Bei ya petroli, dizeli yapaa Aprili

Muktasari:

  • Ongezeko hilo limetajwa na Ewura kusababishwa na kuongezeka kwa bei za mafuta katika soko la dunia, na kupanda kwa viwango vya kubadilishia fedha.

Dar es Salaam. Bei za mafuta ya petroli na dizeli zimepaa nchini Aprili 2024 ikilinganishwa na Machi 2024.

Kwa Mkoa wa Dar es Salaam, petroli imepanda kutoka Sh3,163 Machi hadi Sh3,257 kwa lita, huku dizeli ikiongezeka kutoka Sh3,126 hadi Sh3,210.

Hali kama hiyo pia, itakuwepo katika mikoa ya Tanga na Mtwara ambako ni vituo vya kushushia mafuta. Tanga bei ya petroli imeongezeka kutoka Sh3,209 hadi Sh3,303.

Mtwara mafuta ya petroli yatauzwa Sh3,260 kutoka Sh3,023 mwezi uliopita, huku dizeli imepaa kutoka Sh3,070 hadi Sh3,212.

Petroli itauzwa kwa bei ya juu katika Mkoa wa Kagera eneo la Kyerwa (Buberwa) kwa Sh3,495.

Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura), imesema ongezeko hilo la bei ya nishti hiyo muhimu katika uchumi limechangiwa na kuongezeka kwa bei za mafuta yaliyosafishwa (FOB) katika soko la dunia, kuongezeka kwa kiwango cha kubadilishia fedha za kigeni kwa asilimia 3.19 kutokana na ongezeko la matumizi ya Euro kulipia mafuta yaliyoagizwa.