TAKWIMU NA UCHUMI : Mishahara ya vibarua halmashauri inapunguza kasi ya maendeleo

Muktasari:

Zipo changamoto kadhaa zinazokwamisha utekelezaji wa majukumu ya halmashauri kwa ufanisi kubwa, likiwa ni makusanyo duni ya mapato ya ndani ambayo hayatoshi kukidhi mahitaji ya wananchi na utawala.

Kwa sasa halmashauri nchini zimeelekezwa kutenga asilimia 40 ya mapato ya ndani kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo na asilimia 10 kwa ajili ya mfuko wa vijana na wanawake.

Ibara za 145 na 146 za Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, zinaelezea uwapo wa Mamlaka za Serikali za Mitaa na Majukumu yake.

Zipo changamoto kadhaa zinazokwamisha utekelezaji wa majukumu ya halmashauri kwa ufanisi kubwa, likiwa ni makusanyo duni ya mapato ya ndani ambayo hayatoshi kukidhi mahitaji ya wananchi na utawala.

Kwa sasa halmashauri nchini zimeelekezwa kutenga asilimia 40 ya mapato ya ndani kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo na asilimia 10 kwa ajili ya mfuko wa vijana na wanawake.

Kwa msingi huo, halmashauri inabakiwa na asilimia 50 ya makusanyo ya ndani ambayo inatakiwa kuyatumia kutekeleza shughuli za kawaida zikiwamo vikao vya kisheria, mishahara na gharama za uendeshaji.

Pamoja na changamoto ya mapato zinazozikabili halmashauri nyingi, ulipaji wa mishahara kwa vibarua na watumishi, kasma ndogo za utawala, misitu na wanyamapori umeendelea kuwa mzigo mkubwa kwa mamlaka hizi. Vibarua wa ulinzi, udereva, uangalizi wa ofisi na usafi wanalipwa wastani wa Sh500,000 kila mwezi ukijumuisha na makato mengine ya kisheria.

Watumishi wanaolipwa mshahara katika kasma ndogo za utawala, misitu na wanyamapori ambao awali waliajiriwa kwa makubaliano ya kuchangia gharama zao kati ya halmashauri na Hazina.

Lakini mwaka 2014, Hazina ilijitoa hivyo halmashauri kulazimika kubeba jukumu la mishahara na makato ya kisheria kwa asilimia 100.

Wastani wa mshahara kwa kila mtumishi kwa mwezi katika kasma hizo ni Sh500,000 ikijumuisha makato mengine ya kisheria. Siyo halmashauri zote zina watumishi wanaolipwa mishahara kwa kasma hizo ndogo.

Kwa mfano, halmashauri yenye vibarua 29 inatakiwa kulipa Sh14.5 milioni kila mwezi, ambazo ni sawa na Sh174 milioni kwa mwaka.

Kama halmashauri yenye watumishi 31, inatakiwa kulipa Sh15.5 milioni kila mwezi ambazo ni sawa na Sh186 milioni kwa mwaka. Halmashauri hizi mbili zitapaswa kulipa mishahara ya Sh360 milioni kwa mwaka.

Halmashauri yenye makisio ya makusanyo ya ndani ya Sh900 milioni, ukitoa asilimia 50 ya miradi; vijana na wanawake ambazo ni Sh450 milioni itabakiwa na Sh450 milioni ambazo ukitoa Sh360 milioni ya mishahara itabaki Sh90 milioni.

Sh90 milioni zinazobaki zinatakiwa kukidhi mahitaji ya kuendesha vikao vya kisheria, mahitaji ya ofisi na gharama nyinginezo kwa mwaka jambo ambalo ni gumu kutokana na hali halisi sokoni.

Kwa mtazamo wangu, watumishi hawa wangelipwa na Serikali Kuu kupitia Hazina, ili kupunguza mzigo kwa halmashauri ambazo makusanyo yake ya ndani hayaridhishi.

Ila kama Serikali itaangalia gharama kwa tija inayozalishwa na watumishi hao na kuonekana haina madhara hata wasipokuwapo, ni vyema watumishi wa kada hizo wakapumzishwa kwa manufaa ya umma kwa kutumia taratibu na kanuni.

Kwa ushauri wangu, halmashauri ambayo iliajiri vibarua kwa mikataba isiyo ya kudumu itakuwa na mzigo wa ziada kuwahudumia hivyo, ikiwezekana ni vyema zikaacha kusaini mikataba mipya ya awali inapokwisha kwa kufuata taratibu na kanuni zilizopo. Ushauri huu ni kwa zile zinazoona uwezekano wa kulipa mishahara kwa viwango stahiki na kwa wakati zitashindwa kumudu. Kushindwa kulipa mishahara kunaendana na kushindwa kupeleka michango ya watumishi kwenye mifuko ya hifadhi ya jamii.

Namna nyingine ni kwa halmashauri, kama itaona inafaa, kutumia sekta binafsi kupata watumishi (vibarua) wa kutekeleza shughuli zake. Kwa vyovyote vile, gharama za kumlipa mzabuni binafsi haiwezi kufikia Sh14.5 milioni kila mwezi.

Tukumbuke, baadhi ya halmashauri zimegawanywa hivyo kusababisha kupungua kwa vyanzo na mapato.

Wakati wa mgawanyo wa mali na watumishi, baadhi ya halmashauri mpya hazikuchukua sehemu ya madeni ya zile mama jambo linalomaanisha ziliachiwa mzigo huo. Hali hii imezisababishia kubaki na mzigo mkubwa wa madeni na kushindwa kujiendesha vyema.

Serikali ya awamu ya tano imejielekeza katika kupunguza matumizi na kuongeza mapato kwa manufaa ya wananchi wanyonge na maskini. Ni wakati wa halmashauri kujiendesha kwa manufaa ya wananchi.

Ni vyema wakati huu wa maandalizi ya bajeti ya mwaka ujao wa fedha, suala hili likazingatiwa ili kuharakisha utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa wananchi kwa kuondoa vikwazo hivi.

Kutatua kero za wananchi kunahitaji uharaka wa kuchukua uamuzi ambao mara nyingi unawezeshwa na uwapo wa rasilimali muhimu hasa fedha.

Kukosekana kwake, siyo tu kunachelewesha bali kunawanyima walichokuwa wanastahili kukipata kwa wakati mwafaka. Naamini Serikali italiona hili na kuchukua hatua stahiki kwa wakati.