Kuna aina na njia tofauti za kupata mtaji wa biashara

Muktasari:

Mtaji ni rasilimali unazowekeza ili kuukuza na kupata faida kwenye biashara uliyoibuni na kuianzisha. Unaweza kuwa na fedha taslimu au maarifa binafsi. Zipo aina nyingi za mitaji mfano ardhi, kipaji, nguvu, mtambo au mifugo na mazao.

Kwa wiki kadhaa zilizopita tulikuwa na mada ya bilionea asiye na mtaji ambayo imefikia tamati na leo tunajikita kuangalia jinsi ya kupata wazo la biashara. Zipo njia za kukupa mtaji wa biashara kulingana na mazingira uliyomo.

Mtaji ni rasilimali unazowekeza ili kuukuza na kupata faida kwenye biashara uliyoibuni na kuianzisha. Unaweza kuwa na fedha taslimu au maarifa binafsi. Zipo aina nyingi za mitaji mfano ardhi, kipaji, nguvu, mtambo au mifugo na mazao.

Huhitaji fedha kuwa mchoraji mwenye mafanikio. Watengenezaji wa mifumo ya kompyuta wanahitaji taaluma husika kufanya biashara hiyo. Ipo mifano mingi ya biashara zisizohitaji fedha. Bila kujali aina ya mtaji, leo tutaangalia njia unazoweza kuupata unaendana na biashara yako.

Mtaji mbadala

Hapa ni pale rasilimali nyingine inapotumika badala ya fedha, lakini hufanyi hivyo badala yake unatumia nguvu zako, maarifa fulani, jina la mtu mwingine, kukopa au ubunifu.

Ubunifu ni pamoja na uzoefu au kipaji chako na uwezo binafsi uliojijengea. Watu wengi wako kwenye umasikini wakati wamezungukwa na ndugu matajiri. Amini watu wengi wametajirika kupitia ndugu, jamaa na marafiki.

Ipo mifano ya watu waliotajirika kwa mikopo. Aliko Dangote, tajiri mkubwa kuliko wote barani Afrika aliazima fedha kutoka kwa mjomba wake baada ya kugundua fursa kwenye sekta ya ujenzi. Alianza kununua saruji na kuuza. Leo hii ni bilionea. Kuomba msaada siyo udhaifu bali ni ishara kwamba unajiamini na unaaminika. Kumbuka neno ujasiriamali lina ujasiri ndani yake, hivyo huwezi kuwa na mali bila kuwa jasiri.

Jiwekee akiba

Ingawa ni changamoto kwa Watanzania wengi, ni vigumu mno kufika juu bila kuweka akiba. Wengi hatuwezi kuweka akiba kwa ajili ya malengo yetu, ila nakushauri anza leo kujifunza kufanya hivyo ukiyaendea mafanikio yako.

Usisite kuanza kidogo kwa kuweka akiba polepole mpaka ufike huko unakoenda. Tafuta kazi ya ziada au anzisha biashara au mradi wa pembeni utakaokuongezea kama kipato unachopata hakitoshi. Kupata mtaji kwa kundunduliza ni njia nyepesi ambayo watu wengi hawaioni. Ukiamua kutumia njia hii kamwe huwezi kukosa mtaji.

Hii ina maana unaanza katika hali ya chini kabisa ya kufanya kitu chochote ulichokikusudia halafu faida unayoipata unaiwekeza kwenye biashara yako. Ili kuongeza umakini unaweza ukajiuliza ni mara ngapi umeshika kiasi kidogo cha fedha ukakidharau wakati kingeweza kukusaidia.

Ili uwe tajiri lazima upate maumivu. Watu wengi hawataki kupitia maumivu hayo ndiyo maana wachache wanakuwa matajiri. Walio wengi wanapenda utukufu, lakini hawataki kubeba msalaba. Hivyo usidharau pesa ndogo uliyonayo bali fikiria kwa ubunifu jinsi ya kuizalisha.

Tafuta mbia

Wakati mwingine kutokana na mazingira uliyomo unaweza kuwa na wazo zuri la biashara, lakini ukakosa mtaji. Hapa jambo la msingi ni kuangalia namna unavyoweza kupata mtu wa kushirikiana naye ambaye anataka sehemu ya faida utakayoitengeneza.

Baada ya kuwa na wazo zuri linalotekelezeka ni jambo jema kuwashirikisha wengine watakaochanga mtaji halafu mgawane faida itakayopatikana kuliko kufa na wazo zuri moyoni.

Watanzania tuko nyuma katika kufanya biashara kwa ushirikiano tofauti na mataifa mengine. Hii ni njia inayoongeza ufanisi wa kufanikisha miradi na biashara. Kutokana na uzoefu na maarifa mtambuka yaliyopo miongoni mwenu, ni rahisi kutatua changamoto zinazowakabili.

Tafuta mgavi

Hii ni njia ya uhakika ya kupata mtaji wa biashara uitakayo. Hii hutokea pale unapomuona mzalishaji wa bidhaa fulani ambaye utaingia naye mkataba wa kuchukua bidhaa zake na kuziuza kwa makubaliano ya kurudisha fedha yake baada ya mauzo. Wapo waliotoka kwa njia hii.

Wapo mawakala wengi mtaania ambao unawaona wakiendelea kutanua. Hivi ndivyo wanavyoendesha biashara zao. Licha ya makubaliano ya kimkataba mtakayotakiwa kuyakamilisha kabla ya kuanza utekelezaji, mwisho wa siku utaiishi ndoto yako.

Zipo kampuni kubwa au wajasiriamali wadogo wanaouza kwa namna hii. Kampuni za vinywaji ni mfano mzuri, lakini wapo wasindikaji wa vyakula. Wasagaji wa unga nao ni mfano mzuri. Tafuta biashara uitakayo kisha umtafute mzalishaji wa bidhaa hiyo.

Kopa benki

Zipo taratibu nyingi ambazo huwakatisha tamaa wafanyabiashara wengi hasa wadogo na wa kati kukopa kutoka kwenye taasisi za fedha, lakini kuna njia unaweza kutumia benki zikashawishika kukukopesha hata kama hukopesheki.

Kumbuka ili benki ikukopeshe unahitaji uwe na biashara ambayo imedumu walau kwa miezi sita au zaidi. Pia, watahitaji uwe na mzunguko wa fedha unaoleweka na dhamana ambayo wanaweza kuichukua ukishindwa kulipa.

Aidha, benki watahitaji uwe umefanya usajili wa biashara yako vilevile uwe na akaunti benki na mambo mengine rasmi. Ukiwa ni vitu hivyo kabla hujataka mkopo ni hatua nzuri.

Biashara nyingi nchini zinaendeshwa kiholela. Benki hazitaki wafanyabbiashara wa namna hiyo. Weka utaratibu wa kuwa na vitabu vya hesabu.

Naamini ukifanya moja ya haya niliyoyajadili hapa utakuwa umepata sehemu ya kuanzia na kuachana na fikra za kukosa mtaji zinazowazonga wengi nchini. Amua sasa.