Mbegu za mahindi ya GMO kumfikia mkulima mwaka 2021

Tanzania ni miongoni mwa nchi za Afrika ambazo matatizo ya mabadiliko ya tabia ya nchi, yameathiri  uzalishaji wa mazao mbalimbali ikiwamo mahindi.

Sambamba na hilo, tatizo la magonjwa ya mimea na wadudu nalo limekuwa likichangia hasara kwa wakulima wengi, hali ambayo imekuwa ikiwasababishia hasara hasa wanapokosa mbinu za kukabiliana nao.

Mwishoni mwa mwaka jana, watafiti  wa Wizara ya Kilimo,  Mifugo na Uvuvi kwa ushirikiano na  Tume ya Taifa ya Sayansi  na teknolojia (COSTECH) walipanda mahindi ya majaribio, yaliyozalishwa kwa njia ya uhandisi jeni (GMO).

Majaraibio ya  mahindi haya yanayovumilia ukame, yalifanyika katika kituo cha utafiti wa kilimo cha Makutupora mkoani Dodoma.

Utafiti huo ambao ni moja ya juhudi za kufuta suluhisho la changamoto ya ukame na mvua kidogo inayowakumba wakulima wengi wa mahindi nchini, umevuta hisia za watu wengi hususani wakulima wa zao hilo, wengi wakitaka  kujua maendeleo yake na namna wanavyoweza kunufaika na matokeo ya utafiti huo hasa upande wa mbegu.

Kila aliyefika kituoni hapo na  kujionea jinsi mahindi hayo yanayostahimili ukame yalivyostawi na kuvumilia ukame wa mkoa wa Dodoma, amekuwa na shauku ya kutaka kujua ni lini mbegu  zitawafikia wakulima, wanaopata tabu kutokana na tatizo la ukame katika maeneo mengi.

Hali inakuwa ya kukatisha tamaa pale wanapoambiwa kuwa utafiti huo unaendeshwa kwa sheria kanuni na taratibu za nchi yetu ambazo kiutekelezaji  mbegu hizo zinaweza kuwafikia wakulima mwaka wa fedha wa  2021/2022.

Dk Alois Kulaya ni mtafiti mshauri wa mradi wa mahindi yanayotumia maji kwa ufanisi (WEMA), anasema baada ya kupata takwimu  kwenye maeneo ya wakulima  watalinganisha takwimu walizozipata kwenye maeneo hayo na zile walizozipata awali kwenye kituo cha utafiti wa kilimo Makutuporana. Na endapo zitakuwa sawa ndipo wataanza mchakato ili ziweze kupitishwa kama mbegu.

Anasema wakati utafiti huo ukiendelea kwenye mashamba ya wakulima, wao kama watafiti wataanza uzalishaji wa mbegu za awali ili pale zitakapopitishwa tayari wawe na mbegu mama za kuanzia ambazo zitapewa kampuni ya uzalishaji wa mbegu kwa ajili ya kuzalisha mbegu

Mtafiti huyo anaongeza kuwa  baada  ya wao kumaliza majaribio yao mwaka 2020, wataikabidhi Taasisi ya udhibiti wa mbegu nchini (TOSCI).

Taasisi nayo itatakiwa kupanda msimu mmoja  ili kujiridhisha kama taarifa zilizotolewa na watafiti ni sawa na kisha  kuiruhusu kuwa mbegu.

‘’Baada ya kujiridhisha sasa ndio mbegu hizo bora za mahindi yanayostahimili ukame na kupambana na bungua wa mahindi zitaruhusiwa kuwa mbegu mwaka 2012/2022, ‘’ anasema.

Mahindi hayo ambayo sasa utafiti wake unaendelea nchini , kwa nchi kama Afrika ya Kusini wakulima wake tayari wameshaanza kuyalima na kuyatumia kama chakula.

Kimsingi, mahindi ya GMO  yameonyesha kuwa na  uwezo wa kutoa mavuno asilimia 14 hadi 29  zaidi kuliko mahindi ya kawaida ambayo hayakuboreshwa

Wakati wakulima wakitaka mbegu hizo kupatikana kwa haraka, watafiti wanasema kufupisha muda wa utafiti inawezekana, kwani kwa mujibu wa sheria za nchi za jumuiya ya SADC ambayo Tanzania ni mwanachama, zinaruhusu utafiti kufanyika kwenye mazingira ya nchi hizo na kisha kutumika nchi yoyote kama nchi husika itahitaji.

Calvin Gwabara ni mwandishi mwandamizi wa masuala ya kilimo Chuo Kikuu cha Sokoine cha kilimo, Morogoro. [email protected], [email protected]