Mkwasa: Nimepania kuifanya Yanga iwe ya kimataifa kweli

Muktasari:

Mkwasa anachukua nafasi ya aliyekuwa Katibu Mkuu wa klabu hiyo, Baraka Deusdedit ambaye anarudi kwenye idara ya fedha.

Januari 31, 2017, Klabu ya Yanga ilimtangaza mchezaji wake wa zamani, Charles Boniface Mkwasa kuwa katibu mkuu wa klabu hiyo kwa mkataba wa miaka miwili.

Mkwasa anachukua nafasi ya aliyekuwa Katibu Mkuu wa klabu hiyo, Baraka Deusdedit ambaye anarudi kwenye idara ya fedha.

Kabla ya uteuzi huo, Mkwasa alikuwa kocha wa timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars aliyoifundisha kwa miezi 21.

Spoti Mikiki ilifanya mahojiano maalumu na Mkwasa kuhusu utendaji wake, soka ya Tanzania na mengine mengi.

Swali: Ulikuwa kocha kwa muda mrefu na sasa umeteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa Yanga, hili unalizungumziaje?

Mkwasa: It’s a record’ (ni historia). Haijawahi kutokea, nimekuwa mchezaji wa Yanga, nikawa kocha wa Yanga na leo hii ni Katibu Mkuu wa Yanga, haijawahi kutokea.

Nakumbuka kuna kipindi Lawrance Mwalusako alikuwa Katibu Mkuu wa Yanga, alikuwa mchezaji akawa kiongozi, lakini mimi nina matatu, mchezaji, kocha na kiongozi.

Swali: Uliwahi kufikiria siku moja utakuwa katika safu ya uongozi Yanga?

Mkwasa: Ukweli sikuwahi kufikiria hicho kitu, ndiyo sababu nasisitiza tena ‘it’s a record’ hapa nyumbani kutoka kucheza, kuifundisha hii timu kisha kuwa katibu mkuu, haijawahi kutokea.

Sikuwahi kufikiria kama Yanga itaniajiri niwe katibu mkuu, lakini kumbe wao walikuwa wakifikiria hicho kitu na walitaka mtu ambaye ana taaluma ya mpira, walianza kuchuja na kuniona ninastahili wakaja tukazungumza.

Waliponifuata sikuona sababu ya kusita kwani mpira ni kazi yangu tangu mdogo hadi sasa, hivyo sikuona ugumu wala kujivunga kwenye kibarua hicho.

Swali: Nini vipaumbele vyako?

Mkwasa: Vipaumbele vyangu viko katika makundi matatu; cha kwanza ni kuleta umoja kwenye klabu. Umoja wa wanaYanga, umoja wa wachezaji na zaidi hata katika matawi kuwe na umoja na mshikamano.

Hata kesho (wiki iliyopita) nina mkutano na viongozi wa matawi ya Yanga Mkoa wa Dar es Salaam, tunataka kuwapo na umoja, mshikamano na zaidi kuhakikisha Yanga inatwaa ubingwa.

Pili; Ninachotaka kuona ni Yanga ifike mbali na ifanye vizuri medani za kimataifa. Kumekuwa na kupoteana, kutofanya vizuri linapokuja suala la mechi za kimataifa. Ninataka Yanga iwe ya kimataifa kweli na kwa kuanza, tunatwaa ubingwa msimu huu na pia mechi zetu za Ligi ya Mabingwa Afrika.

Tatu; Kipaumbele changu kingine ni kuhakikisha benchi letu la ufundi linawezeshwa ipasavyo ili kuleta mafanikio kwenye timu na klabu.

Swali: Kulikuwa na mpango wa ujenzi wa Uwanja wa Yanga Kigamboni, ulipoingia ninaamini ulikutana na hili, umejipangaje?

Mkwasa: Ni kweli kuna huo mpango wa Uwanja wa Yanga Kigamboni lakini siwezi kulizungumzia hilo kwa kuwa silifahamu sawasawa, lakini ninachokifikiria na ambacho nimepanga kukiwasilisha kwenye Kamati ya Utendaji ni kuwa na uwanja wetu wa mazoezi hapahapa Jangwani.

Mpango niliona ni kuukarabati uwanja wetu wa Kaunda na kumwaga kifusi ili kunyanyua uwanja. Hapa huwa panajaa maji, lakini tukimwaga kifusi ninaamini kitazuia mafuriko.

Uwanja wa Kaunda ni mzuri na tutaufanyia ukarabati ili uwe na mwonekano stahiki na timu yetu iwe na sehemu nzuri ya kufanyia mazoezi. Huo ndiyo mpango ninaoufikiria kwa sasa. Timu imekuwa ikihangaika na sehemu za kufanyia mazoezi wakati uwanja upo.

