Wednesday, January 11, 2017

Magaidi wa Boko Haram wanashindwa Nigeria

Wazazi na ndugu wa wasichana zaidi ya 200

Wazazi na ndugu wa wasichana zaidi ya 200 waliotekwa na wapiganaji wa kundi la Boko Haram katika Shule ya Sekondari iliyopo Kijiji cha Chibok, Kaskazini mwa Nigeria mwaka juzi, wakiwa na huzuni wakati wa kumbukumbu ya tukio hilo iliyofanyika mwaka jana. 

By Othman Miraji ,Mwananchi

Kwa Rais wa Nigeria, Muhammadu Buhari mambo sasa yanaelekea kuwa mazuri. Yuko katika furaha. Kabla ya Krismasi iliyopita alitangaza kwamba Jeshi la nchi yake limewashinda wapiganaji wa kundi la magaidi wa Boko Haram.

Hapo kabla Jeshi la Nigeria pia lilitangaza kwamba limeliteka eneo la mwisho la maficho ya wanamgambo wa siasa kali za Kiislamu wa Boko Haram katika eneo linaloitwa Camp Zero katika Msitu wa Sambisa.

Ilitajwa kwamba Buhari mwenyewe amejivunia kuhusu majeshi ya nchi yake. Sasa juhudi zaidi zinaelekezwa kuwatafuta watoto wa kike 218 wa shule kati ya 276 waliotekwa nyara na Boko Haram.

Tatizo ni kwamba mwaka mmoja uliopita Buhari aliwahi pia kutangaza kwamba wapiganaji wa Boko Haram “wameshindwa kimbinu.”

Wakati huo, mwaka 2015 kama ilivyo sasa, mashambulio mengi yalielekezwa kwa Boko Haram. Kwa hivyo, kundi hilo la kigaidi likawa halina tena nguvu lililokuwa nazo miaka miwili kabla, kabla ya Buhari kuingia madarakani kama rais.

Mwanzoni mwa mwaka 2015 wanamgambo wa Boko Haram waliyadhibiti maeneo kadhaa ya Kaskazini Mashariki ya Mkoa wa Borno na maeneo mengi ya mkoa huo yalikuwa hayapitiki.

Kurejea kwa Msitu wa Sambisa ulioko milimani karibu na mpaka na Cameroon mikononi mwa majeshi ya Serikali kulionekana zamani kuwa ni jambo muhimu katika kuwashinda magaidi hao.

Sasa wapiganaji hao wanaelekea zaidi Ziwa Chad katika mpaka na nchi jirani ya Niger. Bonde la Ziwa Chad si eneo kubwa la msitu, lakini ni shida kulivuka. Kwa miaka mingi hakuna mtu aliyeshughulika kujenga miundo mbinu katika eneo hilo.

Kwa mujibu wa Shirika la Umoja wa Mataifa linalowashughulikia Wakimbizi (UNHCR), bado kuna karibu watu milioni 2.2 waliokimbilia katika maeneo yanayozunguka Ziwa Chad.

Hamna mtu anayezungumza juu ya kurejea nyumbani wakimbizi hao hivi karibuni. Hamna mkimbizi anayeweza kuondoka kutoka eneo hilo. Zaidi ya hayo ni kwamba hali bado si wazi juu ya usalama katika maeneo hayo.

Pia, bado si wazi bawa gani la Boko Haram lililoshindwa. Baada ya kupita miezi kadhaa ya malumbano, Boko Haram iligawanyika rasmi Agosti.

Kwa mujibu wa wachunguzi wa mambo ni kwamba baadaye mapigano makali yalitokea miongoni mwa makundi yaliyounda Boko Haram.

Kwa Wanigeria upande wa kiongozi wa zamani Abubakar Shekau ukiwa chini ya Abu Musab al-Barnawi- unajiona kuwa ni sehemu ya mtandao wa kigaidi wa Dola ya Kiislamu (IS).

Hayo ni makundi ambayo bado ni hatari na wafuasi wao bado wanafanya mashambulio ya kujitoa mhanga.

Abu Musab al-Barnawi, mwenye umri wa miaka 30 ni mtoto wa mwasisi wa Boko Haram, Mohammed Yusuf, aliyeuawa na jeshi mwaka 2009 huko Maiduguri.

Kifo cha Yusuf

Kuuawa kwa Yusuf ndiko kulikosababisha Boko Haram ianzishe harakati za chini kwa chini. Al-Barnawi alichomoza kwa mara ya kwanza baada ya kutokea mauaji huko Baga mwaka 2015, akiwa ni msemaji wa kundi hilo.

Sasa al-Barnawi anataka kuchukua nafasi ya Abubakar Shekau. Naye Shekau ametangaza kwamba kundi lake ndilo linalofuata njia sahihi na ndilo lenye nguvu.

Punde wiki iliyopita kulifanywa jaribio la mashambulio katika soko la mifugo huko Maiduguri. Katika jaribio hilo, kwa mujibu wa Jeshi la Serikali, alikufa mwanamke aliyejilipua mwenyewe. Mtu wa pili aliweza kukamatwa.

