Bei ya Petrol, Dizeli yapaa

Muktasari:

  • Bei za mafuta ya Petroli na Dizeli zimepanda, kwa mujibu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura).

Dar es Salaam. Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura) imetangaza bei mpya za mafuta ya Petroli, Dizeli na taa zitakazoanza kutumia leo Jumatano, Machi 6, 2024.

 Bei za mafuta ya Petroli na Dizeli zimepanda kwa rejareja na jumla. Mathalani, kwa Dar es Salaam petroli imepanda kutoka Sh3,051 hadi Sh3,163. Hii ni sawa na ongezeko la Sh112 kwa lita. Dizeli imepanda kutoka Sh3,029 hadi Sh3 126 sawa ongeko la Sh97 kwa lita.

Tanga petroli imepanda kutoka Sh3,064 hadi Sh3,209.

Dizeli imefikia Sh3,196 kutoka Sh3,173. Mtwara petrol imefikia Sh3,112 kutoka 3,155. Dizeli imeshuka hadi Sh3,070 kutoka Sh3,354.

Arusha petroli imepanda hadi Sh3,247 kutoka Sh3,120 na Dizeli imepungua hadi Sh3,211 kutoka Sh3,252.

Kwa mujibu wa Ewura mabadiliko ya bei za mafuta kwa Machi 2024 yamechangiwa na ongezeko la bei za mafuta yaliyosafishwa katika soko la dunia (FOB) kwa wastani wa asilimia 4.5 kwa mafuta ya petroli na asilimia 1.99 kwa mafuta ya dizeli.

Tofauti na ilivyozoelelea Ewura wanasema sababu nyingine ya kupanda kwa bei ya nishati hiyo ni matumizi ya EURO katika kulipia mafuta yaliyoagizwa.

Mataifa mengi huhifadhi zaidi Dola ya Marekani kutokana sarafu hiyo kutumiwa katika miamala ya kimataifa kwa zaidi ya asilimia 86, kitendo cha wauzaji kutaka Euro kulipwa kwa bila shaka wanunuzi wamepata changamoto au kuinunua kwa gharama kubwa sarafu hiyo ya mataifa ya Umoja wa Ulaya.

Pia, Ewura inasema bei ya sasa ya mafuta imeathiriwa na kupanda kwa gharama za uagizaji wa mafuta (premiums) kwa Bandari ya Dar es Salaam kwa wastani wa 15.38 kwa petroli na asilimia 40.41 kwa dizeli na kwa Bandari ya Mtwara kwa wastani wa asilimia 7.61 kwa petroli na dizeli.

Gharama za uagizaji wa mafuta zilitarajiwa na wachambuzi wa mambo kuwa zingeongezeka kutokana na changamoto iliyopo sasa katika usafiri kati ya mashariki ya kati na maeneo mengine ambayo yanatumia bahari ya shamu kutokana na fujo zinazofanywa na wapiganaji wa Kihouthi.