Swali: Unafahamika kuwa ni mtu mwenye misimamo na huwa unaamini unachokiamini na ukiangalia mwenyekiti wako, Yusuf Manji huwa ana misimamo yake, huoni inaweza kutokea kila mmoja akasimamia anachokiamini mkakwazana?

Mkwasa: Katika msigano wa watu wawili lazima busara itumike ili kumaliza tofauti, ni kweli mimi huwa ninasimamia kile ninachokiamini.

Sitarajii itokee, kama ikitokea sitakwaruzana naye na bahati nzuri nimebarikiwa kipaji cha kumsoma mtu na kujua niishi naye vipi. Mwenyekiti ni bosi wangu sitampinga zaidi ya kumshauri pale inapostahili.

Swali: Umepanga mengi ikiwamo vipaumbele, ikitokea sasa hukutimiza na ukatimuliwa, huoni kama itakuharibia?

Mkwasa: Kutimuliwa ni kitu cha kawaida popote duniani, katika mpira ukifanya vibaya lazima utaondoka hivyo muda wote unakuwa tayari kwa hilo, vivyo hivyo na kwangu sihofii kutimuliwa maana ni vitu ambavyo tumekutana navyo na tutaviacha.

Swali: Yanga ina migogoro mingi na baadhi ya wachezaji ambao wanaidai kwa nyakati tofauti kama kocha Ernest Brandts kina Said Bahanuzi, kama katibu umejipangaje kumaliza migogoro hiyo?

Mkwasa: Ni kweli kwani nimeingia juzi juzi tu kazini nikakutana na kesi nyingi, nyingine za 2014 na nyingine chini ya hapo, ninachokifikiria ni kuzimaliza na nyingine kwa kutumia busara bila kufikishana kwenye Kamati ya Sheria na Hadhi ya Wachezaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).

“Lakini kuna nyingine mtu anaona kwa kuwa ni kiongozi mpya anataka akuingize ‘chaka’ na kuibuka kwamba anaidai Yanga Sh50 mililioni lakini hana vielelezo. Yote nimeakubali lakini fedha za Yanga hazitoki kienyeji, hii taasisi lazima kila kinachoingia kiwe na maandishi vivyo hivyo kinachotoka pia. Nimekuta deni la Bahanuzi, Coastal Union wanadai kocha Brandts huyu lazima tumlipe, hatuna namna nyingine fedha zake Dola 11,000 lakini madeni mengine hadi tujiridhishe ilikuwaje na kupata ‘evidence’ si kulipana kienyeji.

Swali:Uliaminiwa na Watanzania wakati ulipokabidhiwa timu ya Taifa lakini katika miezi 21 uliiongoza ilishinda mechi moja, sare tatu na kufungwa sita nini tatizo?

Mkwasa: Kuna matatizo matatu kwenye timu yetu ya Taifa. Mosi ni wachezaji. Kila mmoja kucheza kwa falsafa ya klabu yake, mfano Yanga itacheza kwa falsafa ya Zambia kwa kuwa wanafundishwa na kocha Mzambia, Simba itakuwa ya Cameroon na klabu nyingine zitaendelea na mfumo huohuo kulingana na makocha walionao.

Sasa kazi inakuwa kuwaunganisha kupata mfumo mmoja na ukumbuke wachezaji wetu wengi ni ridhaa. Hawana uelewa wa kutosha wa ‘profesheno’, ambao unawachukua siku tatu mnacheza mechi.

Wachezaji wetu, kabla ya kujiunga timu ya taifa wanapaswa kuandaliwa kwenye klabu zao, wanapokuja timu ya taifa kila mmoja ana falsafa ya klabu yake, hivyo kocha anatakiwa apate muda wa kutosha kuwanoa, kuwaunganisha kuwa kitu kimoja, lakini kwa bahati mbaya muda huo haupo kutokana na ligi yetu ilivyo.

Kocha unakuwa na siku mbili au tatu za mazoezi na wakati mwingine usipate kabisa na kuishia kuwapeleka kucheza mechi na kufungwa kisha kurudi na lawama zote zinakuangukia kocha…staili hii huwezi kumudu programu kwenye timu ya Taifa na hili ndilo nililolibaini nikiwa kocha wa Taifa Stars.

Tatizo lingine, hatuna mapro. Tunaye Mbwana Samatta kama mtoto wa dawa, tunamwangalia kwa macho yote, sasa huwezi kumtegemea pro mmoja…Angalia Uganda hivi sasa wametupita wanao wengi.

Swali: Kwa jinsi ulivyoziona Fainali za Afrika kule Gabon, unadhani Tanzania itacheza Afcon 2019?

Mkwasa: Kama kukiwa na msukumo wa maandalizi kwa viongozi, wachezaji na kila mdau, hakuna kinachoshindikana. Kila kitu ni maandalizi.