Hamna mtu anayetarajia kwamba mashambulio ya aina hii yatakoma katika muda mfupi ujao. Lakini katika vita hivi vya Serikali ya Nigeria dhidi ya Boko Haram wanawake na hasa watoto wengi, wamepata hifadhi.

Wanajiunga Boko Haram

Kuzunguka mji mkuu wa Abuja kuna wanaume waliokimbilia kutafuta hifadhi kutokana na mashambulio ya Boko Haram, lakini ni wachache.

Hali ni vivyo hivyo wakati Jeshi la Serikali linapowakomboa watu walioshikiliwa na wanamgambo wa Boko Haram.

Mara nyingi huulizwa: Wako wapi wanaume? Jibu linakosekana. Hasa wale wenye umri kati ya miaka 14 na 35?

Asilimia 70 ya wakimbizi wa ndani waliotimuliwa kutokana na mashambulio ya Boko Haram ni wanawake na watoto. Mausi Segun, anayelifanyia kazi Shirika la Haki za Binadamu la Human Rights Watch katika Nigeria anasema: “Uchunguzi wetu unaonyesha kwamba wanaume wanaandikishwa na Boko Haram kama wapiganaji au wenyewe wanajitolea kwa hiari yao kujiunga na kundi hilo.”

Kuna watu waliofaulu kulikimbia jeshi la Boko Haram baada ya kujiunga nalo. Wale wanaogunduliwa wanafanya njama ya kutaka kulikimbia jeshi hilo baada ya kujiunga nalo hupigwa risasi.

Tangu mwaka 2015 jeshi polepole limefaulu kuyateka maeneo ambayo hapo kabla yalishikiliwa na Boko Haram. Jambo hilo limefurahiwa na wakazi wa maeneo hayo, japokuwa maeneo hayo bado si salama.

Kuna shida nyingine. Nayo ni kwamba watu wanaoshambuliwa na jeshi kwa tuhuma kwamba huenda ni wapiganaji wa Boko Haram wanawekwa katika mazingira magumu vifungoni. Watuhumiwa hawaruhusiwi kuwasiliana na jama zao au na mawakili.

Katika nchi jirani ya Cameroon inasemekana watu 1000 wanaoshukiwa kuwa ni wanachama wa Boko Haram wamewekwa kizuizini. Katika jela ya Maroua, kaskazini kabisa ya nchi hiyo, kila mwezi wanafariki dunia takriban watu wanane kutokana na msongamano.

Pia, wanaume wote wasioonekana huko Kaskazini Mashariki ya Nigeria wamejiunga na kikosi cha jeshi kinachoitwa Civilian Joint Task Force (CJTF) ambacho kimeanzishwa ili kulisaidia Jeshi la Serikali.

Kikosi hicho kinafanya shughuli zake kwa siri na kinalipa Jeshi la Serikali maelezo juu ya watu wanaoshukiwa kuwa ni wanachama wa Boko Haram pamoja na maficho yao. Kuna habari kwamba kikosi hicho kina kati ya watu 26,000 hadi 27,000.

Idadi yote hiyo haifikii idadi ya wanaume waliopotea huko Kaskazini Mashariki ya Nigeria. Na hata kama mtu ataingiza hesabu ya wanaume waliofariki dunia, Human Rights Watch inasema kwamba tangu mwaka 2009, wakati Boko Haram ilipoanza kuwa kundi la itikadi kali, karibu watu 20,000 wamepoteza maisha katika vita baina ya Boko Haram na Serikali ya Nigeria.

Inakisiwa kwamba wanaume wote ambao hawajajiunga na Boko Haram au CJTF na hawako ndani ya magereza ya Nigeria wameuhama mkoa huo na kujificha.

Wasichana 218 waliotekwa

Bado nchini Nigeria na nje ya nchi hiyo kunazungumzwa juu ya wasichana 218 wa shule kutoka Chibok ambao walitekwa nyara tangu Aprili 2014 katika Mkoa wa Borno.

Kwa mara ya kwanza Boko Haram ilitangaza miezi michache iliyopita kwamba itakuwa tayari kufanya mashauriano yasiyokuwa ya ana kwa ana kuhusu hatima ya wasichana hao.

Boko Haram wanataka kubadilishana wasichana hao na wanachama wao walioko kizuizini. Hiyo peke yake ni dalili tosha kwamba Boko Haram imepoteza nguvu zake za awali.

Haina uwezo wa kufanya mashambulio makubwa, haiwezi kuviteka vijiji au kujipatia wanachama wapya. Zaidi ni kwamba wanaishiwa na fedha.

Hata hivyo, bado itachukua muda hadi Rais Buhari ashushe pumzi za mwisho na kujigamba kikweli kwamba jinamizi la Boko Haram limetoweka kabisa huko Nigeria na Afrika Magharibi kwa jumla.

Mwandishi ni mchambuzi wa masuala ya siasa za kimataifa. Anapatikana kwa baruapepe: mwinjuu@hotmail.com na maoni@mwananchi.co.tz

-->