saa mbili nzima kila siku. Mradi uwe mwanachama. Uanachama, kama nilivyoandika majuma machache yaliyopita, hutokana na kuwa unaishi, kihalali, kitongojini.

Sasa Mzungu wetu alipofika juu alikaa mezani, mbali kidogo na tuliokuwa tukijisomesha. Akafungua mifuko miwili. Wa kwanza ulikuwa furushi la msosi alionunua (”take away”), akauweka mezani na kisu na uma. Wazungu hawatumii sana vijiko. Kumaliza, akachopoa chupa ya mvinyo akaiweka pembeni. Hii si kawaida lakini jamaa hakujali. Ukutani pameandikwa dhahiri : kula, kunywa au kutumia simu ndani ya maktaba, marufuku. Maji ya chupa tu

Kamera za video zilizoko kila jumba la serikali (na biashara) zilishatuma taswira na punde mlinzi wa eneo akatua.

Taratibu akamweleza hairuhusiwi kunywa pombe hapa.

Jamaa akafoka ile “si pombe.”

Mlinzi akasisitiza ni pombe. Mzungu anafoka lakini mlinzi anabonga taratibu. Baadaye nilimuuliza mlinzi vipi wanawadekeza watu wa aina hii? Niliwahi kumwona mvuta bangi akitukana ovyo na kusumbua wasomaji. Mlinzi na wakutubi wakabadilishana naye matarakimu kwa upole. Mlinzi akanifafanulia:

“Hatuwezi kujua hali zao zikoje. Labda wana matatizo ya akili. Labda wagonjwa. Lazima tuwe tahadhari.Wakizidisha ndipo tunawaripoti sehemu zinazohusika kwa uchunguzi zaidi...”

Majuma machache yaliyopita niliandika kuhusu namna maktaba za Majuu zinavyohudumia jamii. Suala la ukosefu wa maktaba nyumbani liliwahi gusiwa na marehemu Profesa Chachage S Chachage. Alidai wajenzi wa majumba na sehemu za burudani wako tayari kujenga mabaa zaidi “kuwalewesha wananchi kuliko kuwaelemisha.” Viongozi wetu wanaporarua vichwa kujaribu kutatua matatizo ya umaskini, maradhi na uhalifu wanabidi kuelewa jamii inapoelemishwa hutulizana.

Afrika inasomesha asilimia kumi ; iliyobakia 80% hurandaranda mitaani na vijijini kujikidhi. Ndiyo maana omba omba, majambazi, walevi, nk wanazidi kujaa.

Kwa Ulaya ufukara unakuja kwa ukosefu wa makazi. Wiki hii benki ya Uswisi, UBS, ilitaarifu, London ni jiji la pili duniani kwa nyumba ghali za kupanga au kununua. “Ongezeko limepaa asilimia 25 katika miaka miwili...”

Haina maana Ulaya na nchi zilizoendelea hazielemishi. Ila kiasi cha hohehahe kinabanwa na hali ngumu ya uchumi na ulafi, uroho na ubinafsi wa matajiri.