Malezi huchangia kwenye mafanikio ya mtu kiuchumi

Muktasari:

  • Haiba ya mtu inatokana na tabia na sifa zake. Binadamu wote katika vipindi tofauti vya maisha yao hutengeneza tabia mbalimbali za kufikiri, kuhisi hata kutenda. Baadhi ya tabia hizi hutengenezwa kwa kujua, nyingine kwa kutokujua.

Wazazi au walezi wana mchango mkubwa kwenye mafanikio ya mtoto katika maisha yake ya kiuchumi. Wao, hujenga msingi wa nidhamu ya fedha.

Haiba ya mtu inatokana na tabia na sifa zake. Binadamu wote katika vipindi tofauti vya maisha yao hutengeneza tabia mbalimbali za kufikiri, kuhisi hata kutenda. Baadhi ya tabia hizi hutengenezwa kwa kujua, nyingine kwa kutokujua.

Katika utafiti wa kuchunguza athari za msongo wa mawazo, Dk Mayer Friedman na Dk Ray Roseman waliwaweka watu katika makundi mawili; haiba kundi A na haiba kundi B. Madaktari hawa waligundua kuwa hata kama kazi na aina ya maisha ingefanana, watu wa haiba kundi A wangekuwa na nafasi mara 3 kuteseka na msongo wa mawazo zaidi kuliko kundi B.

Makundi haya yamewekwa ili kukuwezesha upande uliopo. Usichanganyikiwe wala kushtuka pale utakapojikuta una tabia za makundi yote mawili, mara nyingine inaamaanisha kuwa uko vizuri kuhakikisha mambo yanafanyika inavyotakiwa au unavyotaka yawe.

Ila kama unajikuta una tabia zaidi ya nusu za kundi A, inabidi uchukue uamuzi wa kutafuta kubadilika au kubadilisha mtazamo ulionao katika maisha kabla haujajihatarishia maisha yako mwenyewe.

Haiba kundi A ni watu wenye ushindani kwa kila wafanyacho. Hutumia nguvu na kulazimishisha. Hufanya mambo yao mengi kwa haraka. Huwa na uchu wa kupandishwa vyeo na kujulikana katika jamii, hata kama hawana sifa.

Hupenda kujulikana na kuheshimiwa kwa kile walichokifanya. Hukasirishwa haraka na watu au matukio fulani. Hufoka au kuongea kwa vitisho. Hupenda kufanya mambo mengi kwa wakati mmoja.

Hutembea na kula kwa haraka. Mara nyingi huchukia wanapocheleweshwa. Hujali sana muda na hujtahidi kumaliza mambo yao kwa wakati uliopangwa. Kila wanapotakiwa kuwa hufika kwa wakati.

Haiba B siyo watu wa ushindani kazini, michezoni, masomoni au popote penye mkusanyiko. Huyakubali mazingira, hufanya vitu taratibu na kwa kufuata kanuni. Huendelea na kuchukuliana na hali ya kazi iliyopo. Huridhika na nafasi waliyonayo katika jamii.

Hawahitaji kujulikana au kutambulika katika jamii au hata katika matukio. Siyo rahisi sana kuwaudhi.

Mara nyingi hufurahia sana wanapokuwa peke yao. Ni wavumilivu. Hupendelea kufanya kitu kimoja kwa muda muafaka kabla ya kingine.

Hutembea na kula kwa utulivu. Hawakimbizwi na muda au kumaliza kazi. Mara nyingi ni wachelewaji. Nyuso zao ni za kufurahi zisizo na mikunjo.

Vyovyote haiba yako ilivyo fahamu kuwa mfano huo ulishakuwepo miaka mingi iliyopita. Labda uilivyokuwa mtoto ndiyo ilikuwa chanzo cha vile ulivyo leo. Mwanasaikolojia mmoja alipata kusema tunayoyaona kwa mtoto ni picha halisi ya ukubwa wake utakavyokuwa.

Zaidi ya asilimia sabini na tano ya yanayoendelea maishani yanachangiwa na makuzi ya utotoni. Wengi tumeharibu misingi ya kuishi na watu hivyo kujikuta tunaumizwa tangu tukiwa watoto wadogo.

Habari njema ni kwamba hakuna ulazima wa kubaki vile ulivyo, mabadiliko yanawezakana kwa kubadili mtazamo au muonekano na kuboresha ujasiri wako.

Angalia kinachosababisha mtu kujiona au kujitazama vibaya, hii itakuwezesha wewe kujua uko wapi na kwanini. Watu wa kwanza waliowahi kuwa karibu na wewe ni baba na mama yako au yeyote aliyechukua nafasi yao yaani mlezi babu, bibi, shangazi au mjomba.

Kutokana na mtazamo wao juu yako, nawe umetengeneza mtazamo wako juu yako unaoamua jinsi unavyojithamini au kinyume chake. Kwa lugha rahisi ni kwamba, unavyojiangalia ulivyo leo kunatokana, kwa kiasi kikubwa, jinsi wao walivyokuwa wanakutazama.

Kama walikuona lofa basi kuna uwezekano mkubwa nawe utajiona hivyo. Kumbuka, wapo wazazi au walezi wasio na hekima wala wema kwa watoto wao ambao huwasababishia majeraha ya mwili, hisia na akili. Uzuri ni kwamba fungu lao ni dogo.

Ingawa inawezekana kwa wazazi au walezi kusababisha majeraha kwa watoto mara nyingine pasipo kujua kwamba wanafanya hivyo, asilimia kubwa ya watoto wameharibiwa na wazazi wao.

Wazazi ambao huwalinda na kuwatetea watoto wao, wakijaribu kuwafanyia kila kitu hutengeneza watu wazima wenye utegemezi mkubwa, wasioweza kufanya kitu chochote wenyewe wala kusimama kwa miguu yao wenyewe.

Unakuta kazi za shule zinafanywa na mama, mtoto hajui hata kuoga. Hawa hata ndoa huwashinda.

Wale wazazi au walezi ambao wanaotoa mahitaji lakini hushindwa kuonyesha upendo kwa watoto wao hutengeneza kizazi kinachoamini hakipendeki, hakina mvuto, kisicho na thamani na kisichostahili kupendwa.

Baba haijalishi unatoa mahitaji yote yanayohitajika nyumbani kwako, hilo siyo pekee watoto wako wanalolihitaji kutoka kwako. Wape muda wa kuwa pamoja nao. Waruhusu wacheze nawe. Toka nao na jibu ya maswali yao. Waruhusu kuw akaribu nawe.

Watoto wanaohamishwa shule mara kwa mara, hupata shida ya kuzoea mazingira mapya na kujiona wapweke kabla hawajatengeneza marafiki wapya kitu kinachoweza kuathiri haiba kwa kuwazalishia woga au ‘inferiority complex.’