Wanasema kundi la Stars kwenye Afcon ijayo ni gumu lakini siyo gumu kwa upande mwingine kama maandalizi ya kina yatakuwapo kwa timu yetu, kama tuliweza kuwatoa jasho Nigeria kwenye ile mechi, walitimia japo walitufunga bao 1-0 hakuna kinachoshindikana.

Tukijitahidi tunaweza kuvuka, tunaweza kukosa nafasi ya kwanza, jamani hata nafasi ya pili hata best looser tukose?

Swali: Nini nafasi ya Serengeti Boys kwenye Afcon ya U-17 Gabon?

Mkwasa: Kama nilivyosema kwa maandalizi ya Taifa Stars kwa Afcon 2019, kwa hawa pia kikubwa ni maandalizi makini na kupatiwa mechi kadhaa ‘tafu’ za kujipima nguvu kabla ya hizo fainali, wakifanya hivyo nafasi ya kufanya vizuri ipo, kinyume na hapo yatakuwa yaleyale kwani ukiangalia tumefuzu kwa rufaa japo matokeo yalikuwa ni 3-3 Congo wakiwa wamefuzu kwa mabao ya ugenini kabla ya kuwaondosha kwa rufaa, hivyo tufanye maandalizi ya kina.

Kingine ni nguvu ya Serikali, kama ikitia mkono wake, tunaweza kuwa na nguvu na zaidi timu zibaki serikalini na TFF wawe waratibu.

Swali: Uliwahi kuwa kocha wa timu ya wanawake Twiga Stars, nini mustakabali wa soka ya wanawake Tanzania?

Mkwasa: Kama jitihada zikiendelea kufanywa na kuongezewa nguvu zaidi kwenye Ligi ya Wanawake, tunaweza kufika mbali zaidi. Inahitajika mipango madhubuti ya kuiongoza hii timu ili iendelee kufanya vizuri kimataifa.

Kama hakuna mashindano, watapotea. Kuwepo kwa ligi ya wanawake, kunawafanya kuwa bize, lakini pia wasipotezewe, TFF na chama kile cha wanawake, TWFA waitafutie mara kwa mara mechi ili wasipoteze soka yao.

Swali: Nini ambacho viongozi wengi wa mpira Tanzania wanakosea?

Mkwasa: Hili ni suala pana kidogo, lakini kinachotokea unaweza kukuta klabu ina viongozi wasiokuwa na uelewa wa kutosha katika utawala wa michezo, hili ni tatizo kwenye soka yetu na hata michezo mingine pia.

“Vilevile tatizo pia linakuja pale programu zipo lakini hakuna uwezeshwaji hii ni sawa na kazi bure katika soka.

Unaweza kuwa na mengi lakini shida ikaja padogo, fedha, ubunifu, uwezeshwaji na utawala wa soka, wengi hawana weledi huo.

Swali: Wachezaji gani ukiwaona unajidai kuwa walipitia kwenye mikono yako?

Mkwasa: Wako wengi, Mbwana Samatta mwenyewe nimemfundisha akiwa African Lyon, Simon Msuva pia na wengine wako katika timu za majeshi...Nimeanza kufundisha tangu mwanzoni miaka ya 1990, sasa ukiangalia hapo wachezaji ni wengi, wengi mno.

Swali: Una sifa zote za kufundisha soka nje ya nchi, kwa nini hupendi kufundisha nje ya Tanzania?

Mkwasa: Sijapata fursa hiyo bado, pamoja na kwamba nje ya nchi kuna changamoto nyingi. Nilikuwa miongoni mwa makocha 15 tulioomba kufundisha Zesco ya Zambia na katika mchujo tukabaki watatu.

Bahati mbaya akachaguliwa kocha kutoka Serbia. (Zesco inanolewa na kocha, Zlatko Krmpotić) Lakini bado nitaendelea kusaka fursa japokuwa ninakwazwa na mikataba. Sijawahi kuwa bila mikataba, nikimaliza huu unakuja huu na kama unavyoona, umetoka wa TFF ukaja wa Yanga…hiyo labda kwa baadaye kwa kuwa sasa siwezi mimi ni mwajiriwa wa Yanga kwa miaka miwili, labda wenyewe wakiniruhusu kufanya hivyo basi nitafanya.

Swali: Ulikuwa na madai na TFF, mmeshamalizana?

Mkwasa: Hivi leo (wiki iliyopita) ninakwenda kukutana nao kuhusu suala langu, bado hatujamalizana. Tulitengeneza hesabu wakawa wamekosea, tulirekebisha na sasa tunataka kumalizana.

Swali: Unapangaje maisha ya michezo na familia?

Mkwasa: (Anacheka), tunaendelea, mke wangu Betty ni mwanasiasa na mimi ni kocha na sasa katibu mkuu wa Yanga. Tunachokifanya ni kupanga muda wa majukumu ya kazi na yale ya familia, lakini natekeleza wajibu wangu kama baba ipasavyo na masuala ya mpira na maisha yanakwenda.