Mambo muhimu yanayoweza kusaidia kurejesha uhusiano mzuri katika maeneo ya kazi

Muktasari:

  • Kama uko kazini, licha ya uwezo na uzoefu wako, inawezekana umekuwa muathirika wa uhusiano mzuri na wafanyakazi wenzako wa chini au mabosi wanaokusimamia.
  • Je, hali hiyo imekukatisha tamaa pengine hata kuathiriwa kisaikolojia na kushuka kiwango cha uchapakazi?

Unaweza kuwa miongoni mwa maelfu ya vijana walioacha au kupoteza kazi kwa sababu ya kuharibu uhusiano wao mahali pa kazi.

Kama uko kazini, licha ya uwezo na uzoefu wako, inawezekana umekuwa muathirika wa uhusiano mzuri na wafanyakazi wenzako wa chini au mabosi wanaokusimamia.

Je, hali hiyo imekukatisha tamaa pengine hata kuathiriwa kisaikolojia na kushuka kiwango cha uchapakazi?

Baada ya hali hiyo, umegundua kuwa sehemu ya chanzo au ni changamoto ya kutokuwa sawa katika mwenendo wa wafanyakazi wenzako.

Uzoefu unaonyesha, uhusiano kazini ni ugonjwa mkubwa unaopoteza ajira za mamilioni ya wanaoamini uwezo wa kuchapa kazi au ubora wa vyeti ndiyo kila kitu.

Hata hivyo, ukweli ni kwamba, uhusiano kazini unaweza kuwa zaidi ya uzoefu, uchapakazi na ubora wa vyeti. Ni kipaumbele muhimu katika ulinzi wa ajira.

Wahusika katika uhusiano ni kundi la wafanyakazi na mabosi ambao ni wasimamizi wao mahali pa kazi.

Mazingira rafiki hunogesha molari ya mfanyakazi hatua inayoongeza uwezo wa kuzalisha kila siku.

Kama uko kazini kwa muda mrefu au utakuwa unafuatilia ajira mpya kwa sasa, ni muhimu kuangalia namna ya kulinda mazingira ya kufanyia kazi.

Katika Makala haya, tutaangalia maeneo ya viashiria vinavyoweza kusaidia kurejesha uhusiano kazini.

Dosari hazikwepeki

Kwanza ni muhimu kutambua dosari hazikwepeki kwa sababu ya mazingira ya kazini. Kwa kawaida, muda wa kufanya kazi kwa ajira za kampuni, taasisi au mashirika binafsi au ya umma, ni tano hadi saba.

Siku tano ni sawa na saa 40 kwa wiki. Kila siku kuanzia saa 2:00 asubuhi hadi saa 10:00 jioni, unatakiwa kuwa kazini,muda ambao ni zaidi ya asilimia 70 ya mawio katika siku.

Katika kampuni unayofanyia kazi, kuna wafanyakazi zaidi ya 100 ambao unatakiwa kushirikiana nao kutekeleza majukumu mbalimbali ili mambo yasonge.

Unapokuwa kazini, unakutana na watu wenye tabia, elimu, dini na mitazamo tofauti, lakini hata viwango vya kipato pia. Katika mazingira ya aina hiyo, dosari na mikwaruzano haikwepeki.

Changamoto inajitokeza katika hatua za ujenzi na ulinzi wa uhusiano, jambo ambalo limewashinda wengi.

Kwa namna yoyote, kuna jambo linaweza kumkwaza mmoja kati ya yenu, hivyo kama mtu ni muelewa, ni muhimu kujifunza namna ya kuishi katikati ya kundi la watu wa aina hiyo licha ya kwamba itachukua muda.

Fanya utafiti mdogo

Ili kurejesha uhusiano uliopotea kazini ni sawa na kufanya ukaguzi wa nyumba inayohitaji matengenezo. Lazima utambue ni eneo gani linalohitaji kufanyiwa marekebisho au ikiwezekana uanze upya kujenga msingi.

Pindi utakapotambua na kukiri kuwapo kwa tatizo, wakati huo huo unatakiwa kutambua njia sahihi ya kurejesa upya uhusiano uliopotea.

Kwa mfano, umekuwa ukipuuzwa mawazo na mipango yako unayowasirikisha wenzako ofisini, lazima utafakari kuna kasoro gani.

