Lianzishwe somo shuleni liitwe “Hisia za Mwalimu Nyerere”

Mwalimu Nyerere

Muktasari:

  • Pamoja na kukua kwa GDP, vilevile hutengeneza wastani mzuri wa pato la ndani kwa gawio la kichwa (GDP per capita). Matokeo ya juu zaidi ni kukua kwa uchumi na kupunguza namba ya wasio na ajira. Maana wafanyabiashara wakubwa huajiri wafanyakazi wengi kuendesha taasisi zao.

Nchi inapokuwa na akina Reginald Mengi, Said Bakhresa, Ally Mufuruki, Rostam Aziz, Mohammed Dewji ‘MO’, Yusuf Manji na wafanyabiashara wengine wengi waliofanikiwa katika daraja lao, huchagiza kukua kwa Pato la Ndani la Taifa (GDP).

Pamoja na kukua kwa GDP, vilevile hutengeneza wastani mzuri wa pato la ndani kwa gawio la kichwa (GDP per capita). Matokeo ya juu zaidi ni kukua kwa uchumi na kupunguza namba ya wasio na ajira. Maana wafanyabiashara wakubwa huajiri wafanyakazi wengi kuendesha taasisi zao.

Kuifanya nchi kubebwa na tabaka kubwa la watu wa uchumi wa kati, unahitaji idadi kubwa ya wafanyabiashara ambao watawekeza kwenye viwanda. Taifa lenye viwanda vingi vinavyofanya kazi kwa ufanisi, hukua haraka katika tabaka lake la uchumi wa kati.

Taifa lenye viwanda vingi vinavyoendeshwa vizuri kibiashara, maana yake linakuwa na mauzo mengi nje ya nchi. Ikiwa litakuwa na wastani mzuri wa GDP per capita, likadhibiti vifo vya watoto na akina mama wajawazito, likawa na kadirio bora la watu wake kuishi, hupiga hatua kwenda kuwa nchi iliyoendelea.

Faida ya viwanda ni kustawi pia kwa biashara zitokanazo na kilimo. Viwanda vitahitaji malighafi ambazo nyingi asili yake ni mashambani. Kwa Tanzania ambayo uchumi wa watu wake kwa zaidi ya asilimia 80 unategemea kilimo, uwepo wa viwanda vingi ni msingi madhubuti wa maendeleo.

Kupitia ile nadharia maarufu ambayo huzungumzwa sana bungeni kwamba “kupanga ni kuchagua”, Taifa lenye kuhitaji kujistawisha katika tabaka la kati kiuchumi (middle class), litaangalia vigezo vya kuifikisha nchi kwenye matarajio husika.

Moja ya vigezo vya kufanyia kazi ni nchi kuhakikisha inawalinda wafanyabiashara wakubwa waliopo pamoja na wajasiriamali wanaokuja vizuri (promising entrepreneurs), vilevile kutengeneza mazingira bora kwa nchi kuwa wafanyabiashara wazuri.

Hisia za Mwalimu

Hili ni somo ambalo linatakiwa kufundishwa ili Taifa liwe na idadi kubwa ya kizazi kipya cha Mwalimu Nyerere. Unaweza kufikiria Tanzania ikiwa na akina Mwalimu Nyerere 100,000, itakuwa nchi ya heshima kiasi gani?

Mwalimu Nyerere aliyekuwa mfuatiliaji na kila alipoona jambo halipo sawa alilikosoa. Nyakati za uongozi wa Rais wa pili, Alhaji Ali Hassan Mwinyi na Rais wa tatu, Benjamin Mkapa, aliikosoa Serikali kwa sababu aliamini kuwa watawala lazima wakosolewe.

Somo la Hisia za Mwalimu Nyerere likifundishwa shuleni, nchi itanufaika mno kuwa na kizazi bora chenye kuishi mfumo bora wa Baba wa Taifa. Mfumo wa kuiishi Tanzania na kuacha matokeo ya kuishi kwake.

Kusoma hisia matokeo yake ni kuambukizwa hisia zenyewe. Hisia za kutambua kuwa cheo ni dhamana, kwamba ukiwa nacho usikitumie kuonea wengine au kujitajirisha. Usithubutu kutumia dhamana yako kubagua watu kwa kutoa huduma kiupendeleo.

Hisia za Mwalimu Nyerere zikifundishwa vizuri shuleni na watu wakafaulu, kisha wenye damu ya maambukizi ya hisia za Mwalimu Nyerere wakishika uongozi nyakati zijazo, nchi itavutia kwa kuwa na viongozi ambao siyo tu kwamba wataonekana waliandaliwa kuongoza, bali kwa uzalendo wao na ujasiri wa kusimamia misingi.

Mwalimu Nyerere alikuwa mtu wa misingi. Alithibitisha hivyo alipokuwa Rais wa Tanganyika kisha Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Aliijenga nchi kwa misingi inayoeleweka na hata baada ya kuondoka madarakani alikosoa nchi kutotii misingi.

Nchi ikiwa na maambukizi makubwa ya hisia za Mwalimu Nyerere, Taifa litakuwa na kizazi kipana cha watu wenye kuwajibishana bila kuoneana aibu wala kuogopana. Ukiwa na Bunge lenye idadi kubwa ya wabunge ambao damu zao zina maambukizi makubwa ya hisia za Mwalimu Nyerere, Serikali lazima inyooke.

Hisia za Mwalimu Nyerere zifundishe utu na uwajibikaji, ukweli na uadilifu, huruma na unyenyekevu. Tuwe na watu wengi ambao wakikabidhiwa mamlaka makubwa, Taifa linakuwa halina wasiwasi, maana misingi halisi ya uongozi anakuwa amefuzu kutoka kwenye somo la Hisia za Mwalimu Nyerere.

Tuwe na kizazi kipya cha watu wenye kumuishi Mwalimu Nyerere. Nchi yenye viongozi kama Mwalimu Nyerere, watoto wao hawataishi peponi wakati wa maskini wakiwa jehanamu. Watoto wao hawatasoma shule za kimataifa na kuacha wa makabwela wakikosa vitabu na vyoo shuleni.

Taifa linahitaji watu wasio wabinafsi ambao wanaifikiria nchi kabla ya masilahi yao. Watu hao hawawezi kuonekana kipindi hiki ambacho maisha yamekuwa ya kuonyesha ufahari wa kumiliki vitu kuliko kusogeza mbele gurudumu la maendeleo ya nchi.

Pia, watu aina ya Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere, hupatikana kwa nadra sana kwenye wadi za wazazi.

Mwalimu Nyerere ambaye alikuwa na fursa ya kujitengenezea utajiri kuliko Mtanzania mwingine yeyote, lakini alikufa maskini. Watu waaminifu wa aina yake si rahisi kuwapata kwenye Serikali za Karne ya 21.

Mfanano wa Mwalimu Nyerere ni Jose Mujica ambaye alikuwa Rais wa Uruguay kuanzia mwaka 2010 mpaka 2015.

Aliiongoza nchi kwa nidhamu ya hali ya juu. Alikataa maisha ya kifahari akiwa Ikulu na aliondoka madarakani akionyesha kweli hakuiba. Kwamba kwake Urais ulikuwa kuwahudumia watu na si kujinufaisha.