UCHAMBUZI: Maendeleo yanawezekana tukiwekeza kwa wajasiriamali

Muktasari:

Tafsiri nyingi zimeelezea rasilimali watu kuwa ni watu ambao ni mtaji wa taasisi au jamii. Watu hawa wana ujuzi, maarifa na uwezo wa kuzalisha fursa zilizo na faida kubwa na zenye kudumu kwa muda mrefu.

Mwalimu Nyerere alitufundisha kwamba ili nchi iendelee inahitaji vitu vinne; watu, ardhi, siasa safi na uongozi bora.

Kwa hali ilivyo sasa nchini, ili Taifa liendelee tunahitaji rasilimali watu au mimi nawaita wajasiriamali.

Tafsiri nyingi zimeelezea rasilimali watu kuwa ni watu ambao ni mtaji wa taasisi au jamii. Watu hawa wana ujuzi, maarifa na uwezo wa kuzalisha fursa zilizo na faida kubwa na zenye kudumu kwa muda mrefu.

Kwa wale waliojifunza uchumi na somo la kilimo ngazi ya sekondari au chuo watakumbuka, tulijifunza kwamba rasilimali za uzalishaji (factors of production) zimegawanywa katika makundi manne ambayo ni ardhi, nguvu kazi, mtaji na mjasiriamali

Rasilimali ya nne ndio rasilimali muhimu zaidi kuliko nyingine kwa sababu hufanya kazi ya kuziunganisha rasilimali ardhi, nguvu kazi na mtaji ili kukamilisha mzunguko wa uzalishaji.

Kwa muktadha huo, Tanzania hatuna tatizo la ardhi, hatuna tatizo la watu, siasa safi zinatengenezwa, uongozi bora hautoki mbinguni, unatengenezwa na mtaji pia unatafutwa na kutengenezwa.

Kinachokosekana kiasi cha kusababisha tushindwe kubadili taswira ya uchumi wetu, ni kutokuwa na kundi linaloitwa rasilimali watu au wajasiriamali.

Tumshukuru Mungu kwamba tangu uhuru tumefanikiwa kujenga Taifa la watu wamoja, watu wanaoishi kijamaa.

Kwa mtaji huu wa umoja wetu na utulivu tulionao, tuna fursa ya kuijenga Tanzania kuwa taifa kubwa na lenye nguvu kiuchumi katika bara la Afrika.

Tuanze kujenga Tanzania ya wajasiriamali wanaotegemewa ndani na nje ya mipaka yetu. Tuamue kwamba mahali popote, kwenye sekta yoyote, kila mtu afanye kazi kwa ubora wa kiwango cha juu na ubunifu.

Kinyume na hivi, tuamue kuwa taifa la watu wa kawaida; tunaofikiri kawaida, tunaopenda vitu vya kawaida na tulioamua kuishi maisha ya kawaida huku tukiogopa mawazo mapya na kukosa uthubutu.

Kwa wingi wa rasilimali za nchi hii, tunahitaji watu wenye uwezo wa kuunganisha rasilimali na fursa ili kuipata Tanzania tunayoitaka. Wajasiriamali ndio kundi linaloweza kuifanya kazi hii.

Lazima Serikali ione haja ya kuwekeza katika kundi hili, kwani ndiyo mtaji wa kutufikisha kwenye matarajio kama taifa; matarajio ya kuifanya Tanzania kuwa nchi ya uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025.

Tukipata mtaji wa wajasiriamali milioni mbili pekee, uchumi wa Tanzania utabadili taswira yake. Kupitia mtaji huu tutabuni biashara, viwanda, taasisi za kiuchumi na kijamii, tutazalisha bidhaa na huduma zenye ubora na zinazoweza kushindana katika soko la ndani na nje. Pia, tutazalisha fursa za ajira za kutosha kwa ajili vijana wanaoingia katika soko la ajira kila mwaka na tutakusanya kodi ya kutosha kuendesha bajeti ya nchi.

Ni rahisi kama kila mkoa ukatengeneza wajasiriamali wakubwa, wa kati na wadogo wanaofikia 60,000. Huu ni mtaji utakaolivusha Taifa.

Ili tujiondoe kwenye orodha ya nchi maskini duniani, tunahitaji kuwekeza kwa wajasiriamali hasa kwa kupitia mabadiliko kwenye elimu.

Tuboreshe mfumo wa elimu ili uwe zana itakayosaidia kuzalisha wahitimu watakaokuwa mtaji na siyo mizigo kwa Taifa.

Wahitimu wenye uwezo wa kujitegemea kifikra na kiutendaji; wenye uwezo wa kuona na kutumia fursa na rasilimali zinazowazunguka, wabunifu na walio na uwezo na uthubutu wa kukabiliana na changamoto mbalimbali.

Boniface Ndengo ni mjasiriamali na mtaalamu wa fedha. Simu 0784519486.