Hatua ya kwanza, tumia njia ya kukutana uso kwa uso na mfanyakazi mmoja kabla ya mwingine, na umuulize maswali upate majibu yake.

Kutengeneza dhana potofu ni makosa, lakini ni sahihi zaidi kutumia njia ya maswali yatakayokupatia mwanga wa kujua chanzo cha tatizo.

Matumizi ya lugha sahihi ya kushawishi katika maswali ni muhimu.

Kwa mfano, ninaweza kufanya jambo lolote linaloongeza thamani kwa mfanyakazi mwenzangu? Unaweza kuhoji, “Unaonaje mwenendo wangu hapa kazini.”

Jenga utamaduni wa kujishusha

Kuomba msamaha kwa mfanyakazi mwenzako haimaanishi kila wakati wewe ni mkosefu na wenzako ndiyo wako sahihi. Hapana! Inamaanisha ni jinsi gani una thamini uhusiano wako. Hatua ya kukubaliana na hali halisi iliyopo kwa wakati husika pia ni ishara inayoakisi amani na maridhiano na wafanyakazi wenzako.

Siyo kila jambo unahitaji kuuliza au kukosoa wakati wa mijadala. Katika hatua za kujenga uhusiano upya, ni hatari sana kujitokeza na kuzungumza.

Kila mazungumzo au maoni unayotoa mahali pa kazi, yajikite katika mtazamo chanya.

Pili, siyo kila haki unayoipoteza unatakiwa kuipigania katika hatua ya ujenzi wa uhusiano wako.

Kumbuka katika kipindi hicho, wafanyakazi watakuwa kwenye kundi linalotathmini mwenendo wa mabadiliko yako.

Kwa mfano, usitoe maoni ya kukosoa juu ya maoni ya wengi. Una haki ya kukaa kimya, lakini usionyeshe dalili au kukejeli mawazo yaliyopendekezwa na wafanyakazi wenzako kwenye mkutano.

Hatua ya kujishusha isikufanye uwe mnyonge, kumbuka haiwezi kuwa njia pekee ya kurejesha uhusiano, lakini inahitajika sana. Jaribu kujenga utamaduni wa kusikiliza, kushirikisha au kushiriki na kuuliza jambo linalohusu maisha ya kila siku kazini. Kwa mfano, michezo na matukio ya kufurahi pamoja.

Jikite katika kurejesha uhusiano

Ujenzi wa kurejesha uhusiano unaweza kuingia dosari au kuimarika zaidi wakati wowote kama itatokea hali inayohusisha mgogoro wa kampuni na wafanyakazi.

Hatua ngumu inahusu ujenzi wa uhusiano, lakini itategemeana na juhudi zako binafsi zitakazokuongezea imani. Katikati ya imani hujitokeza heshima vitu vinavyoshabihiana.

Kuwa tayari kulipia gharama

Kwa mfano, meneja wako Jenifa amekutolea mfano wa mfanyakazi asiyekuwa na nidhamu huku akimtaja mwingine ambaye ni mfano wa kuigwa. Hali hiyo isikukatishe tamaa.

Tulia na usionyeshe dalili za kumchukia kwani suala la uhusiano linahitaji muda ili wafanyakazi wenzako waweze kusahau maumivu yako.

Usilazimishe uhusiano unaohitaji, lakini wapatie nafasi wafanyakazi waweza kukuzoea kwenye uhusiano mpya. Itasaidia kuingia hatua nyingine ya kufanikisha ujenzi wa uhusiano wako mahali pa kazi.

Subiri na tazama

Baada ya kukubalika kwa msamaha wako, imani na uaminifu umeanza kurejea. Unachotakiwa kufanya ni kusubiri na kuwa mtazamaji zaidi.

Uvumilivu kwa hatua hiyo itasaidia kujenga imani na uhusiano mpya juu yako.

Fuatilia dalili za kukubalika kwa juhudi zako katika kurejesha uhusiano na angalia mapokeo ya wafanyakazi wenzako kupitia ishara na mawasiliano kwa vitendo au mazungumzo.

Linda mahusiano mapya

Baada ya kufanikiwa katika hatua zote, onyesha mtazamo chanya wakati wote ili kulinda uhusiano huo.

0716186074