Kadi za mkopo ni fursa ya kukuza ujasiriamali, uchumi

Wakati Serikali ikichukua hatua kuimarisha sekta ya fedha inayotakiwa kuwawezesha zaidi wajasiriamali kufanikisha kuelekea uchumi wa viwanda, ni muhimu kila mwananchi akajitathmini kama anakopesheka.

Inaweza isitoshe kufahamu kama unakopesha bali kiasi gani unaweza kukipata kutoka kwa zaidi ya benki na taasisi za fedha 58 zilizopo nchini.

Baada ya kusuasua kwa utoaji wa mikopo mwaka jana kulikochangiwa kwa kiasi na ongezeko la mikopo isiyolipika, Benki Kuu (BoT) imezitaka benki za biashara na taasisi za fedha kuweka mkakati utakaohakikisha mikopo hiyo inapungua huku ikihamasisha ukopeshaji kwa sekta binafsi.

Kuonyesha uwezekano wa suala hilo, tayari riba ya dhamana za Serikali imeshuka jambo linalomaanisha uwapo wa fedha za kutosha kuwakopesha wajasiriamali wa sekta tofauti za uchumi nchini.

Licha ya uwapo wa benki nyingi nchini, bado idadi ya Watanzania wanaotumia huduma zake ni ndogo. Ripoti ya Sekta ya Kuendeleza Huduma za Fedha Tanzania (FSDT) ya mwaka jana inaonyesha ni asilimia 17 tu ya wananchi wanatumia huduma hizo huku wachache zaidi wakikopesheka.

Miongoni mwa changamoto zinazowakimbiza wengi kukopa kutoka kwenye taasisi hizo ni urasimu uliopo katika kukamilisha taratibu zilizowekwa ikiwamo sharti la kuwa na dhamana na ujazaji wa fomu kadhaa. Changamoto hizi zilichangia ama kushuka kwa faida au kupata hasara kwa benki nyingi nchini kwa mwaka 2017.

Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Afrika (BoA-Tanzania), Wasia Mushi anasema faida ya benki hiyo mwaka jana ilishuka mpaka Sh5 bilioni ikilinganishwa na Sh5.6 bilioni iliyopatikana mwaka 2016.

“Mwaka jana tulipata faida lakini haikuwa ile tuliyojiwekea katika malengo yetu,” anasema Mushi na kuongeza “Mwaka huu tumejipanga kutengeneza faida ya Sh6.5 bilioni.”

Kuongeza mikopo kwa wajasiriamali, benki hiyo inasema itatoa kipaumbele kwa sekta za madini, viwanda, kilimo na usafirishaji. Serikali inapigia chapuo uanzishaji na uendelezaji wa viwanda wakati kilimo kikiajiri Watanzania wengi zaidi.

Kadi za mkopo

Kukabiliana na baadhi ya changamoto zinazowakwaza wananchi kukopa kutoka benki za biashara, matumizi ya teknolojia hayaepukiki. Kwa miongo kadhaa sasa tangu huduma za fedha zilizpoanza kuenea nchini, katikati ya miaka ya 1990, mabadiliko kadhaa yameshuhudiwa.

Mwanzoni, wateja walikuwa wanatumia kitabu cha benki (bank passbook) kuweka au kutoa fedha. Ilikuwa ni lazima uhudumiwe ndani kwa chochote unachohitaji lakini maendeleo ya sayansi na teknolojia ikaviongoa vitabu hivyo. Sasa wengi wanazo kadi.

Kumbukumbu zinaonyesha Benki ya CRDB ilikuwa ya kwanza kutoa kadi hizo kwa wateja wake. Ilikuwa Mei 2002 ilipotambulisha Tembocard. Ikiwa na miaka sita tu tangu ianzishwe, ilichochea mapinduzi ya kurahisisha huduma kwa wateja.

Kutokana na mvuto wake kwa wateja, benki nyingine nazo ziliiga na sasa wateja wote wa benki za biashara nchini wanatumia ama kadi za Visa au Matser. Ikiwa na zaidi ya wateja milioni 1.2, Benki ya CRDB imeshatoa kadi milioni mbili kwa wateja wake.

Kama ilivyotokea miaka 16 iliyopita, Februari 21, benki hiyo ilizindua kadi mbili za mkopo ambazo ni TemboCard World Reward Credit Card and TemboCard Gold Credit. Kadi hizo zinazohamasisha maisha ya kisasa, zinamruhusu mteja kukopa mpaka Sh50 milioni kulingana na uwezo wake.

Kadi za Tembocard World Reward zinawaruhusu wateja wa CRDB kukopa mpaka Sh50 milioni huku wakipewa mpaka siku 50 kurejesha mkopo huo wakati wale wa kadi za Tembocard Gold wakikopeshwa mpaka Sh20 milioni na kutakiwa kulipa ndani ya siku 45.

Kutokana na mkopo ambao mteja ataupata kupitia kadi hizi, anaweza kuchukua fedha taslimu kiasi kisichozidi asilimia 30 huku kinachobaki akitakiwa kukitumia ama kwenye vituo vya mauzo maarufu kama Point of Sales au kufanya malipo mtandaoni. Maisha ya kidijitali.

Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB, Dk Charles Kimei anasema umeandaliw autaratibu maalumu wa kuwapata wateja wa kwanza kutumia kadi hizo.

“Kama ilivyokuwa mwaka 2002, tunatarajia tutapata wateja wengi watakaozichangamkia kadi hizi ambazo iznampa mteja furs aya kukopa akiwa popote duniani. Lakini tutaanza na tulionao ambao taarifa za akaunti zao tunazo,” anasema Dk Kimei.

Kwenye uzinduzi wa kadi za kwanza, kumbukumbu za benki hiyo zinaonyesha zaidi ya kadi 400,000. Kufanikisha huduma zake, benki hiyo pia ilianzisha PoS ambazo kwa sasa zipo zaidi ya 1,000 nchini kote.

Faida

Ingawa zinafanana na kadi za kawaida kwamba zinaweza kutumika popote duniani, kadi za mkopo zina faida nyingi zaidi.

Zinampa mteja uhuru wa kununua bila wasiwasi kutokana na uhakika wa kupata mkopo ndani ya muda mfupi popote alipo na kufanikisha haja za moyo wake.

Mkurugenzi wa huduma mbadala wa Benki ya CRDB, Philip Alfred anasema kadi ya Tembocard Gold inawapa wateja uwezo wa kukopa kuanzia Sh500,000.

“Kila mtu huwa na changamoto za fedha. Wapo wanaohitaji fedha nyingi wakati wengine wanataka kiasi kidogo tu. Kadi hizi zinawafaa hata wazazi wanaosomesha watakapokwama ada za watoto wao,” anasema Alfred.

Baada ya kukopeshwa, Alfred anasema mteja akilipa ndani ya siku 30 hatotozwa riba yoyote ila akizidisha atatakiwa kulipa asilimia 2.5 kwa kila mwezi unaozidi.

Pamoja na unafuu huo, anasema mteja hupewa taarifa ya kila mwezi kumfahamisha mwenendo wa deni lake na masuala mengine kuhusu akaunti yake.

Kama ilivyo kwenye kukopa, urejeshaji wa mkopo unaotolewa kupitia kadi hii nao ni rahisi hivyo kupunguza usumbufu wa ufutiliaji.

Wateja hawa pia hupata punguzo la bei kwenye maduka, hoteli au mighahawa mbalimbali duniani ambako wanafanya shughuli tofauti za kila siku zikiwamo sehemu maalumu za kupumzikia kwenye viwanja vya ndege.

Wadau

Kuwapo kadi za mkopo, wadau wanasema ni mwanzo wa kujenga uchumi wa kisasa. Ikumbukwe, kwa kadi hizi, Tanzania inakuwa nchi ya pili Afrika baada ya Afrika Kusini, kuwa nazo.

Mwenyekiti mstaafu wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Tanzania, Johnson Minja anasema ni suala hili limekuja wakati muafaka.

Anasema ni hatua kubwa kwa benki ya ndani kujiendesha kimataifa kwani ni jambo linalofungua milango kwa Watanzania wengi kushiriki uchumi wa dunia.

“Biashara nyingi duniani leo hii zinaendeshwa kwa mtandao na kadi hizi ndizo zinazotumika kufanya malipo. Wananchi wengi wakiwa nazo si tu wataweza kununua mtandaoni bali kasi ya kuuza pia itaongezeka,” anasema Minja.

Alizihusisha kadi hizo na kuendele akuimarika kwa Soko la Hisa Dar es Salaam (DSE) akieleza kwamba kampuni nyingi zinaendelea kujiorodhesha hivyo kuongeza ushiriki wa Watanzania.

Licha ya soko hilo la nyumbani, Minja anasema kadi za mkopo zinatoa fursa kwa wananchi kushiriki ununuzi na uuzaji wa hisa kwenye masoko yaliyoendelea zaidi duniani.

“Ununuzi wa hisa za kampuni zilizoorodheshwa soko la hisa duniani au bidhaa zake hufanywa zaidi mtandaoni. Ukiwa na credit card unaweza kuwekeza mahali popote upatakapo ukiw ahapahapa nyumbani,” anaeleza.

Zipo faida za kikodi pia kutokana na kumiliki kadi hizo. Minja anasema, kwa wafanyabiashara au wasafiri wanaonunua bidhaa nje ya nchi na kuja nazo nchini wanapaswa kurudishiwa Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) jambo linalofanywa kwa urahisi zaidi ukiwa na akaunti yenye kadi hizo.

Mhadhiri mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Omari Mbura anasema mchango wa kadi hizo kuchochea biashara na viwanda ni mkubwa sana.

Anasema kwa wafanyabiashara watakaokuwanazo, watakuwa na uhakika wa kununua bidhaa wazitakazo muda wowot ekwa kiasi wakitakacho kabla dirisha la ununuzi halijafungwa.

Hilo pia linaweza likafanyika kwa watumiaji wa bidhaa nyingi zinazopaswa kununuliw akwa pamoja iwe kwa matumizi ya nyumbani au uzalishaji viwandani.

“Ukiwa na kadi hii tayari una uhakika wa kununua ukitakacho hata kama hauna fedha nyingi kwenye akaunti yako. Unaweza kuingia mkataba wa kununua ukitakacho kutokana na kadi hii pia,” anasema Dk Mbura.