Mabwawa haya kumwingizia Said Sh28 milioni

Mussa Said akijiandaa kulisha samaki wake katika mabwawa ya asili aliyochimba wilayani Mkuranga. Picha na Alawi Masare

Muktasari:

Kijana huyu mhitimu wa stashahada ya ufugaji samaki kutoka Chuo cha Uvuvi Mbegani, Bagamoyo amekuwa na malengo ya kujiajiri tangu akiwa masomoni.

Vijana wengi wanapomaliza masomo yao, wanawaza zaidi kuajiriwa. Lakini kwa Musa Saidi ni kinyume chake.

Kijana huyu mhitimu wa stashahada ya ufugaji samaki kutoka Chuo cha Uvuvi Mbegani, Bagamoyo amekuwa na malengo ya kujiajiri tangu akiwa masomoni.

Unapozungumza naye, hukosi kubaini kuwa ni kijana mwenye maono mapana kuhusu maendeleo binafsi na yale ya nchi yake.

Ni kwa sababu hii, hata alipoanza mchakato wa masomo, alitamani kusoma kitu kitakachomfanya ajiajiri na siyo kupata cheti cha kutafutia kazi.

Wakati fulani alilazimishwa na ndugu zake kuomba kazi serikalini akafanya hivyo ili kuwaridhisha, lakini alikataa kwenda kwenye usaili baada ya kuitwa. Aliamini mshahara atakaopata hautamsaidia kufikia malengo na kutimiza ndoto zake.

 

Ajikita kwenye ufugaji

Kwa sasa ameamua kujikita kwenye ufugaji wa samaki, ambao anaamini utamfikisha mahala pazuri kiuchumi, licha ya kuwapo kwa changamoto kadhaa.

Mradi huo wa mabwawa mawili anauendesha wilayani Mkuranga Mkoa wa Pwani akiwa na samaki aina ya kambare 10,000.

“ …mimi ni miongoni mwa watu walioathirika na usomaji wa vitabu. Riwaya nyingi nilizosoma zimenipa picha na ninaamini kwamba huwezi kufanikiwa kiuchumi kwa kuajiriwa. Nimeamua kutumia taaluma yangu ya ufugaji samaki kujiajiri na In shaa Allah (Mungu akipenda), siku moja nitatoka tu,” anasema Musa huku akiwalisha samaki siku Mwananchi ilipomtembelea.

Anasema mabwawa haya yanatumia maji ya asili ambayo hujaa bila kutumia nguvu nyingine kama vile pampu kuyajaza.

Kitaalamu, Musa anasema kambare hukua haraka na usimamizi wake ni nafuu kuliko aina nyingine za samaki na hilo ndilo lilimfanya achague aina hii ya samaki kwa kuanzia. Soko lake pia ni la uhakika.

Iwapo mambo yatakwenda vizuri, anatarajia kuingiza Sh28 milioni kutokana na uwekezaji wake unaokadiriwa kufikia Sh11 milioni mpaka wakati wa uvunaji. Samaki aina ya kambare huvunwa baada ya miezi sita.

 

Changamoto

Hata hivyo, Musa anakabiliwa na changamoto kadhaa ili kufanikisha malengo yake kama yalivyo katika mpangokazi alioundaa.

Kwanza, upatikanaji wa mtaji kwa ajili ya kazi yake. Kwa mfano, Musa anahitaji Sh5 milioni kukamilisha Sh11 milioni alizozikadiria kwa ajili ya uwekezaji wake wa sasa.

“Mifumo ya kibenki siyo rafiki sana kwa sisi tunaoanza na hasa ukiwa mmoja. Nilienda Mkuranga kuangalia uwezekano wa kukopeshwa lakini nikaambiwa tunatakiwa kuwa katika kikundi cha watu angalau watano. Nina hati ya eneo langu iliyotolewa na serikali ya kijiji lakini hii haitambuliki kwenye taasisi za fedha,’’ anaeleza.

Musa anasema angepata mtaji zaidi, angeanzisha sehemu ya kuzalishia samaki ili kupunguza gharama za kununulia mbegu.

 

Wito wake

Musa anatoa wito kwa Serikali, taasisi za fedha na mashirika ya misaada kuwasaidia vijana wenye ndoto na mipango ya kujiajiri, hata wakiwa mmoja mmoja badala ya kuangalia vikundi pekee. Anawataka Watanzania kujiamini, kuchangamkia fursa za kilimo ma kuzingatia ushauri wa wataalamu.

 

Historia yake

Musa ni mtoto wa mwisho katika familia yenye watoto watano. Baba yao alifariki mwaka 1996 wakabakia na mama ambaye hakuwa na uwezo hata wa kuwasomesha.

Baada ya kumaliza kidato cha nne, alichaguliwa kuendelea na masomo katika Shule ya Sekondari ya Ufundi Tanga.

Hata hivyo, hakujiunga na shule hiyo kutokana na mazingira ya kifamilia ambayo licha ya kumfanya asimudu kugharamia masomo yake, pia yalimlazimu afikirie kitu cha kumuingizia pesa za kusaidia familia yake.

Hapo akaamua kwenda kusomea ufugaji wa samaki katika chuo cha Mbegani ngazi ya cheti na baadaye stashahada chini ya usimamizi wa mjomba wake.

Mwaka 2015, Musa aliamua kufungua blogu kuhusu ufugaji wa samaki (ufugajisamaki.blogspot.com) ili kutoa habari zinazohusu ufugaji samaki.

Ukurasa huu umemkutanisha na wakulima wengi na umekuwa chanzo cha mapato kutoka kwa wakulima wanaohitaji ushauri zaidi kuhusu ufugaji samaki.

Wakati huo, rafiki zake waliokuwa na kampuni inayojulikana kwa jina la Aquaculture and Environmental Services Ltd walivutiwa na blogu yake kumuomba waunganishe nguvu.

Wakaibadili blogu yake na kuwa aquacultureservices.blogspot.com ambayo inaendelea kutoa mafunzo mtandaoni.

“Hivi tunavyozungumza nimetembea mikoa karibu yote Tanzania kwenda kuhudumia wafugaji wa samaki isipokuwa Rukwa, Katavi, Kigoma, Ruvuma na Geita. Kule Zanzibar nimewahi kupeleka mbegu za kambare 2,000 na kwa kweli bado ni jambo jipya kabisa, ‘‘ anaeleza.

 

Ufugaji wa samaki kibiashara

Samaki wanaweza kufugwa kwenye mito, maziwa, mabwawa ya asili na hata ya kutengenezwa. Ukitaka kufuga kibiashara, waone wataalamu kwa ajili ya ushauri wa kila hatua kuanzia ujenzi wa mabwawa hadi kuvuna.

0718986328