Bei ya petroli yapaa, ni ya juu zaidi katika miezi 20 iliyopita

Muktasari:

  • Kwa mujibu wa Ewura, mabadiliko ya bei za mafuta kwa  Mei 2024 yamechangiwa na ongezeko la bei za mafuta yaliyosafishwa katika soko la dunia (FOB) kwa wastani wa asilimia 3.90 kwa mafuta ya petroli na kupungua kwa wastani wa asilimia 1.31 kwa mafuta ya dizeli.

Dar es Salaam. Bei ya petroli kupitia katika bandari ya Dar es Salaam inayoanza kutumia Mei 01, 2023 ni ya juu zaidi katika kipindi cha miezi 20 iliyopita, Mwananchi limebaini. 

Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura) imetangaza bei mpya ya rejareja kwa lita ya petroli kufikia Sh3,314 ikiwa ni bei ya juu zaidi tangu Sh3,410 iliyotangazwa Agosti, 2022.

Katika kipindi hicho hakukua na bei ya juu iliyozidi hiyo wakati iliyokaribia ni Sh3,281 ya Oktoba 2023. Vilevile bei ya chini zaidi ilikua Sh2,736 ya Julai 2023. 

Kwa mujibu wa Ewura, mabadiliko ya bei za mafuta kwa  Mei 2024 yamechangiwa na ongezeko la bei za mafuta yaliyosafishwa katika soko la dunia (FOB) kwa wastani wa asilimia 3.90 kwa mafuta ya petroli na kupungua kwa wastani wa asilimia 1.31 kwa mafuta ya dizeli.

Mtandao wa Trading Economics ulionyesha bei ya mafuta ghafi kwenye soko la dunia ilipanda hadi Dola 85.4 (Sh213,500) kwa pipa moja Aprili,  ikilinganishwa na Dola 69.1 (Sh172,750)  Januari. Hata hivyo bei imeonekana kushuka kidogo Mei 01 na kufikia Dola 80.8 (Sh201,250) kwa pipa.

Wakati bei ya petroli ikipanda bei ya dizeli imeendelea kushuka na kufikia Sh3,196 kwa Mei mwaka huu ikiwa ni Sh252 pungufu ukilinganisha na miezi saba iliyopita. 

Vilevile bei ya Sh2,840 ya lita ya mafuta ya taa iliyosalia kwa miezi minne mfululizo ni chini zaidi katika miezi 21 iliyopita, ambapo Agosti 2022 ilikua Sh3,765 ambayo haijawahi kufikiwa.

Kuhusu ongezeko hilo la bei, Katibu Mkuu wa Umoja wa Wamiliki na Waendesha Vituo vya Mafuta Tanzania (Tapsoa), Augustino Mmasi akizungumza na Mwananchi Digital, leo Mei Mosi, 2024 amesema Serikali inachoweza kufanya  kupunguza  bei ya mafuta hususan petrol ni kuondoa baadhi ya  kodi na tozo kwenye mafuta.

“Usafirishaji wa mafuta upo chini  na upatikanaji wa fedha za kigeni ni changamoto, kwenye usafirishaji wa mafuta duniani meli inalazimika kuzunguka mataifa mbalimbali  kutokana na nchi nyingine kuwa na vita, hivyo huo mzunguko ni gharama” amesema Mmasi.

Jambo lingine amesema meli zinazosafirisha mafuta bima yake imepanda hivyo suluhu pekee ni kupunguza kodi na tozo za ndani.

 “Sh50 pekee ikiondolewa kwenye petroli nafuu itakayopatikana ni kubwa,”amesema.

Kwa upande wa Mkurugenzi Mtendaji wa  Chama cha Waagizaji na Wasambazaji Mafuta Tanzania (Taomac), Raphael Mgaya amesema kupanda kwa bei ya mafuta kwenye soko la dunia na uhaba wa dola ni sababu zisizozuilika, na ipo nje ya uwezo wa nchi kudhibiti.

“Bei ya mafuta imepanda juu lakini itashuka hivi ndivyo ilivyo, pia suala la uhaba wa dola ni la muda watu wavumilie hiki ni kipindi cha mpito,”amesema.

Bodaboda wanalia

Akizungumzia maumivu watakayopata, Mwenyekiti wa Waendesha Bodaboda Mkoa wa Dar es Salaam,  Michael Massawe amesema suala la bei ya petroli ni zaidi ya maumivu kwao.

“Biashara yetu inategemea kupatana na abiria sasa ni ngumu eneo ambalo amelizoea kwenda kwa Sh1,000 kumuongezea bei, hii biashara ni huria,  ukikataa kumpeleka abiria kwa sababu ya masilahi mwenzako anampeleka hata kwa hasara  unabaki hujafanya kazi, mafuta yapo juu na vipuri vipo juu maana yake maumivu kwetu ni makubwa,”amesema.

Massawe ameshauri Serikali kuangalia namna ya kupunguza makali ya mafuta,  licha ya kinachoelezwa ni sababu ya kupanda kwa dola na bei ya mafuta katika soko la dunia.